Tuesday, 17 September 2013

Padri: Wahalifu wa tindikali wanalindwa

17th September 2013
  Ni utekelezaji wa ajenda ya siri Z'bar
  Ambebesha zigo Kamishna wa Polisi
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema
Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Cheju, Zanzibar, Joseph Mwang’amba, aliyemwagiwa tindikali wiki iliyopita na kuumia vibaya usoni na kifuani, amesema uhalifu huo unakingizwa kifua na watu wenye nguvu katika jamii.

Akizungumza jana akiwa wodini katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili JIJINI Dar es Salaam, pia alisema inawezekana kuna ajenda ya siri iliyojificha kufuatia mfululizo wa matukio ya watu kumwagiwa tindikali visiwani humo na wengine kuuawa huku vyombo vya usalama vikishindwa kuwasaka na kuwakamata wahusika.

Bila kuwataja wahusika, alionyesha wasi wasi wake kwamba kuna kundi lenye nguvu katika jamii linalowalinda na ndiyo maana hawakamatwi.

Aidha, Padri Mwang’amba alisema kuwa tukio hilo halitamrudisha nyuma katika kufanya kazi yake ya kitume na kwamba atakapopata nafuu atarejea Zanzibar kuendelea na kazi yake.

Ingawa hakuwa tayari kutaja wenye nguvu hao, lakini ndani ya jamii kuna makundi mawili yenye nguvu, ama ni za kisiasa au za fedha. Kwa maana hiyo walengwa wa kauli ya Padri Mwang’amba ni kati ya makundu hayo.

Padri Mwang’amba ambaye alimwagiwa tindikali Ijumaa iliyopita na kulazwa Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar kabla ya kuhamishiwa Muhimbili, alisema ili kurejesha imani kwa jamii, Serikali inatakiwa kuchukua hatua ya kukisaka na kukikamata kikundi cha watu wanaoaminika ndio wanajihusisha na vitendo hivyo ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

Padri Mwang’amba alisema katika kuonyesha wasiwasi juu ya matukio hayo, hata Kamishna wa Polisi Zanzibar, Musa Ali Mussa, hajachukua jitihada za kwenda kumjulia hali hospitalini kama walivyofanya viongozi wengine wa Serikali na wa Jeshi la Polisi.

“Nashukuru Dk. Shein (Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar); Mbunge wa Jimbo la Kusini Magharibi; Ofisa Usalama wa Taifa wa Mkoa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, lakini nashangaa Kamishna wa Polisi Zanzibar hajafika kuniona,” alisema Padri Mwang’amba.

Alisema tukio la kummwagiwa tindikali siyo la kwanza kutokea kisiwani Zanzibar na kwamba yametokea mengi, lakini katika hali ya kushangaza mpaka sasa hakuna hata mtu mmoja aliyekamatwa  kwa kuhusishwa na matukio hayo.

 “Yapo matukio ya kupigwa risasi mapadri na wengine kumwagiwa tindikali. Masheikh na wasichana wawili wa Uingereza ambao nao walimwagiwa tindikali, lakini mpaka sasa ni mtuhumiwa mmoja tu anayedaiwa kumpiga risasi Padri Mkenda ndiye aliyekamatwa na kesi inaendeshwa kwa kificho,” alisema Padri Mwang’amba.

Aliongeza kuwa ni jambo la kushangaza kuona kikundi kidogo cha watu kikiachwa kufanya unyama huo na kujigamba kuwa kitahakikisha kinamaliza Ukristo Zanzibar hasa viongozi wa Kanisa Katoliki huku serikali ikikaa kimya bila kuchukua hatua.

Alisema matukio haya ni changamaoto kwa makanisa yote kuungana kuangalia usalama kama yalivyoungana wakati makanisa kadhaa yalipochomwa moto.

“Sijui tufanyaje ili kukomesha tabia hii ambayo sasa imeanza kuzoeleka, maana kama siyo risasi basi ni tindikiali na mbaya zaidi hatujui nani atafuata baada ya mimi,” alisema Padri Mwang’amba.

Akizungumzia hali yake alisema kwa sasa anaendelea vizuri, isipokuwa bado mikono imevimba na bado kuna uvimbe usoni, lakini anategemea hali yake itaendelea kutengamaa zaidi kutokana na matibabu mazuri anayopata.

