Thursday, 19 September 2013

MAGUFULI NA TAFSIRI YA NENO "PEOPLES POWER...?" YA CHADEMA

 
 
      WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli amesema kuwa anafurahishwa na salamu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa kuwa kila neno katika salamu hiyo lina maana na linaashiria ushindi.

Magufuli ameyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa sekta ya miundombinu ya barabara wa Mkoa wa Iringa, katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi za Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Christine Ishengoma.


Alisema neno ‘People’ linamaanisha Watanzania waliompigia kura Rais Jakaya Kikwete na ‘Power’ likiwa na maana ya nguvu za rais.

"Mkuu wa Mkoa wewe ni dokta, unafahamu maana ya neno People, yaani ni watu, mimi ninawapongeza sana hawa wanaosema ‘Peoples Power’, kwani neno People ni watu ambao ndiyo Watanzania waliomchagua Rais Kikwete, na Power ni nguvu, hakuna mwenye Power kama rais, maana ya Authority ni Rais Kikwete ambaye ndio tunapata miradi mbalimbali ya barabara, miradi ya umeme na Big Results Now, kwa hiyo mimi ninawapongeza sana wale wanaosema Peoples Power," alisema Magufuli.

Akizungumzia juu ya nidhamu ya fedha, Magufuli alisema kumekuwa na matumizi yasiyostahili kwa baadhi ya Halmashauri juu ya fedha za miradi ya barabara, ambapo wakurugenzi hutumia fedha hizo kulipana posho za vikao.

Aidha Magufuli alisema Halmashauri zinapaswa kuibua vipaumbele na kuvitekeleza ili kupunguza changamoto za wananchi, na kwamba Mkoa wa Iringa utapatiwa zaidi ya shilingi Bilioni 5.6, ambazo zitasaidia kuboresha miundombinu ya barabara za wilaya katika mkoa huo.

Magufuli pia aliitaka Manispaa ya Iringa kubuni barabara za pembezoni ya mji na kujenga kituo kikubwa cha mabasi yaendayo mikoani.

Aidha Dk. Ishengoma alimuomba waziri huyo kulichukulia uzito suala la upanuzi wa barabara ya Mlima Kitonga, kwa madai kuwa ufinyu wa barabara hiyo umekuwa ukichangia usumbufu mkubwa pindi magari yanapokwama na hivyo kuziba barabara hiyo na kusababisha msongamano mkubwa.
 
SOURCE: KILELE CHA HABARI