Posted Ijumaa,Septemba20 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
alisema mikutano wanayoifanya na asasi za kiraia imebainisha kwamba
uteuzi wa Tume ya Katiba ulifanyika kwa ubaguzi.
Dar es Salaam/Simiyu. Wakati
vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi vikiendelea na shinikizo la
kutaka Rais Jakaya Kikwete asitie saini Muswada wa Marekebisho ya Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe
amemwomba mkuu huyo wa nchi auridhie ili kuepusha vurugu ambazo zinaweza
kujitokeza katika kikao kijacho cha Bunge.
Ameonya kuwa muswada huo ukirudi bungeni unaweza
kusababisha vurugu kubwa zaidi ya zile za mara ya kwanza kutokana na
tofauti kati ya wabunge wa CCM na wale wa vyama vya Chadema, CUF na
NCCR-Mageuzi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Chikawe alisema
kelele zinazopigwa na wapinzani hivi sasa hazisaidii kwa kuwa muswada
huo ulipitishwa baada ya taratibu zote kukamilika.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo, atamshangaa
Rais Kikwete ikiwa atasikiliza kelele za wapinzani kwa sababu
walishirikishwa kupitia kamati na hata bungeni kabla ya kupitishwa
kwake.
“Nitamshangaa sana Rais Kikwete kama atashindwa
kusaini muswada huo kwa sababu ya kelele za wapinzani. Tuliwashirikisha
katika kila mchakato kabla na baada ya kuuwasilisha bungeni,” alisema
Chikawe.
Alisema kitendo cha wapinzani hao kujiunga pamoja
na kuanzisha kampeni za kuwahamasisha wananchi ili waukatae muswada
hakisaidii lolote, kwa sababu sheria zote zinatungwa bungeni na siyo
kwenye Viwanja vya Jangwani wala Ikulu.
Vyama vyampinga JK
Wakati Chikawe akisema hayo, viongozi wa Chadema,
CUF na NCCR-Mageuzi wameshikilia msimamo wao kwamba wataendelea kupinga
muswada huo uliopitishwa na Bunge, Septemba 6, mwaka huu.
Wakizungumza Dar es Salaam jana walipokutana na
Shura ya Maimamu ikiwa ni mwendelezo wao wa kukutana na asasi za kiraia,
viongozi wakuu wa vyama hivyo, walisema kamwe kasi yao ya kutaka
kutosainiwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
haiwezi kupunguzwa kwa namna yoyote kwa kuwa wanatetea masilahi ya
Watanzania na siyo mtu binafsi.
Kauli yao imekuja siku moja baada ya Rais Kikwete
kusema kuwa baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakisema uongo kuhusu mchakato
wa Katiba unavyokwenda.
Wanasiasa pia hao wamepinga matumizi ya kauli za
kibabe kwenye mchakato huo na kuonya kuwa nguvu ya dola haiwezi
kushindana na nguvu ya umma.
Mbali na hayo, wanasiasa hao walisisitiza kwamba
hawatapiga magoti kuomba Katiba Mpya, kwani ni ya Watanzania wote na si
mali ya wanasiasa, chama cha siasa wala wabunge.
Rais Kikwete alikaririwa na magazeti mbalimbali jana akipinga
madai ya wapinzani kuwa hakuzingatia maoni yao wakati wa uteuzi wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba.
“Nafahamu kwamba tunaambiwa tunasema uongo, lakini
ni vizuri ifahamike wazi kuwa hatuwezi kupunguzwa nguvu na kauli hizo
alizozitoa Rais Kikwete, kwani msimamo tulionao ni kuendelea kutetea
Watanzania,” alisema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Mbowe alimshauri Rais Kikwete atumie busara kwa kutosaini mkataba huo ili mchakato uende vizuri.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema
mikutano wanayoifanya na asasi za kiraia imebainisha kwamba uteuzi wa
Tume ya Katiba ulifanyika kwa ubaguzi.
“Tunafahamu kwamba Rais ana nguvu ya kuteua
wajumbe wa tume hiyo kwa mujibu wa sheria, lakini kuna taasisi zimekosa
wawakilishi kwenye tume, mfano hai ni Shirikisho la Vyama vya Watu wenye
Ulemavu (Shivyawata), walitakiwa wapeleke majina ya watu watatu, lakini
hakuna hata mtu mmoja kati yao aliyeteuliwa,” alisema Profesa Lipumba.
Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia alisema
viongozi wa Shivyawata waliwaeleza wazi kuwa hawana mwakilishi kwenye
Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Wanasiasa hao leo wanatarajia kukutana na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (Tec).
Nape alonga
Akizungumzia madai hayo ya upinzani, Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema kama wanataka waaminike,
watoe ushahidi kuthibitisha wanachokidai.
“Hawa watu ni vigeugeu. Kwanza, Rais alipoteua
wajumbe wa Tume, Chadema walijitokeza hadharani na kupongeza. Baadaye
haohao waliibuka na kuanza kuishutumu Tume wakisema kuwa imekosa weledi.
“Wakati wa mchakato wa kukusanya maoni, Chadema
haohao, ambao waliiona Tume haina weledi, wakapeleka maoni yao hukohuko.
Ukifuatilia haya mtu unashindwa kuelewa msimamo wa watu hawa ni upi
hasa,” alisema Nape mkoani Simiyu.
Imeandikwa na Patricia Kimelemeta, Aidan Mhando na Rachel Shempemb.SOURCE: MWANANCHI