Hata hivyo, Kamishana Mussa, alipoulizwa kuhusu madai ya kuwa hajaenda kumjulia hali padri huyo, alisema: “Haiwezekaniki watu wote kwenda hospitali. Sote kama Wazanzibari tukienda kumwangalia hospitali itakuwaje.”

Alisema siyo sehemu ya kazi yake bali anashughulikia kesi yake na kuhoji kuwa kama atakwenda huko atapata wapi muda wa kufuatilia kesi hiyo.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Zanzibar limeanza operesheni ya kuwasaka waingizaji, wasambazaji na wauzaji wa tindikali kwa lengo la kupunguza matumizi yake kiholela na limefanikiwa kuwakamata watu 15.

Kamishna Mussa alisema operesheni hiyo ilianza mara baada ya kuona matumizi ya tindikali kukithiri kinyume cha sheria.

Alisema miongoni mwa watu waliokamatwa ni vijana wanaojihusisha na imani kali za kidini na siasa zenye mwelekeo wa kikundi cha Al Shaabab cha Somalia.
Alisema baadhi ya vijana hao walikamatwa wakitaka kwenda kujiunga na Al Shaabab na walikiri kuwa wanakwenda kupigana vita vya Jihad.


Kamishna Mussa alipoulizwa baada ya mkutano na waandishi wa habari kuhusiana na mahali ambako vijana hao walikuwa wanaelekea kupigana vita ya Jihad, hakueleza zaidi ya kusema wanawahoji zaidi kwa kuwa wana wasiwasi kuwa wanajihusisha na  kikundi cha Al-Shaabab.

Kuhusu sheria ya udhibiti wa tindikali Zanzibar, Kamishna Mussa alisema sheria inayoelezea uuzwaji na matumizi ya tindikali ni kubwa, hivyo asingeweza kuielezea na kuomba apewe muda wa kuisoma na kuitolea ufafanuzi siku nyingine.

POLISI WAKOSOLEWA


Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema Jeshi la Polisi limekuwa la kisiasa zaidi na hivyo kukosa weledi wa kufanya kazi ya uchunguzi kuwakamata watuhumiwa wanaojihusisha na vitendo vya kinyama vya kumwagia watu tindikali.

Akihojiwa jana katika kipindi cha Kumepambazuka kinachorushwa na Radio One Stereo kuhusu mfululizo wa matukio ya tindikali, Profesa Lipumba alisema Jeshi la Polisi linatakiwa kuwa na weledi na intelejensia inayoweza kufanya uchunguzi wa kina kufuatilia nyendo na kuwakamata watuhumiwa.

“Kuna tatizo la kukosa weledi ndani ya Jeshi la Polisi Zanzibar, polisi wangekuwa na weledi wanaofanya matukio haya wangekamatwa kirahisi,” alisema.

Alisema tukio la Padri wa Kanisa Katoliki kumwagiwa tindikali, siyo la kwanza bali kumekuwa na matukio ya aina hiyo toka 1995 na Zanzibar yamekuwa yakijitokeza mara kadhaa, lakini cha kushangaza hakuna wanaokamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Aliongeza kuwa kutokana na mfululizo wa matukio haya, kuna haja kwa serikali kuwatambua watu wanaojihusisha na biashara ya kemikali na wanunuaji wanaonunua kwa wauzaji ifahamike wanakwenda kutumia kwa kazi gani.

MREMA: NI KAMPENI CHAFU
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, alisema matukio ya watu kumwagiwa tindikali ni kampeni chafu inayofanywa na baadhi ya watu wachache.

“Watu wachache wasiifanye nchi iwe mateka, serikali ihakikishe hatua zinachukuliwa kwa gharama zozote kuwadhibiti,” alisema.

Kamishna Mussa, alisema jeshi hilo kulaumiwa ni kutolitendea haki kwani limekuwa likijitahidi kufanya kazi kwa nguvu kupunguza uhalifu nchini ingawa yapo matukio mengine ambayo limeshindwa kuwajua wahusika.

Imeandikwa na Samson Fridolin, Thobias Mwanakatwe, Gwamaka Alipipi, Dar na Rahma Suleiman, Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE