Wahenga
walisema asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Kwa Bukoba nilikotokea
wanasema ‘akagunjua kalafa tikaulila nzamba' (ka-mnyama ka-kufa huwa
hakasikii baragumu). Baragumu ni njia ya mawasiliano iliyokuwa ikitumiwa
tangu enzi. Hata wauza samaki kwa Bukoba huwa wanatumia baragumu
(olukuri) wanapotembeza (wanapouza) samaki.
Wawindaji wakienda porini, hutumia baragumu kwa ajili ya kuashiria
wapi wamemwona mnyama wanayemwinda na kuwapa mbwa wanaofukuza mwelekeo
wa alipo mnyama. Sasa kwa mnyama asiyekuwa makini au ambaye siku yake ya
kufa ikiwa imefika, badala ya kusikia baragumu akajificha, yeye anatoka
hadharani kuchanja mbunga.
Sitanii,
leo nimeona bora nigusie vurugu zinazoendelea katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC). Kwa wanaofahamu historia ya Jumuiya hii, watakumbuka
Mwanasheria Charles Njonjo wa Kenya jinsi alivyoshiriki kikamilifu
kuvunja Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 1977. Jumuia hii ilivunjika
kutokana na matamshi ya Njonjo yaliyokuwa mawazo ya Wakenya.
Njonjo
alisema Kenya ndiyo Afrika Mashariki na Afrika Mashariki ndiyo Kenya.
Kenya ilionesha dharau kubwa katika Jumuiya kwa kiwango cha Tanzania na
Uganda kugeuzwa wanachama daraja la pili. Yale yale yaliyotokea mwaka
1977 yanatokea sasa mwaka 2013.
Rais
Paul Kagame wa Rwanda ametumia fursa ya Wakenya kutoipenda Tanzania kwa
dhati, wameungana na wamemwingiza mkenge Museveni, sasa Jumuiya
inaondoka.
Kagame
anakataa ushauri wa kuzungumza na waasi nchini Congo, lakini
kilichodhihirika Agosti 30, 2013 kimedhihirisha wazi pasi shaka kuwa
Kagame ndiye mmiliki wa M23 inayosumbua Congo. Amepeleka vikosi vitatu
vya jeshi DRC, vifaru vimepigwa picha vikivuka mpaka kutoka Rwanda
kwenda DRC. Hatua hii imethibitisha wazi kuwa madini na mbao za Congo
ndiyo chimbuko la utajiri wa Rwanda.
Tumeshuhudia
sasa wanazindua miundombinu Mombasa bila kumwalika Rais Jakaya Kikwete
wakishirikiana na Museveni, tuliyemsaidia kuingia madarakani, ila
naamini huyu mzee bado anawapima akili zao.
Uhuru
Kenyatta sijajua labda anakerwa na kauli ya John Magufuli aliyoitoa
kwenye Mkutano wa Raila Odinga kuwa CCM inamuungano mkono Odinga.
Anadhani Tanzania ni CCM, hivyo msimamo wa CCM ni msimamo wa Tanzania.
Kabla
sijaendelea, nimeona ni bora hapa chini nibandike neno kwa neno habari
ya Ndugu Manyerere Jackton, aliyoiandika katika Gazeti la Tanzania
Daima, Oktoba 6, 2010 alipokuwa ziarani Ngara, mkoani wa Kagera, kama
ifuatavyo:-
Ngara wapinga Rwanda, Burundi kukaribishwa EAC, Chanzo kikuu ni vita, ukabila, Wasema watavuruga amani nchini
Na Manyerere Jackton, Ngara
WANANCHI
katika Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera, wanapinga nchi za Rwanda na
Burundi kupewa uanachama katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Msimamo
wa wananchi hao umefahamika kwenye mikutano iliyohutubiwa na Naibu
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Diodorus Kamala, juzi.
Naibu
waziri huyo yuko katika ziara ya kuitambulisha wizara, kueleza fursa
zinazotokana na Jumuiya hiyo; na kukusanya maoni mbalimbali ya wananchi,
yakiwamo ya ama, Burundi na Rwanda ziruhusiwe kujiunga au zisiruhusiwe.
