15th September 2013
Hatimaye
serikali imeonyesha wasiwasi juu ya mwenendo wa nchi tatu zilizo
miongoni mwa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Imepinga dalili zinazoonekana kwa nchi za
Kenya, Uganda na Rwanda, kutumia jina la EAC kuomba fedha au kugharamia
miradi inayopaswa kuwa ya Jumuiya.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa
Afrika Mashariki, Dk. Abdallah Abdallah, wakati akizungumza na NIPASHE
Jumapili jijini Dar es Salaam juzi.
Alisema malalamiko hayo, yalishawasilishwa
pia katika kikao cha baraza la mawaziri wa EAC, kilichofanyika hivi
karibuni jijini Arusha.
Dk. Abdallah, alisema serikali imemtaka
Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard Sezibera, kutoa maelezo juu ya gharama
ya miradi kadhaa inayoaminika kuwa sehemu ya jumuiya hiyo.
Nchi hizo zimekuwa katika mchakato wa kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo na kuonekana kuitenga Tanzania.
Marais wa nchi hizo, Uhuru Kenyata
(Kenya), Yoweri Museveni (Uganda) na Paul Kagame (Rwanda), walikutana
mara mbili bila kumualika Rais Jakaya Kikwete.
Kwenye vikao viwili vilivyofanyika Kampala
na Nairobi, viongozi hao walikubaliana kutekeleza kwa haraka miradi ya
ujenzi wa reli itakayounganisha nchi hizo na bomba la mafuta
litakalojengwa kuanzia Sudan Kusini hadi Mombasa na jingine kutoka
Kampala hadi Kigali.
Katika hatua nyingine, nchi hizo
zimetangaza kuanzia Januari, Mosi mwakani, raia wao watembeleana bila
kuwa na hati ya kusafiria, pia kuwa na viza moja kwa watalii.
Katika kuonyesha umoja huo unakuwa katika
sura ya jumuiya, mkutano wa Kenya ulioambatana na ufunguzi wa gati
katika bandari ya Mombasa, nchi za Burundi na Sudani Kusini zilialikwa
na kuwakilishwa na mawaziri wao waandamizi. Tanzania haikualikwa.
Katika hatua nyingine, juzi vyombo vya
habari viliwakariri baadhi ya mawaziri wa nchi hizo waliopewa jukumu la
kusimamia makubaliano hayo, wakieleza makubaliano hayo ni ya Jumuiya
nzima na endapo Tanzania ikipenda kuingia itakaribishwa.
Pia, Dk. Abdallah, alisema hatua
zilizochukuliwa na nchi hizo kwa kukubali kuanzisha utaratibu wa
matumizi ya viza moja na vitambulisho vya pamoja, ni mfano wa ubabe
usiokidhi matakwa ya kidemokrasia.
"Tatizo linakuja kwamba Tanzania ni nchi
ya kidemokrasia, inafanya uamuzi wa kushirikisha wananchi wake, lakini
wenzetu wanatumia ubabe ili kutulazimisha, kitu ambacho hakikubaliki,"
alisema Dk. Abdallah.
Alisema kimsingi suala hilo halikupelekwa
na kukubaliwa na nchi tano za EAC zikiwamo Tanzania na Burundi, kama
makubaliano ya jumuiya yanavyoeleza.
Alisema, kama nchi hizo zilikusudia kuwapo
utaratibu huo, zingeitisha kikao na kupata baraka za nchi zote, ili
kutoa uhuru kwa nchi zinazotaka kuanza zifanye hivyo.
"Utaratibu unaweka wazi kabisa, lazima
nchi tano zikubaliane kwanza kwa jambo lolote, hata kama ikitokea nchi
mbili au tatu zitaamua kuanza hakuna tatizo, lakini hilo halikufanyika
sisi tunasikia kwenye vyombo vya habari," alisema.
Dk. Abdallah alisema Tanzania haipingi kwa
nchi hizo kuanzisha miradi ya kimaendeleo kwa sababu ni jukumu lao kwa
ajili ya kujijenga kiuchumi.
Hata hivyo, alisema lazima miradi hiyo iwe nje ya makubaliano ya kiuchumi na biashara ya EAC.
Alisema kama miradi hiyo itahusisha katika jumuiya na kutumia rasilimali zake itakuwa kinyume na makubaliano hayo.
"Tanzania ni mwanachama muanzilishi,
inachangia jumuiya, ni makosa makubwa fedha au ufadhili ukatumika
kupitia mgongo wa chombo hicho ikiwa mwanachama mmoja hajui chochote,"
alisisitiza.
Alitolea mfano kwamba Tanzania imetekeleza
miradi kama hiyo kwa baadhi ya nchi wanachama, lakini ilifanya kama ya
nchi na nchi na haikuhusisha umoja huo.
"Tulitumia fedha zetu kwa kujenga na
kutekeleza miradi yetu, kama wenzetu wakiingiza kwenye Jumuiya itakuwa
makosa, tunashauri waendelee kufanya kama ushirikiano wa nchi na nchi
pekee," alisema.
Hata hivyo juhudi za kumpata Dk. Sezibera
kuelezea juu ya hatua hiyo ya serikali ya Tanzania haikuweza kufanikiwa
baada ya alipopigiwa simu kuonyesha kuzimwa.
Naibu Waziri aliwataka wananchi kutohamaki
wala kuwa na wasiwasi na mwenendo uliokuwapo katika EAC, akisema
viongozi wao waliopewa mamlaka wanafanya kazi kubwa ya kuhakikisha
maslahi ya Watanzania yanalindwa.
Alisema yeye na Waziri wake Samuel Sitta, wapo makini na kila kinachofanywa kinakuwa na umuhimu wa nchi.
"Tuna uhuru wa nchi kuona jambo hili
linatufaa au halitufai, hatuwezi kuburuzwa kutokana na uharaka wa watu
fulani, huo ndiyo msimamo wetu na wananchi wanatuelewa," alisema.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI