Thursday 26 September 2013

Mmoja wa magaidi alizungumza Kiswahili

INGAWA duka la Westgate liko karibu dakika 15 tu kutoka nyumbani kwangu, nilikuwa nikienda kule kwa nadra kununua vitu. Mara kwa mara huwa kuna watu wengi katika duka hili katika siku za mwisho mwa wiki na hivyo niliona kama karaha. Jumamosi ilikuwa maalumu kwa sababu nilitaka kutumia muda wangu na mkwe yangu, Amina (si jina halisi) na baadhi ya marafiki zetu ambao watoto wao walikuwa wakishiriki katika shindano la upishi.


Tulikuwa juu ya ghorofa la mwisho saa 5.00 asubuhi. Shindano la upishi lilikuwa likiendelea.

Baada ya muda, Amina aliamua kuelekea chini kwa ajili ya kununua vitafunwa. Sikuwa na njaa sana hivyo niliamua kubaki hapo hapo. Nilitaka kuangalia watoto wakipika.

Karibu saa saba na robo, Amina alikuwa hajarejea nilipokuwa, lakini sikuwa na hofu na nilibakia hapo hadi niliposikia sauti ya milio ya bunduki.

Nilishikwa na kihoro na kumpigia simu mwanangu. Ni ofisa usalama na nilidhani pengine angeweza kusaidia.

“Kuna milio ya risasi hapa. Naweza kusikia milio ya risasi. Tafadhari fanya unaloweza,” nilimwambia.

Niliongea naye kwa muda mfupi kwa simu kwa sababu nilitaka kuzungumza na mkwe wangu. Katika simu aliniambia kuwa alikuwa amejificha katika benki iliyo kwenye kituo hicho cha biashara. Alisisitiza kwamba yu salama na alitaka niwe mwangalifu.

Mazungumzo yetu yalihitimishwa ghafla nilipoona watu wawili wakija juu. Walikuwa na bunduki na haikunichukua muda nikaona mabomu ya kutupwa kwa mkono yakining’inia katika mikanda yao.

Nyuso zao hazikufichwa na tuliziona wazi kana kwamba walikuwa hawajali iwapo tungeweza kuwatambua baadaye. Mara moja nilianza kuwa na wasiwasi huenda nisitoke hai.

Katika kitambo hicho, hofu yangu ilikuwa kubwa. Magaidi walipoanza kurusha risasi na magurunedi holela, umati ukaangua kilio kwa kihoro.

Watu walianza kukimbia kwa mshtuko huku mwelekeo wao ukiwa haueleweki. Nami nilikimbilia katika hema lililokuwa likitumika kama jiko la watoto na kujificha humo.

Awali nilidhani walikuwa wakifyatua risasi kwa bahati mbaya. Hata hivyo, punde nikaona kwamba wale watu waliokuwa wakikimbia huko na huko wakipiga kelele ni wale waliokuwa wamepigwa risasi. Huku kukiwa na makelele, niliwasikia magaidi wakiwaita Waislamu:

“Kama ninyi ni Waislamu, mnaweza kunyanyuka na kuondoka,” walisema.

Lakini haikuwa rahisi kama ilivyodhaniwa. Waislamu walitakiwa kuthibitisha imani yao. Walitakiwa kutaja jambo fulani kutoka aya za Korani kabla ya kuachiwa. Na hata baada ya hapo bado unaweza kupoteza maisha yako. Mwanamke mmoja ambaye alisema alikuwa Muislamu lakini hakuonekana kuwa Muislamu alipigwa risasi na kufa.

Sina uhakika kwa nini sikutumia dini yangu ili kujiokoa mapema. Pengine ilitokana na hofu. Pengine ilitokana na hali ya ukaidi.

Nikiwa nimejificha nyuma ya maboksi na meza katika hema, watu nisiowajua wakawa wa karibu nami kuliko marafiki. Magaidi lazima walijua tulipo; kulikuwa na maeneo mengi ambayo tungeweza kuyatumia kujificha.

Hata hivyo, tulitulizana wenyewe kwa wenyewe huku tukiwataka watoto wanyamaze kwa sababu sauti zingeweza kutufichua pale tulipo.

Lakini pamoja na juhudi zetu zote za kuwatuliza wanyamaze, bado baadhi ya watoto hawa hasa wale wadogo walilia.

Tuliomba. Tuliwasilisha maombi yetu kimyakimya kwa Muumba wetu, pengine tukiona hiyo ni siku yetu ya mwisho kuwa hapa duniani.

Tulikuwa tumejificha kwa dakika 20 wakati nilipomsikia mmoja wa magaidi akipokea simu kupitia simu yake ya mkononi. Hakuzungumza kwa sauti kubwa, lakini ilikuwa sauti tulivu ya Kiswahili iliyosikika vema masikioni.

Maneno halisi ilikuwa vigumu kuyakumbuka. Lakini alisema kuwa ameua watu wengi na wengine zaidi walijeruhiwa.

Dakika chache baadaye baada ya kupokea simu, magaidi walirusha risasi ovyo juu ya paa na kuondoka. Nikadhani kwamba milio hiyo ya mwisho ililenga kutuogopesha na kutuonya tusijaribu kuondoka mahali tulipo.

Tuliokolewa muda mfupi baadaye na wakati nikitembea kutoka katia jengo hilo tuliona miili ikiwa imezagaa sakafuni, nilijisikia nisiye na msaada kwamba sikuweza kufanya lolote kuzuia hali hii.

Nilikuwa huru lakini mkwe wangu alikuwa bado amenasa katika jengo. Nilipompigia simu alinihakikishia kuwa yu salama tena kwa sauti tulivu. Alinitaka nisiwe na wasiwasi, ombi ambalo halikuwezekana kwangu.

Amina aliokolewa saa 12 jioni. Saa kadhaa nikiwa nyumbani kwa mwanangu na kwa rafiki yangu kusubiri neno la matumaini kutoka kwake ilikuwa tete hakika.

Nilifarijika sana wakati alipompigia simu mwanangu akimtaka aende kumchukua kutoka Visa Oshwal.

Saa zaidi ya 24 baada ya ile iliyokuwa siku njema nikiwa na mkwe wangu iligeuka kuwa jinamizi, na bado ninatetemeka nikiikumbuka. Hata hivyo, nina furaha kuwa hai na ninashukuru Amina na mimi tulitoka Westgate bila majeraha.

*Hii ni simulizi ya mmoja wa watu waliookoka katika tukio la ugaidi la Westgate.

SOURCE: MTANZANIA