
Meli ya Gold Star iiliyosajiliwa Tanzania ikiwaka moto baada ya
mabaharia wake kuichoma iliponaswa ikiwa imebeba dawa za kulevya aina ya
bangi katika pwani ya Italia juzi. Picha ya Reuters
Posted
Jumatatu,Septemba9
2013
saa
22:49 PM
Kwa ufupi
Tunashindwa kupata maneno stahiki ya kulaani
kitendo cha kusajili meli za kigeni kiholela na kuziwezesha kufanya
biashara au vitendo vya kihalifu, huku zikipeperusha Bendera ya
Tanzania.
Ni jambo la kusikitisha kwamba jina la Tanzania
limezidi kuchafuliwa mbele ya jumuiya ya kimataifa baada ya meli ya
mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa Zanzibar kukamatwa Jumamosi iliyopita
katika Bahari ya Mediterranean ikiwa na tani 30 za dawa za kulevya aina
ya bangi yenye thamani ya Sh125 bilioni.
Meli hiyo iliyokuwa ikipeperusha bendera ya
Tanzania ilinaswa na askari wa doria wa Italia waliokuwa Pwani ya Sicily
katika Bahari hiyo ya Mediterranean. Idara ya Ushuru ya nchi hiyo
ilisema, meli hiyo ilikamatwa baada ya taarifa za kiintelijensia kwamba
ilikuwa imebeba dawa hizo, lakini ikasema haikutarajia kama ingekuwa
imebeba mzigo mkubwa kiasi hicho.
Tukio hilo la aibu kubwa kwa Tanzania
limethibitishwa na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar
(ZMA), Abdi Omar ambaye alisema juzi kwamba ofisi yake iliwasiliana na
Kampuni ya Philtex yenye ofisi zake Dubai ambayo ilithibitisha kuisajili
meli hiyo mwaka 2011 kwa niaba ya Serikali ya Zanzibar kwa kazi ya
kubeba mizigo chini ya Kampuni ya Gold Star.
Alisema kutokana na tukio hilo, Kampuni ya Gold
Star imekiuka masharti ya Sheria ya Usajili wa Meli na ile ya Umoja wa
Mataifa (UN) zinazozuia meli kubeba dawa za kulevya, huku akisema ofisi
yake itafanya uchunguzi na kuchukua hatua. Jeshi la Polisi nchini
lilithibitisha kukamatwa kwa meli hiyo na kusema ilikuwa ikipeperusha
bendera ya Tanzania na kwamba ilisajiliwa na Serikali ya Zanzibar.
Tunashindwa kupata maneno stahiki ya kulaani
kitendo cha kusajili meli za kigeni kiholela na kuziwezesha kufanya
biashara au vitendo vya kihalifu, huku zikipeperusha Bendera ya
Tanzania. Hakuna ubishi kwamba usajili holela wa meli za kigeni ambao
umekuwa ukifanywa na Serikali ya Zanzibar, sio tu umeharibu jina zuri la
taifa letu mbele ya jumuiya ya kimataifa, bali pia umesababisha maafa
makubwa ambapo watu wengi wamepoteza maisha kutokana na meli hizo
kusajiliwa pasipo kukidhi vigezo vilivyowekwa kisheria.
Yafaa tujikumbushe hapa, angalao kwa muhtasari tu
jinsi usajili huo holela ulivyosababisha maafa na kuharibu jina la taifa
letu nchi za nje. Bila shaka sote tunakumbuka maafa yaliyotokea huko
Zanzibar kutokana na kuzama kwa MV Spice Islander, Septemba 10, 2011 na
MV Skaget, Julai 19, 2012 ambapo watu wengi walipoteza maisha kutokana
na ubovu wa meli hizo.
Lakini matukio mabaya zaidi yalikuwa pale meli za
Iran 36 ziliposajiliwa na Serikali ya Zanzibar wakati nchi hiyo ikiwa
chini ya vikwazo vya UN, lakini zikakwepa vikwazo hivyo kwa kujisajili
Zanzibar na kupeperusha Bendera ya Tanzania. Kwa hatua hiyo, Tanzania
iliponea chupuchupu kuwekewa vikwazo na UN na mataifa mengine, ikiwamo
Marekani. Hakuna anayejua hatua zitakazochukuliwa dhidi ya Tanzania
kutokana na kukamatwa kwa meli hiyo ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa
Zanzibar ikiwa na shehena kubwa ya dawa za kulevya, pia ikiwa
inapeperusha Bendera ya Tanzania.
Tunadhani sasa umefika wakati wa suala la usajili
wa meli za kigeni kuwa suala la Muungano. Ni hatari kubwa pale kila
upande wa Muungano unapofanya kivyake mambo nyeti kama usajili wa meli
za kigeni. Nani hajui kwamba kufanya hivyo tunahatarisha usalama wa
taifa letu?
source: Mwananchi
source: Mwananchi