Friday 27 September 2013

Oestradiol: Homoni zinazochochea ngono kwa wanawake

 
Na Florence Majani, Mwananchi

Posted  Ijumaa,Septemba27  2013  saa 14:37 PM
Kwa ufupi
  • Wanawake wenye kiwango kikubwa cha vichocheo (homoni) aina ya oestradiol, wana mwamko mkubwa wa kushiriki tendo la ndoa kuliko wanawake wenzao wenye kiwango kidogo cha vichocheo hivyo.

Ni ajabu, wala si jambo la kawaida kwa wanawake walio wengi kujikuta katika matamanio, kiasi cha kujikuta wakilazimika kushiriki tendo la ndoa.
Hata hivyo, homoni kadhaa zilizoko katika miili ya wengine zinawachochea kujitumbukiza kwenye tendo hilo.
Utafiti wa baadhi ya wanasayansi umeonyesha kuwa baadhi yao wana kiwango kikubwa cha vichocheo mwili kinachoweza kushawishika kuwa na mpenzi wa nje au kumchoka haraka mwenza wake baada ya kuishi naye kwa kipindi fulani.
Wanasayansi hao wamefanya uchunguzi na kugundua kuwa, wanawake wenye kiwango kikubwa cha vichocheo (homoni) aina ya oestradiol, wana mwamko mkubwa wa kushiriki tendo la ndoa kuliko wanawake wenzao wenye kiwango kidogo cha vichocheo hivyo.
Vichocheo hivi aina ya oestradiol (oestrogen) ni vile  vinavyotumika katika kuzalisha mayai ya uzazi wa mwanamke. Pia, vichocheo hivyo ni vile ambavyo humpa mwanamke mwamko wa tendo la ndoa.
Wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Saikolojia nchini Uingereza walifanya utafiti kuhusu uhusiano uliopo kati ya vichocheo na tabia za watu na kubaini kuwa kiwango cha vichocheo  huweza kuelezea tabia ya mwanamke ikiwamo kumsababisha kuwa na tamaa za mwili zaidi tofauti na wanawake wengine.
Wanasayansi hao, Dk Kristina Durante na Norm Li walitoa ushahidi wa utafiti wao kuwa mfumo wa kisaikolojia unachangia kwa kiasi kikubwa katika mwamko wa tendo la ndoa na tabia kwa wanawake.
Wanawake  52 wenye umri wa kati ya miaka 17 na 30, wote wanafunzi wa vyuo vikuu walishiriki katika utafiti huo  na kuambiwa wasitumie njia yeyote ya uzazi wa mpango kwa sababu njia hizo huongeza vichocheo mwilini.
Kwa upande wao, watafiti walipima kiwango cha homoni hizo kwa wanawake wote na walipewa maswali ya kujibu yaliyohusu mienendo yao ya kimapenzi, kutosheka na wenzao pamoja na uwezo wa kuvumilia kutofanya tendo la ndoa kwa kipindi fulani.
Pia, washiriki hao walitakiwa kujibu maswali maalumu ambayo yanapima uwezekano wa washiriki hao kuwasaliti wenzao wao.
Mwishowe, watafiti hao walibaini kuwa, wanawake wenye kiwango kikubwa cha vichocheo vya oestradiol wanapenda utani, wanapenda kupigana busu na ni rahisi kupata mwenza mpya wa kudumu wakati wowote.
“Matokeo yetu yalibaini kuwa, wanawake wenye kiwango kikubwa cha rutuba za uzazi hawatosheki na mwenza mmoja hasa waliyeishi naye kwa muda mrefu. Wana uwezo wa kutafuta mwenza mwingine anayewatosheleza,” alieleza Dk Durante.


