Kwa ufupi
Mbali na kufanyika kwa vitendo hivyo kituo hicho
kinadaiwa kuwa soko kubwa la biashara haramu ya dawa za kulevya aina ya
Bangi na Mirungi.
Dar es Salaam. Hali ya usalama kwenye Kituo
Kikuu cha Mabasi yaendayo Mikoani (UBT), imekuwa tete baada ya kuibuka
kwa kundi kubwa la matapeli wanaowaibia abiria na kuwabambikizia kesi
kwa kutumia njia ya ulinzi shirikishi.
Mbali na kufanyika kwa vitendo hivyo kituo hicho
kinadaiwa kuwa soko kubwa la biashara haramu ya dawa za kulevya aina ya
Bangi na Mirungi.
Kundi hilo ambalo linajulikana kama vishoka
limekuwa likifanya vitendo hivyo kuanzia saa mbili usiku kwa kujifanya
kuwa wao ulinzi shirikishi, na kufanya utapeli huo kwa kuwakamata abiria
na baadhi ya watu wanaoingia kwenye kituo hicho na kuwapa makosa
mbalimbali.
Uchunguzi uliyofanywa na gazeti hili takriban siku
tatu kwenye kituo hicho majira usiku na mchana, umebaini kwamba mchezo
huo mchafu umekuwa ukifanyika kwa muda mrefu ambapo tayari kundi kubwa
la watu wametapeliwa na kuibiwa vitu mbalimbali.
Uchunguzi huo umebaini kwamba moja ya utapeli
unaofanywa na kundi hilo la vijana wanaojiita ulinzi shirikishi, ni
kutumia pete feki za dhahabu ambazo wanazitumia kuwatapeli fedha abiria.
Pia, licha ya kufanya utapeli huo kwa kutumia
dhahabu feki, kundi hilo linatumia bidhaa ya sabuni kuwatapeli simu
abiria. Sabuni hutengenezwa kwa mfano wa simu na kuwabambika watu kuwa
ni simu halisi.
Licha ya kufanyika kwa vitendo hivyo, uchunguzi
pia umebaini kuwepo kwa biashara haramu ya dawa za kulevya aina ya bangi
na mirungi.
Uchunguzi pia umebaini kwamba vijana hao matapeli
wakimkamata mtu kwa kisingizio cha kuhusika na wizi, wanamtoza faini
kati ya Sh50,000 hadi 70,000. Makosa yanayodaiwa kuwa madogo kama
kukojoa au kutupa uchafu wanatoza faini ya kati ya Sh10,000 hadi
Sh20,000 kila siku.
Akizungumzia suala hilo Mwenyekiti wa Serikali ya
Mtaa wa Ubungo (NHC), Amani Sizia alithibitisha kuwepo kwa vitendo hivyo
vya uhalifu na kudai kwamba UBT imegeuka kuwa shamba la bibi kwa
wahalifu.
Sizia alisema: “Kwa kweli hali ya kituo cha mabasi
ya Ubungo na maeneo jirani imekuwa mbaya sana, kuna vikundi vya ulinzi
shirikishi ambavyo ni feki zaidi ya vitano. Vikundi hivyo vimekuwa
vikifanya kazi ya kuwatapeli abiria.”
Alisema kwa kuthibitisha zaidi nyakati za usiku
kila kibaka anageuka kuwa mlinzi shirikishi, na kufanya kazi ya utapeli
ili kujipatia fedha.
“Nashukuru sana ndugu yangu mwandishi kwa
kunitafuta UBT kwa sasa haifai, kuna vitendo vingi vya uhalifu ambavyo
vinafanyika nyakati za usiku. Kila kibaka ikifika wakati huo anageuka
kuwa mlinzi shirikishi,” alisema Sizia
Sizia alibainisha kwamba ukitaka kuamini matapeli hao wanafanya
kazi hiyo bila kuwa na vitambulisho, ni kwamba wanachofanya ni
kuwakamata watu na kuwaomba fedha bila hata kuwafikisha kwenye ofisi za
kata. Mwandishi wa habali hizi alithibitisha kuwepo kwa matapeli hao
baada ya kusimama sehemu moja ya eneo hilo la Ubungo na kujisaidia haja
ndogo, ambapo alikuja kijana mmoja aliyejitambulisha kuwa ni mlinzi
shirikishi na kumtaka alipe fedha.
Mwandishi alipomtaka kijana huyo aliyevalia kofia
na koti lenye rangi ya kung’aa, hakuwa nacho na kulazimisha alipwe fedha
ili amwachie.
Mwandishi alimpa Sh2,000 na kumwachia huku amkimtaka asirudie tena kufanya kosa hilo.
Gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Ulinzi
Shirikishi kituoni hapo James Mapunda, ambaye alithibitisha kuwapo kwa
vitendo hivyo vya kihalifu na kudai kuwa vinafanywa na watu
wanaojitambulisha kama walinzi jamii.
Kamanda huyo alikwenda mbali zaidi na kubainisha
kuwa licha ya kufanyika kwa uhalifu huo pia kuna vitendo vingine vya
biashara haramu ya bangi, dawa za kulevya aina ya mirungi, wizi wa
kompyuta mpakato (laptop) pamoja na biashara ya tiketi bandia.
“Ndugu yangu mwandishi hapa hapafai hata kidogo
kwani imegeuka kambi ya matapeli na wezi kwani kumekuwa na vitendo vingi
vya kihalifu vinavyofanywa na wahalifu wanaojitambulisha kama walinzi
shirikishi. Hata hivyo kumekuwa kunafanyika biashara haramu ya dawa za
kulevya,” alisema Mapunda.
Mapunda alidai kwamba vitendo hivyo vinafanyika na
kwamba haviwezi kuisha kwani kuna baadhi ya maofisa wa polisi kituoni
hapo wanatambua, kwani huwa wanalipwa posho na watu hao.
Gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi Magomeni
(OCD) Yahaya Athumani ili kuthibitisha vitendo hivyo, hata hivyo
alisema hana taarifa za kufanyika kwa utapeli huo na biashara haramu ya
dawa za kulevya.
“Tunatambua kwamba UBT kuna uhalifu mwingi ambao
unafanyika, lakini tumekuwa tukifanya doria za mara kwa mara ili
kuimarisha ulinzi,” alisema Athumani.
Kamanda Athumani alikana kuwa na taarifa za kufanyika kwa vitendo hivyo na kuahidi kufanyia kazi taarifa hizo.
“Ndugu yangu wewe ndiyo unanipa taarifa, kwa kuwa
mimi siyo msemaji wa Polisi nitafanyia kazi, kwani UBT ipo chini
yangu,”alisema.
Hata hivyo gazeti hili lina taarifa za kuwepo kwa
Polisi wanaoshirikiana na wahalifu hao kwa kulipwa posho kila wanapo
fanya vitendo hivyo.
source: Mwananchi
source: Mwananchi