Sunday 13 October 2013

Daktari mwenye matatizo ya akili atibu, afundisha MNH

Dk Kishiwa akiwa na mkewe, Mwajabu Chuma. Picha na Kalunde Jamal. 

Na Kalunde Jamal, Mwananchi

Posted  Jumapili,Oktoba13  2013  saa 11:29 AM
Kwa ufupi
Gazeti hili lilishuhudia daktari huyo akimwelekeza mmoja wa madaktari wa MNH namna ya kumsaidia mgonjwa wake. Kwa mujibu wa mazungumzo yao, hali ya mgonjwa husika ilimchanganya daktari huyo, hivyo kutaka kupata msaada kwa Dk Kishiwa.

Dar es Salaam. Huwezi kuamini lakini huu ndio ukweli, kwamba watu kadhaa wamekuwa wakimiminika kupata msaada wa tiba, ushauri wa kitabibu na wengine masomo ya udaktari kwa mtu ambaye imethibitika kwamba hivi sasa ana matatizo ya akili.
 Huyu si mwingine bali ni Mark Paulo Kishiwa ambaye kitaaluma ni daktari, aliyewahi kufanya kazi Hospitali za Kasulu, mkoani Kigoma na Bugando mkoani Mwanza, lakini sasa mvua na jua humwishia akiwa maeneo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Ukimwona mara kadhaa utamkuta akiimba nyimbo zisizo rahisi kuzielewa kutokana na hali anayonekana kuwa nayo ya matatizo ya akili, lakini anapokuwa sawa, hugeuka kuwa msaada kwa wengi; madaktari wa MNH ambao huomba ushauri kwake, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi za Tiba Muhimbili (MUHAS) na wagonjwa ambao hutaka ushauri pia.
Dk Kishiwa anasema: “Naikumbuka Aprili 26, 1981, ilikuwa Jumatatu ya Pasaka, ndipo nilianza kuugua. Nilijikuta nikifanya vitu visivyo vya kawaida.
Nilimwaga maji ovyo ndani, nilimwaga nguo na vitu mbalimbali, kila kitu kilikuwa ovyo. Baada ya muda niligundua kufanya vitu siyo vya kawaida…Hivyo ndivyo nilivyoanza kuchanganyikiwa na hali hii imenitokea mara kwa mara.”
Aliongeza: “Yaliponitokea hayo, nilikuwa nikifanya kazi mkoani Kigoma katika hospitali iliyopo wilayani Kasulu (hakuitaja jina) ndipo kilikuwa kituo changu cha kazi.”
Pamoja na Dk Kishiwa kuwa na matatizo ya akili, imethibitika kuwa baadhi ya madaktari wa MNH wamekuwa wakikimbilia kwake kupata ushauri, lakini kubwa ni lile la kufundisha masomo ya ziada kwa baadhi ya wanafunzi MUHAS.
Pia amekuwa akifuatwa na watu wanaomfahamu hasa wanawake wakimwomba ushauri hata kuwaandikia dawa kutokana na maradhi waliyonayo. Mwandishi wa habari hii ni mmoja wa waliopata ushauri wa kitabibu kutoka kwa Dk Kishiwa.
Tiba na ushauri
Uchunguzi wa wiki kadhaa katika eneo la MNH, nyumbani kwake Chamazi na hata katika familia yake, umethibitisha kwamba Dk Kishiwa licha ya kuwa mgonjwa wa akili bado ni msaada mkubwa kwa watu wengi.
Gazeti hili lilishuhudia daktari huyo akimwelekeza mmoja wa madaktari wa MNH namna ya kumsaidia mgonjwa wake. Kwa mujibu wa mazungumzo yao, hali ya mgonjwa husika ilimchanganya daktari huyo, hivyo kutaka kupata msaada kwa Dk Kishiwa.
Uchunguzi pia ulibaini kuwa wakati fulani, Dk Kishiwa anakuwa katika hali ya kawaida na kuweza kutoa ushauri, hata kutibu kwa kuwaandikia dawa wagonjwa akiwa eneo hilo la Muhimbili.

Jioni moja gazeti hili lilishuhudia wanawake wawili waliobeba watoto mgongoni wakiwa na Dk Kishiwa, aliyekuwa akiwaandikia kitu kwenye karatasi. Baada ya tukio hilo mwandishi aliwauliza iwapo wanamfahamu, na walijibu; “Tunamfahamu, ni daktari alikuwa akituandikia dawa.”
Hata hivyo, uchunguzi ulibaini kuwa mambo yanapobadilika, Dk Kishiwa huwa mkali asiyetaka kuwa karibu na mtu au kuzungumza naye, huku akifanya vioja vinavyothibitisha hali yake ya matatizo ya akili. Hali hiyo ilimlazimisha mwandishi kuendelea kumfuatilia kwa siku kadhaa katika eneo hilo la MNH na kufanikiwa kuzungumza naye.
Kwa mujibu wa watu wanaomfahamu hasa madereva teksi wa eneo hilo, walisema Dk Kishiwa hushinda hapo na kwamba pamoja na kuwepo kwa wafanyabiasha na madereva wengi, daktari huyo humsikiliza dereva mmoja anayepatana naye na mara nyingi hutekeleza anayomweleza.
Kwa msaada wa dereva huyo, Dk Kishiwa anaeleza historia ya maisha yake kuwa alizaliwa Desemba 25, 1954, alipata elimu katika Shule ya Msingi Tumbi mkoani Tabora hadi darasa la nane na kuendelea na masomo kupitia shule kadhaa ikiwemo Sekondari ya Busonga na Sekondari ya St Mary’s ya Tabora.kwamba katika elimu ya sekondari alipata daraja A kwa masomo yote 11.
“Sikuwahi kufeli, nilipata daraja A katika masomo yote 11 niliyosoma yakiwemo kemia, baolojia, hisabati na civics. Baada ya hapo nilijiunga na jeshi kwa mujibu wa sheria kwa miezi sita katika kambi ya Mafinga,” anasema Kishiwa bila kutaja miaka aliyosoma.
Anakumbuka kuwa 1974 ndipo alijiunga na Chuo cha Tiba Muhimbili, ambapo alisoma kwa miaka mitano na kumaliza 1979, bila kufeli somo hata moja na baada ya hapo alipangwa kwenda Hospitali ya Bugando, Mwanza kikiwa ni kituo chake cha kazi cha kwanza.
Anasema alikaa Bugando kwa mwaka mmoja tu na mwaka uliofuata akapelekwa Wilaya ya Kasulu, Kigoma kama Mganga Mfawidhi na huko ndipo lilipoanzia tatizo alilonalo hadi sasa.
Itaendelea Jumapili ijayo…..

SOURCE: MWANANCHI