Akiwa
katika Kijiji cha Kabanga, wilayani Ngara, ambako ni mpakani mwa
Tanzania na Burundi, wananchi walitoa maoni yao kwa uwazi na kupinga kwa
nguvu zote Burundi na Rwanda kupewa uanachama kwenye Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Aliyeanza
kutoa maoni yake ni Suleiman Minani, na akasema: “Kujiunga kunahitaji
muda, hawa wamekuwa katika mapigano kwa muda mrefu, wametuletea uhalifu,
hasa ujambazi. Hapa Ngara ujambazi umeletwa na wakimbizi hawa.
“Sisi Watanzania Kiswahili ndicho kitambulisho, Warundi na Wanyarwanda sasa wakizungumza Kiswahili, wanaonekana ni Watanzania.
“Kwa nini Serikali inachelewa kutoa vitambulisho kwa raia wake?” alihoji.
Mwananchi
huyo alitoa mfano kwa kusema wakati fulani alisafiri na Wanyarwanda
kwenda Mwanza. Walifika kwenye kizuizi, na akastaajabu kuona wakitoa
kadi za uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na kuruhusiwa kuendelea
na safari.
“Mimi
nilipita kwa kitambulisho cha gazeti, hatuna vitambulisho na viwango
vya kuoleana ni vikubwa, kule (ng’ambo upande wa Burundi) tuna wajomba,
mimi nashauri wasubiri kujiunga kwenye Jumuiya, wakiruhusiwa sasa,
usalama wetu utayumba,” alisema.
Mwananchi
Seleman Senduka alisema: “Kabla ya kuwakaribisha Rwanda na Burundi,
kwanza tujue sisi (Kenya, Tanzania na Uganda), tumefaidika vipi na
Jumuiya yetu.”
Naye
Jason Bahina alisema: “Sisi Watanzania hatuna matatizo ya ukabila na
vita; wenzetu wanamalizana kwa kuuana. Wanahukumiana kwa kuangaliana
pua.
“Kabla
ya kuwakaribisha, CCM ifanye kwanza kazi ya kisiasa, ijiridhishe kama
kweli kujiunga kwao hakutaleta mgogoro. Kilichosambaratisha Jumuiya ya
kwanza ni tofauti za kisiasa, kwa hiyo kabla ya kuwakaribisha Rwanda na
Burundi, lazima mataifa haya yaeleweke siasa zao.”
Mwananchi
mwingine, Joseph Balindie, yeye alisema wananchi wana wasiwasi mkubwa
kuona Rwanda na Burundi zinataka kujiunga kwenye Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
“Tuna wasiwasi, tabia za wenzetu - kuwashirikisha ni ngumu, wale wanauana, kuwashirikisha si rahisi,” alisema.
Naye
Gideon Ruvulahende (66), alisema: “Kuungana ni jambo zuri, sasa kama
Rwanda na Burundi nao wanataka kuungana na sisi, kwanza wapewe masharti
ya kuumaliza ukabila wao.”
Japhet
Israel (62) alisema kwa umri wake huo, hajawahi kusikia Rwanda na
Burundi kuna amani. Alikiri kuwa wananchi katika nchi hizo ni ndugu
zetu, na kwamba hata baadhi yao wanafanana na Watanzania, lakini kwa
suala la kuwakaribisha kwenye Jumuiya kwa sasa, haliafiki.
“Tukiungana
tutaharibu usalama wetu, kwanza wajirekebishe, wajue sote tu Waafrika,
wajue Watutsi na Wahutu wote ni Waafrika, wajue weupe (Watutsi) na weusi
(Wahutu) ni Waafrika, wakijua hivyo, sasa ndipo wakaribishwe kujiunga,”
alisema Israel. Ofisa Uhamiaji Mkuu wa Kituo cha Kabanga, Harride
Mwaipyana, alitumia fursa ya mkutano huo wa hadhara kutoa maoni yake.