Hata hivyo, daktari huyo alisema kuwa, wanawake wa aina hiyo hawapendi kushiriki tendo la ndoa ovyo au kuwa na wapenzi wa muda mfupi, bali wanaweza kuwa na wenza wawili wa kudumu ili mradi wamtosheleze.
Almasi Nyangasa, Daktari Bingwa wa magonjwa na upasuaji wa moyo anasema, vichocheo vya mwanamke vinabadilika kulingana na mzunguko wake wa mwezi.
 “Wanawake wana vichocheo  vya aina nyingi. Viwango vya vichocheo hivyo hubadilika kulingana na mzunguko wake” anasema
 Anaizungumzia homoni ya oestradiol na kusema kuwa homoni hiyo inatakiwa kuwa katika kiwango cha kawaida, ikizidi au ikipungua basi mwanamke anaweza kuwa na tabia zisizo za kawaida.
Kwa mfano, mwanamke anaweza kuwa na mwamko wa kufanya mapenzi au asiwe nao kabisa. Pia,  baadhi wanapata mabadiliko ya miili yao kama chunusi au kuwa na hasira.
 “ Hata hivyo, si lazima mwanamke mwenye kiwango kikubwa cha homoni hii akawa na uwezo mkubwa wa kushika mimba. Wingi wa homoni hizo zinaweza kumfanya mimba ziharibike au asishike kabisa” anasema
Dk   Nyangasa  anasema tabia za mwanamke hubadilika pindi homoni zake zinapopita katika mzunguko ambao husababisha yai kupevushwa na  ama ashike mimba au apate  hedhi.
 “Inawezekana mwanamke akawa siyo wa kawaida, hivyo akawa na homoni hii kwa kiasi kikubwa hivyo akawa na mwamko mkubwa wa tendo la ndoa” anasema
Anaongeza kuwa wingi au uchache wa homoni huweza kuharibu mzunguko wa hedhi kwa mwanamke ambapo anaweza kupata hedhi siku nyingi zaidi au siku chache.
Naye Dk Meshack  Shimwela, Bingwa wa Magonjwa ya Ndani ya Mwili, anasema homoni humbadilisha mwanamke kwa hali ya ajabu.
 Anatoa mfano kuwa wako wanawake wenye vinyweleo vingi mikononi na miguuni, wenye sauti za kiume na wenye miili imara mithili wa wanaume.
Kuhusu mwamko mkubwa wa kujamiiana,  Dk Shimwela anasema wingi wa homoni ukizidi unaweza kumfanya mwanamke akawa na mwamko mkubwa lakini wapo ambao si wa kawaida.

“Kuna watu ambao si wa kawaida, lakini hili linahusiana na saikolojia ya mtu pamoja na tabia yake,.” Anasema.
 Hata hivyo anasema, mwamko wa kujamiiana humkuta kila mwanamke kadri homoni zake zinavyobadilika lakini baadhi  yao homoni zao zinakuwa nyingi na wanapata mwamko ambao si wa kawaida.
 Dk Antoinnete Molekhele wa Kitengo cha Afya ya Uzazi, Hospitali ya Rosebank, Afrika Kusini anachambua namna vichocheo vinavyofanya kazi na kusema kuwa, mayai ndiyo yanayozalisha homoni.
“Mayai yetu yanatengeneza homoni za oestrogen na progesterone kwa kiasi kikubwa  na kiasi kidogo cha homoni za kiume aina ya testosterone na andorstenedione,” anasema
Pia, anasema wanawake na wanaume wana homoni mbili za muhimu ambazo zinatengenezwa na tezi ya ‘pituitary’  ambazo ni FSH na LH.
 Anasema kichochezi cha FSH (Follicle Stimulating Hormones) kinadhibiti utengenezwaji wa mayai na kichochezi cha LH (au luteinizing horomone) inasimamia utengenezwa wa vichocheo vya mwamko wa kujamiiana.
“Kichochezi cha LH, ndicho kinachosimamia kwa kiasi kikubwa mwamko wa kujamiiana na inapozidi  kiwango chake cha kawaida  basi inaweza kumuathiri mwanamke,” anasema Dk Molekhele
 Kwa wanawake,  kiwango cha homoni  za oestrogen (oestradiol) hupanda taratibu katikati ya mwezi, kisha huanza kushuka kwa kasi wakati yai linachavushwa na siku ya 14 hushuka kabisa na mwanamke huanza kupata hedhi.
“Wanawake hutofautiana viwango vya homoni hii na kuwafanya kuwa tofauti linapokuja suala la mwamko.” Anasema
 Anaongeza kuwa, homoni humuathiri zaidi mwanamke ambaye anaanza kufikia kikomo cha hedhi, kwani wakati mwingine huweza kupata dalili za ujauzito wakati hana au kupata hasira na kukosa kujiamini.

SOURCE: MWANANCHI