Monday, 16 September 2013

`Wabunge ni majangili`

13th September 2013
  Wamo maofisa wa serikali, wafanyabiashara
  Watakaokamatwa sasa kufilisiwa mali zao
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu (katikati), akiongoza maandamano dhidi ya ujangili yaliyofanyika kutoka Ubungo mpaka Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam jana. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli na kulia kwake ni Mkurungezi Mkuu wa Idara ya Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa.
Serikali imesema miongoni mwa wanaokwamisha vita dhidi ya ujangili ni wabunge kutokana na baadhi yao kujihusisha na biashara ya pembe za ndovu.

Pamoja na kuwataja wabunge ambao ndiyo watunga sheria nchini, serikali imesema pia vita hiyo inashindwa kupata mafanikio kutokana na kuwa na mtandao mkubwa wa wafanyabiashara wakubwa na maofisa wa serikali kujihusisha na biashara hiyo.

Hata hivyo, serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), haikueleza ni jinsi gani wabunge wanavyojihusisha na biashara ya pembe za ndovu ambayo imelalamikiwa sana kutokana na kusababisha idadi kubwa ya tembo kuuawa katika Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba.

Baadhi ya maofisa hao wa serikali wametajwa  ni pamoja na wa viwanja vya ndege, idara za wanyama pori na askari wa Jeshi la Polisi.

Nyalandu aliyasema hayo jana muda mfupi baada ya kupokea maandamano ya wanaharakati wa African Wildlife Trust, ambao walitembea kutoka mkoani Arusha mpaka jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupinga ujangili dhidi ya tembo.

Nyalandu alisema watu wanaojihusisha na biashara hiyo, wana mawasiliano ya kisasa.

Alisema mbali na kuwa na mawasiliano ya aina hiyo, pia wanawatumia vijana ambao huwapa magari na vitendea kazi, zikiwamo silaha za moto.

Alisema vitu vingine ambavyo vimekuwa vikiikwamisha serikali kupambana na ujangili, ni rushwa na mmomonyoko wa maadili.

Alisema baadhi ya watumishi wa umma wanaojihusisha na ujangili wamekuwa wakifanya hivyo kutokana na kusukumwa na uroho wa kutaka utajiri wa haraka.

Kwa mujibu wa Nyalandu, kumekuwa na ongezeko kubwa la bei katika biashara hiyo kwenye masoko haramu yaliyoko Mashariki ya Kati ya Asia, kama China, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa makundi ya majangili.

Alisema kudorora kwa uchumi na ongezeko la umaskini, kumekuwa kukisababisha watu kuwa na fikra potofu na kujiingiza kwenye vitendo vya ujangili na kufanya kama sehemu ya kazi yao. 

Nyalandu alisema kiwango cha kuuawa kwa tembo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.

Alisema mwaka 2009, tembo walikuwa 350,000 na mwaka 2010 hadi 2012, walipungua na kufikia 130,000, huku mwaka huu wakiwa 378 waliouawa. Aliwataka majangili na wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara hiyo kuacha na kujisalimisha polisi.

Pia alivitaka vyombo vya usalama kushirikiana kwa pamoja na kwamba majangili hao wakikamatwa watatangazwa katika vyombo vya habari duniani kote, kupelekwa mahakamani na kutaifisha mali zao.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, alisema idadi ya tembo imepungua sana katika mbuga za wanyama nchini, hali ambayo imefanya idadi sahihi ya tembo waliobaki kutojulikana.

Lembeli ambaye pia ni Mbunge wa Kahama (CCM), alisema serikali lazima isimamie kwa umakini na si kusubiri kukaa barabarani.

Hivyo, alisema kuna haja ya kwenda kwenye mapori walipo majangili na kupambana nao ili kuepusha tembo kuendelea kuuawa kwani wanyama hao wanahitajika hasa katika suala zima la kivutio.  Lembeli alisema gari la Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi hivi karibuni lilikamatwa likiwa na pembe za ndovu, lakini  cha kushangaza dereva  ambaye alikamatwa aliachiwa baada ya kukaa siku nne mahabusu ya polisi.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Philip Mulugo, alipotakiwa na NIPASHE jana kuzungumzia suala hilo, aliahidi kulifuatilia.
 
CHANZO: NIPASHE