Thursday 26 September 2013

Sitta ‘avishukia’ vyombo vya ulinzi

 
Na Raymond Kaminyoge

Posted  Alhamisi,Septemba26  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
“ Ukiona mwenzako ananyolewa na wewe tia maji, vyombo vya ulinzi na usalama viimarishe ulinzi hasa kwenye mikusanyiko ya watu,”

Dar es Salaam. Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuacha kufanya kazi kwa mazoea, bali viimarishe ulinzi ili kukabiliana kuweza matukio ya kigaidi.
Sitta alisema hayo jana baada ya kufungua mkutano wa Chama cha Waajiri Tanzania (Ate) na sekta binafsi.
Alisema tukio la ugaidi lililotokea Nairobi nchini Kenya ambalo limesababisha vifo vya watu 62 linaweza kutokea mahali popote ikiwemo Tanzania.
“ Ukiona mwenzako ananyolewa na wewe tia maji, vyombo vya ulinzi na usalama viimarishe ulinzi hasa kwenye mikusanyiko ya watu,” alisema.
Alisema vyombo vya ulinzi vinatakiwa kuwa macho muda wote ili kukabiliana na hatari yoyote inayoweza kutokea.
“Tunawapa pole wenzetu wa Kenya kwa maafa hayo, nasi tuchukue tahadhari kwa sababu magaidi hawasemi ni lini watakuja kuvamia,” alisema.
Akizungumzia tukio hilo, Sitta alisema ni la kutisha ambalo linalaaniwa na kila mpenda amani na kwamba magaidi hao wanatakiwa kusakwa popote walipo,ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

SOURCE: MWANANCHI