Na Aidan Mhando na Rachel Shempemba
Posted Jumatano,Septemba18 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumatano,Septemba18 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Ni vyama vya Siasa na Jukwaa la Katiba, sambamba na kufanikisha elimu ya mchakato wa Katiba kwa Watanzania.
Dar es Salaam. Jukwaa la Katiba Tanzania,
limesema limeungana na vyama vikuu vya upinzani nchini ili kutoa elimu
ya mchakato wa Katiba kwa Watanzania kupitia asasi za kiraia.
Pia, jukwaa hilo limeungana na vyama hivyo
kumshinikiza Rais Kikwete asisaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba Mpya uliopitishwa bungeni Septemba 6, mwaka huu.
Kauli ya kuungana na vyama hivyo ilitolewa Dar es
Salaam jana na Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Deus Kibamba baada ya kukutana
na wenyeviti wa vyama hivyo vikuu vya upinzani ngazi ya taifa.
Tamko hilo lilitolewa jana muda mfupi baada ya
kukamilika kwa kikao cha ndani kilichofanyika kati ya uongozi wa jukwaa
na wenyeviti wa vyama hivyo.
Vyama vilivyofika kwenye kikao hicho
kilichofanyika kwenye ofisi za Jukwaa la Katiba ni pamoja na Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho kiliwakilishwa na Mwenyekiti
wake, Freeman Mbowe, Chama cha Wananchi (Cuf), Profesa Ibrahim Lipumba
na Chama cha NCCR- Mageuzi, James Mbatia.
Mkutano huo ambao unaelezwa kuwa ni wa kawaida
wenye lengo la kushirikisha asasi za kiraia, ulifanyika kwa muda wa saa
tano huku waandishi wa habari wakitakiwa kusubiri nje ya ofisi hizo ili
kupewa taarifa ya mambo yaliyodaiwa yanaweza kusababisha kutengeneza
Katiba ya upande mmoja.
Mkutano huo ambao ulianza saa 3 asubuhi,
ulimalizika saa 8 mchana ambapo viongozi wa vyama vya upinzani na Jukwaa
la Katiba walitoka kwa pamoja na kutoa matamko yao.
Akizungumza baada ya kutoka kwenye mkutano huo
Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deus Kibamba alisema, lengo la kukutana na
viongozi wa vyama hivyo ni kuhakikisha mchakato wa Katiba unafanyika kwa
haki na Katiba itakayopatikana iwe ya Watanzania wote na siyo ya upande
mmoja.
Naye msemaji wa viongozi hao,Profesa Ibrahim
Lipumba alisema, ushirikiano huo umetokana na Muswada wa Marekebisho ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya kupitishwa bungeni Septemba 6, mwaka
huu, kwa nguvu na wabunge wa CCM.
Lipumba alibainisha kwamba kuanzia sasa watafanya
mikutano na asasi za kiraia ili kuungana pamoja kutoa elimu na
kushinikiza Rais Kikwete asisaini muswada huo.
Leo wanatarajia kukutana na wawakilishi wa vyama vya walemavu.
SURCE: MWANANCHI
SURCE: MWANANCHI