Saturday 21 September 2013

Nina wake wengi feki

Majuto akiwa na mkewe Aisha 
Na Kalunde Jamal, Mwananchi

Posted  Septemba21  2013  saa 13:15 PM
Kwa ufupi
Wiki iliyopita Amri Athumani ‘King Majuto’, alizungumzia umaarufu wake Kenya na vijana wa sarakasi. Leo anazungumzia familia yake. Endelea...


Majuto anasema kuwa ana watoto tisa ingawa hakuwa tayari kuwazungumzia mama wa watoto hao zaidi ya kumwongelea mkewe wa sasa, Aisha Mbwana kwa kuwa wake zake aliozaa nao baadhi ya watoto kwa bahati mbaya walishafariki dunia.
Alisema kuwa yanapokuja masuala ya familia huwa anapenda azungumze mkewe na kwa ridhaa yake. Kwa mujibu wa Majuto anapenda aitwe mke halali kwa kuwa wake feki anao wengi kupitia michezo ya kuigiza na wengine wenye fikira potofu hutumia picha hizo kutengeneza habari za uongo.

Aisha anaizungumziaje familia yake
Kama kawaida ya wanawake wa Tanga ana lafudhi ya huko ambayo huvutia kuzungumza nao, anaanza kwa kunieleza kuwa alianza kuitwa mke halali wa nguli huyo wa sanaa za maigizo mwaka 1997, walipofunga ndoa .
Anasema kuwa alikutana na nguli huyo maeneo ya Buguruni, Dar es Salaam, ambako alikuwa akiishi na dada yake aliyekuwa kaolewa na rafiki yake mzee Majuto, ‘Mwanachia’ (kwa sasa ni marehemu), ambaye walikuwa wakiigiza pamoja.
Anasema hakuwa na hili wala lile hadi alipoamua kuondoka na kurudi kwao maeneo ya Vingunguti, ambako ndiko walikokuwa wanaishi wazazi wake na kupewa taarifa kuwa posa imepelekwa kwa ajili yake.
“Nilipoambiwa kuhusu hiyo posa sikufikiria kama atakuwa ni mzee Majuto kwa kuwa alikuwa ni kama shemeji yangu kutokana na kuwa karibu na shemeji yangu,” anasema Aisha ambaye ni mama wa watoto watatu.
Anaendelea kueleza kuwa siku ambayo wanafamilia walikutana na kumuuliza kama anamfahamu mchumba na kutajiwa jina kuwa ni Amri Athumani, aliuliza mara mbili kwa kuwa alikuwa hamfahamu huyo mtu hadi alipoambiwa kuwa ni King Majuto.
“Kwa mila za Wabondei mchumba wa kwanza anakubaliana na wazazi, halafu binti anapewa taarifa na kwa kuwa wazazi ni wakubwa inabidi binti akubali, na ndivyo ilivyokuwa kwangu nikakubali na kuolewa na Majuto,” anasema mama huyo.

Anaingia kwenye uigizaji kufuata nyayo za mumewe
Aisha anafafanuwa kuwa kabla ya kuolewa na Majuto hakuwa mwigizaji lakini baada ya kuolewa, mumewe huyo alimwingiza kwenye uigizaji na filamu ya kwanza kuigiza na mumewe huyo ni ‘Fukara hatabiriki’.
Mkewe huyo anasema kipindi hicho Majuto alikuwa anafanya kazi bila kuwa na kikundi zaidi ya wanafamilia, hivyo na yeye alikuwa mmoja wao akicheza kama mama na Majuto kama baba.

Katika kuashiria kuwa ni yeye alikuwa chachu ya mkewe kuwa mwigizaji Majuto anaunga mkono kwa kusema kuwa; “kipindi filamu hiyo inatoka hakukuwa na filamu kabisa na kama nilivyosema mwanzo kwa hapa nyumbani inaweza kuwa ni moja ya zile za kwanza kabisa, hivyo niligundua kipaji cha mke wangu kwa kumtazama tu, kwani hakuna ambako aliwahi kujifunza kama sasa ambapo unaweza kutazama filamu mbili tatu ukajifunza kitu, kwani wakati huo hata televisheni hatukuwa nayo, kwa kweli alijitahidi,” anasema kwa msisitizo Majuto.
“Nilimjaribu nyumbani kama anaweza kuigiza filamu fupi fupi akaweza, nikaona kwa nini nisifanye naye kazi kwa faida ya familia na kupunguza kufanya kazi na watu wengi ambao watahitaji niwalipe na wakati huo hakukuwa na fedha kama sasa,” anasema Majuto na kuongeza kuwa:
“Alifanya vizuri hadi sikuamini kuwa kulikuwa na kipaji nakipita hadi moyo wangu ulipodunda ndiyo nakigundua,” anasema nguli huyo huku anacheka na kuchekesha kidogo kama kawaida yake.
Aisha anaongeza kuwa hakuishia hapo kwani alicheza michezo zaidi ya 10, kabla ya kupumzika baada ya kupata ujauzito wa mtoto wake wa kwanza mwaka 2000, ambapo baada ya hapo hakuwahi kufanya kazi tena na mumewe zaidi ya ile ya ‘mazingira ya misitu’ na ‘mazingira ya bahari’, ambayo zilikuwa ni filamu maalumu za kueleimisha kuhusu kutunza misitu na bahari.

