Thursday, 3 October 2013

Chipaka atimua waandishi

3rd October 2013
Mwenyekiti wa Tadea,John Chipata
Ziara ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuvitembelea vyama imezua mapya, baada ya Mwenyekiti wa Tadea, John Chipata, kuwafukuza waandishi wa habari waliofika katika ofisi za chama hicho akitaka wasisikilize mazungumzo kati yake na msajili.

Hatua hiyo ilikuja muda mfupi baada ya Msajili, Jaji Francis Mutungi, kufika katika ofisi za chama hicho Magomeni jijini Dar es Salaam jana mchana ukiwa ni mwendelezo wa kuvitembelea vyama hivyo na kujitambulisha.

Baada ya Jaji Mutungi kuingia katika ofisi za chama hicho akiongozana na ujumbe wake, ndipo Chipata alipoinuka kwa jazba huku akitoa kauli za matusi na kuwazuia waandishi wa habari wasiingie katika ofisi hizo.

“Siwataki waandishi wa habari hapa, sitaki makanjanja katika ofisi yangu, waandishi gani mnaandika habari ambazo siyo za kweli,” alisema Chipata.

Baada ya kutoa kauli hiyo, Chipata aliwafuata waandishi hao na kuwaambia waondoke, lakini waandishi walipogoma ndipo alipotoa amri kwa mmoja wa wajumbe wa chama hicho kuwaondoa waandishi.

Mjumbe huyo pasipo kutaja jina lake wala wadhifa alitumia lugha ya busara kuongea na waandishi hao akiwataka kuitikia wito uliotolewa na mwenyekiti wa Tadea.

“ Nisikilizeni wanangu, mwenyekiti ameshaonyesha kukasirika na ameshasema muondoke, nawaomba mimi mnyanyuke mkakae pale nje, mazungumzo yakimalizika mimi nitawaeleza yote yaliyozungumzwa,” alisema.
 
CHANZO: NIPASHE