“Nipo
hapa kuanzia mwaka 1999, nimesoma tabia za pande zote. Tusikurupukie
kitu bila kukijua. Sisi Tanzania, Kenya na Uganda tunajuana tabia
zetu. “Tabia za hawa wenzetu (Rwanda na Burundi) ni mbaya - hawana
amani, wanabaguana, kuna vikao vya usiku vya kujadiliana. Wanakutana kwa
mambo ya siri wakitumia vijisherehe, wanaalikana.
“Ukiwaingiza
hawa, nchi itaharibika, wanapenda kutawala, wanajiona ni bora kuliko
mtu yeyote duniani, tusiwakaribishe kabisa. Tuchukue muda mrefu
sana. “Mheshimiwa Naibu Waziri naomba ulichukue hili kwa umuhimu wa
kipekee. Ujambazi wameleta wao…,” alisema Mwaipyana, akionekana dhahiri
kuchukizwa na Rwanda na Burundi kujadiliwa kujiunga kwenye Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
Maoni
kama hayo yametolewa na wananchi wengi katika maeneo mengi ambayo Dk.
Kamala ameyazuru. Kutoka Gazeti la Tanzania Daima, Ocktoba 5,
2006. Kinachotokea leo kinathibitisha bila chembe ya shaka wasiwasi
waliokuwa nao wakazi wa Ngara. Inawezekana Kenya, Uganda, Burundi na
Rwanda, na sasa nasikia zimeialika Sudan Kusini kuna jambo wasilotaka
kulisema. Na hili mimi nalisema. Hawa wanadhani wakitupa msukosuko kama
nchi, tutakubaliana na madai yao ya muda mrefu.
Nchi
hizi mara zote zimekuwa zikitaka suala la ardhi liwe la Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Kimsingi hili haliwezekani. Lugha hii inamaanisha kuwa
wanataka ardhi ya Tanzania ndiyo ichukuliwe. Ukichukua ardhi ya nchi za
Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda ukubwa wa eneo la Tanzania bado
unazidi nchi hizi kwa wastani wa kilomita za mraba 100,000.
Ukiacha
ukubwa wa eneo la ardhi ya Tanzania, pia mfumo wa ardhi nchi za Kenya
na Uganda, sina hakika sana kisheria Rwanda na Burundi, ila nikisoma
kwenye mitandao sioni tofauti kubwa, kwa nchi hizi ni majanga. Nasema ni
majanga kwa sababu katika nchi hizi ardhi inamilikiwa na watu binafsi.
Siwezi kuthibitisha hili, ila inaelezwa kuwa familia ya Kenyatta
inamiliki asilimia 25 ya ardhi yote ya nchi hiyo.
Hapa
unaweza kuona tatizo lilivyo. Uganda Kabaka anamiliki asilimia kubwa ya
ardhi katika eneo linaloitwa Buganda, na hii ina maana kuwa hakuna mtu
yeyote anayeweza kugusa ardhi hii wanayoimiliki. Rwanda na Burundi kuna
msongamano mkubwa wa watu na hivyo kwao kupata ardhi ya ziada ni
mahitaji na si matakwa.
Kinachotokea
sasa ni kuwa wakubwa hawa wamekuwa sawa na hadithi ya ‘Sungura mjanja’.
Wameruka hadi wamechoka mikia, ila sasa wanasema ‘hawazitaki mbichi
hizi’. Mwelekeo wa kutususa ninaouona sasa unaelekea katika kuunda
Jumuiya ya Afrika Mashariki ‘Academia’. Hapa kuna hatari, manyang’au
wawili wakiunganisha nguvu, mwisho wa siku wakikuta hakuna wa kupambana
naye wanageukana.
Kuna
kila dalili kuwa busara isipotawala, Kagame akaona bora aendeleze vita
DRC kujipatia utajiri wa Wacongo, hakika sitashangaa vita hii ikisambaa
ikaingia Rwanda, hatimaye ikaivunja Jumuiya ya Afrika Mashariki. Je,
wewe msomaji unadhani EAC iko kwenye mkondo salama? Nipe jibu.
SOURCE: JAMHURI MEDIA
|