Anazungumziaje mafanikio yao
Anaendelea kueleza kuwa ameishi na mumewe huyo kwa kazi hiyo ya uigizaji na hapo nyuma haamini jinsi ambavyo maisha yalikuwa magumu, akilinganisha na jinsi ambavyo wamepiga hatua hivi sasa.
Mkewe Majuto anasema kuwa anajivunia hatua waliyopiga katika maisha hasa kutokana na kusota sana siku za nyuma, kwani hata wakati wanajenga na mumewe nyumba hiyo hali haikuwa nzuri.
“Naamini maneno ya wahenga kuwa kujenga ni akili na siyo mali, kwani nikikumbuka kipindi tunajenga nyumba hii hali ilivyokuwa na sasa hali ilivyo naona tulitumia akili zaidi ya fedha, kwani fedha alizokuwa anapata mume wangu zilikuwa ndogo ukilinganisha na sasa,” anasema mama huyo.
Majuto anakubaliana na mkewe kwa kusema kuwa uigizaji ulikuwa ni mgumu sana kipindi hicho na fedha ilikuwa ndogo, tofauti na sasa kila kitu kipo lakini na fedha ipo, kibaya zaidi waigizaji wenye vipaji kama wao hakuna.
Aisha anasema kuwa alipata mtoto wa kwanza mwaka 2001, aitwaye Bilali, ambaye anasoma darasa la sita, wa pili Halima ambaye alimpata mwaka 2007 na wa tatu ni Rutifia aliyempata mwaka huu.
Ninataka kujua kama mzee Majuto bado anaendelea kupata watoto zaidi ya hao kwa kuwa ukijumlisha na wengine atakuwa na watoto tisa, “Wewe Mnyamwezi usiniletee wazimu nisimpe mimba kwa nini wakati mke wangu bado binti na anahitaji watoto, nawahitaji na awalete tu hadi waishe,” anajinasibu Majuto huku anacheka kwa nguvu.
Hata hivyo, Aisha anamwelezea mumewe huyo kuwa ni mpole na mkarimu anayependa watu.


Anaendelea kueleza kuwa ukimtazama Majuto na mambo yake huwezi amini kuwa ni baba bora na mkarimu kwa familia, na hana utani katika mambo ya msingi.
Mkewe huyo anaeleza mafanikio yao ambayo anaamini pamoja na mumewe kuwa mstari wa mbele kutafuta fedha, lakini yeye ana mchango mkubwa.

Mafanikio
Anasema amepata mafanikio kiasi kutokana na kazi ya mumewe na anachofanya ni kuhakikisha fedha yao haifanyi mambo yasiyo ya lazima katika familia.
Mkewe huyo anafafanua kuwa kwakuwa hakuna anayekunywa pombe wala kuvuta sigara, hakuna sababu ya kukosa maisha mazuri na fedha za ziada.
Anayataja mafanikio kuwa ni kumuhimiza mumewe kununua shamba kwa ajili ya kujiandaa na maisha ya baadaye; “alinisikia na tukanunua shamba la ekari 20 huko Muheza ambako tumeotesha mihogo, mahindi na michungwa, ikiwemo ufugaji wa kuku 600, nikiwa ndiyo msimamizi mkuu, na ninataka aniongezee cherehani katika kiwanda ambacho kwa sasa zipo saba tu,” anasema Aisha.
Majuto anamalizia kwa kuwataja baadhi ya watoto wake akianza na mwanawe wa kwanza aitwaye Athumani ambaye ana miaka 40, Haruna, Omari, Yusuphu, Shafii, Hamza, na watoto wake watatu ambao aliwapata akiwa na mkewe anayeishi naye sasa Aisha Mbwana, ni Bilali, Halima na Rutifia.
Kwa kumalizia Majuto alitoa wito kwa vijana hasa wasanii kwenda na kasi ya maisha kwa maana ya kuwekeza kwa ajili ya maisha ya baadaye, kwa kuwa tasnia ya sanaa imekuwa na watu wengi, huku wapya na wenye uwezo wakizaliwa kila siku.

SOURCE: MWANANCHI