Wednesday, 11 September 2013

Mkuu wa jeshi CAR afutwa kazi

 
Imebadilishwa: 11 Septemba, 2013 - Saa 10:19 GMT
Muasi wa zamani Michel Djotodiam akiapishwa kama rais wa CAR
Mkuu wa jeshi la Jamuhuri ya Afrika ya Kati, amefutwa kazi baada ya wapiganaji wanaomuunga mkono rais aliyeondolewa mamlakani kuanzisha mapigano mapya.
Kwa mujibu wa mafisa wakuu, angalau watu 60 wameuawa kwenye mapigano hayo Kaskazini Magharibi mwa mji mkuu
 
Muasi wa zamani Michel Djotodiam, aliapishwa kama rais mpya wa nchi hiyo mapema mwezi huu baada ya wanajeshi kumwondoa mamlakani,
Francois Bozize mwezi Machi.
Umoja wa Mataifa umeonya kuwa Jamuhuri ya Afrika ya Kati huenda ikawa taifa lililoporomoka na hata kutishia amani katika kanda hiyo.
Takriban thuluthi moja ya watu 4.6 raia wa nchi hiyo, wanahitaji msaada wa chakula , makaazi , huduma za afya na maji.
Wanajeshi wanaomuunga mkono bwana Bozize wanasemekana kutwaa angalau mji mmoja tangu kuanza mashambulizi yao wiki jana.
Hii ndiyo operesheni ya kwanza kubwa wanajeshi wafuasi wa rais wa zamani wameweza kufanya, tangu kuondolewa mamlakani.
Nafasi ya Jean-Pierre Dolle-Waya kama mkuu wa majeshi itachukuliwa na Generali Ferdinand Bombayake, kulingana na taarifa iliyosomwa katika redio ya taifa.
Gen Bombayake alikuwa mkuu wa usalama wa rais wa zamani, Ange Felix Patasse, aliyeondolewa mamlakani mwaka 2003 kwa njia ya mapinduzi na bwana Bozize.
Wafanyakazi wa mashirika ya kibinadamu, wametuhumu wapiganaji wa zamani wasio na maadili kwa kupora mfumo wa afya pamoja na kuwaibia raia tangu waasi wa Seleka kuchukua mamlaka mwezi Machi.

source: BBC Swahili