Na Daniel Mjema, Mwananchi
Posted Septemba7 2013 saa 11:40 AM
Posted Septemba7 2013 saa 11:40 AM
Kwa ufupi
Dodoma. Polisi mkoani Dodoma, wanaumiza vichwa 
namna ya kumpata Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema) 
wanayemtafuta kwa udi na uvumba kwa tuhuma za kumpiga Polisi wa Bunge.
Mbunge huyo kijana alifanikiwa kuwapiga chenga ya 
mwili(kutoroka) polisi hao waliokuwa wametanda eneo la Bunge juzi, 
mahususi kwa lengo la kumkamata lakini aliwatoroka bila wao kumtambua.
Habari za uhakika zilizopatikana jana na juzi, 
zilisema tayari polisi wamesambaza taarifa ya simu ya upepo katika mikoa
 ya jirani ya Morogoro na Singida ili wamkamate watakapomuona.
Polisi hao wa Bunge na makachero wengine, juzi 
jioni walitanda katika Viwanja vya Bunge kwa lengo la kumkamata lakini 
mavazi aliyokuwa ameyavaa mbunge huyo yakawachanganya wasimtambue.
“Unajua Polisi walikuwa wamejiandaa wakijua Sugu 
(Mbilinyi) angefika jioni kipindi cha Bunge akiwa amevaa suti aliyovaa 
asubuhi yake, lakini akaja na mavazi tofauti kabisa,”kilidokeza chanzo 
chetu.
Sugu alifika eneo hilo la Bunge juzi saa 11:00 
jioni akiwa katika gari la Kiongozi wa Upinzani Bungeni (KUB), Freeman 
Mbowe na kushiriki mkutano wa wanahabari Ukumbi wa Msekwa.
Akizungumza na gazeti hili juzi kabla ya mkutano 
huo na wanahabari, mbunge huyo alisema, tayari amepata taarifa ya kuwapo
 maagizo ya yeye kukamatwa lakini akasema yuko tayari kutetea haki yake.
“Nimeambiwa OC-CID (mkuu wa upelelezi) ametoa 
maagizo nikamatwe eti kwa kumpiga Polisi… Mimi nashangaa sana kwa sababu
 mimi ndiye niliyepigwa lakini natakiwa kukamatwa,”alisema.
Haifahamiki aliwezaje kuwatoroka polisi na 
kufanikiwa kuondoka lakini waliendelea kuganda viwanja vya Bunge hadi 
saa 3:00 usiku wakiamini bado alikuwa ofisi za Kambi Rasmi ya Upinzani 
Bungeni.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Susan 
Kaganda, jana alilithibitishia gazeti hili kumsaka mbunge huyo kwa 
mahojiano na kwamba tayari taarifa hiyo wameiwasilisha kwa Katibu wa 
Bunge.
“Ni kweli tunamhitaji kwa ajili ya mahojiano na 
kama unavyojua utaratibu unavyosema lazima uliarifu Bunge na sisi tayari
 tumemuandikia katibu wa Bunge ili amtaarifu (Mbilinyi) ili aje,”alisema
 Kaganda.
Juzi jioni wakati akiahirisha Bunge, Ndugai 
alisema mbunge huyo amefanya vitendo vya aibu kwa kumpiga kichwa na 
kumchania sare polisi mmoja wa Bunge na kuharibu kipaza sauti cha Bunge.
Wakati Ndugai akisema hivyo, jana Mbunge wa Simanjiro, 
Christopher Ole Sendeka aliomba mwongozo wa Spika kuhusu Mbilinyi 
kujichukulia sheria na kumpiga Polisi nje ya ukumbi.
Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama alisema 
atautolea maamuzi mwongozo huo baada ya kushauriana na Wanasheria wa 
Bunge na viongozi wa taasisi nyingine zinazoshabihiana na hilo.
Kiini cha kutafutwa kwa mbunge huyo ni vurugu 
zilizotokea juzi mchana ndani ya ukumbi wa Bunge baada ya Naibu Spika 
,Job Ndugai kuwaamuru polisi kumtoa kwa nguvu kiongozi wa Upizani,Mbowe.
source: Mwananchi
source: Mwananchi
