Tuesday, 15 October 2013

HATARI: Ripoti ya UN yaianika Serikali

Naibu waziri wa fedha, Saada Salum 

Na Goodluck Eliona, Mwananchi

Posted  Oktoba12  2013  saa 7:48 AM
Kwa ufupi
Siku za hivi karibuni baadhi ya viongozi wakubwa duniani wamekuwa wakizitaka Serikali kutunga sera za maendeleo zitakazoendana na hali halisi ya maisha ya watu wa eneo husika.


Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikitajwa kuwa ni miongoni mwa nchi zenye amani na utulivu, imebainika kuwa Watanzania ni miongoni mwa watu wasio na furaha na waliokata tamaa hapa duniani.
Ripoti inayoonyesha orodha ya nchi zenye furaha duniani ya mwaka 2013 (World Happiness Report 2013), imeitaja Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi 10 za mwisho duniani kati ya nchi 156 zilizofanyiwa utafiti huo.
Ripoti hiyo iliyoandaliwa na kundi la wataalamu kutoka Umoja wa Mataifa (UN), kati ya mwaka 2010 na 2012, inaonyesha kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 151 ikiburuta mkia pamoja na nchi za Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Benin na Togo.
Upatikanaji wa huduma za jamii, mtazamo wa watu kuhusu rushwa, umri wa kuishi, ukosefu wa kazi, pato la taifa na ukarimu wa watu katika nchi husika, ni baadhi ya vigezo vilivyoangaliwa wakati wa kuandaa taarifa hiyo.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alieleza kushtushwa na ripoti hiyo kwa maelezo kwamba ni asilimia 11.7 tu ya Watanzania wasio na ajira na kwamba wale wanaofanya kazi, wanapata huduma zote za msingi, ikiwa ni pamoja na kwenda likizo na mishahara inayolingana na taaluma zao.
“Watanzania wana furaha, kwa upande wa wafanyakazi wanapata haki zao zote wanazostahili, sijui ni vigezo vipi wametumia…kwa mujibu wa takwimu za 2006 ni asilimia 11.7 ya Watanzania ndio waliokuwa hawana kazi, lakini wakati huo idadi ya watu ilikuwa ndogo, hivi sasa imeongezeka,” alisema Kabaka na kuongeza:“Usafiri ndiyo tatizo linalowasumbua wafanyakazi wengi kwa kuwa wanachelewa kwenda kazini.”
Naye, Naibu Waziri wa Fedha, Saada Salum alisema pamoja na vigezo vingine vilivyotumika kutambua furaha ya Watanzania, umaskini ndiyo unaoweza kuwa chanzo cha Tanzania kushika nafasi za mwisho.
“Inategemea na vigezo vingine walivyovitumia, nakubali kuwa Tanzania ni maskini pengine hali hiyo imeifanya nchi kushika nafasi ya mwisho,” alisema Salum.
 
Nchi zilizoongoza
Taarifa hiyo imezitaja nchi tano; Denmark, Norway, Uswisi, Netherlands na Sweden kuwa ndizo zinazoongoza kwa watu wake kuwa na furaha zaidi duniani, huku Angola ikishika nafasi ya kwanza Afrika na ya 61 duniani ikifuatiwa na Algeria (73), Libya (78), Ghana (86), Zambia (91), Lesotho (98), Morocco (99) na Swaziland (100).
Kwa upande wa Afrika Mashariki, wananchi wa Uganda ndio walionekana kuwa na furaha zaidi kwani nchi hiyo imeshika nafasi ya 120 wakifuatiwa na Kenya (123), Tanzania (151), Rwanda (152) na Burundi (153).
Ripoti hiyo inabainisha kuwa kati ya mwaka 2005 na 2012, nchi 60 duniani ziliongeza viwango vya furaha kwa watu wake, kati ya hizo 16 zikiwa barani Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Nchi 29 zilibaki katika viwango vya awali, huku watu kutoka nchi 41 wakipunguza viwango vyao vya furaha.
Ikilinganishwa na ripoti ilifanywa kati ya 2005 – 2007, Tanzania imeshuka kutoka asilimia 40 hadi 37. Ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia 10 ya watu duniani wanasumbuliwa na matatizo ya akili ambayo yamewasababisha kukosa furaha.
Hata hivyo, imebainika kuwa mtu mmoja anaweza kukosa furaha kutokana na sababu zaidi ya moja.
“Mtu mmoja anaweza kukosa furaha kutokana na sababu mbalimbali kama umaskini, ukosefu wa kazi, kuvunjika kwa ndoa na kusumbuliwa na ugonjwa. Lakini sehemu kubwa, matatizo sugu ya akili yamesababisha kukosekana kwa furaha,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Alipoulizwa kuhusu ripoti hiyo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi alisema bado hajaiona na kwamba atakapoisoma atakuwa tayari kuizungumzia.
“Sijaiona ripoti hiyo kwa hivyo siwezi kusema chochote hadi niione, wewe si umeiona ndiyo maana ukatupa maswali?” alihoji Dk Mwinyi.
Wataalamu wanena
Mwanasaikolojia Modesta Kimonga, alisema Watanzania wengi wanakuwa na hasira kila wakati kutokana na kukosa matumaini, baada ya mambo yao kushindwa kufanikiwa.
Alisema hali hiyo inatokana na watu wengi kushindwa kudhibiti magonjwa na matatizo mengine yanayowakabili.
“Watanzania wengi wanasumbuliwa na mood disorder, wanakuwa wakali, wenye hasira kila wakati. Mambo yao hayaendi wamekosa tumaini. Hali hiyo inawakumbwa hata watoto ambao wanakosa mahitaji yao ya msingi,” alisema Kimonga.
Hata hivyo, ripoti hiyo inaeleza kuwa zipo sababu mbalimbali zinazowafanya watu kuwa na furaha: “Wanauchumi wanasema furaha inaletwa na kipato kikubwa, wanasaikolojia wanaamini furaha inakuja baada ya mtu kuwa na afya njema na viongozi wa dini wanaamini furaha huletwa na maadili mema,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Honest Ngowi alisema kuna uhusiano wa karibu kati ya umaskini na furaha, kwa kuwa mtu asiye na kipato cha kununua mahitaji yake ya msingi hawezi kuwa na furaha.

“Gharama za bidhaa zipo juu, mtu masikini hawezi kuwa na furaha, hata hivyo haimaanishi kuwa nchi tajiri ndizo zenye furaha. Nchi kama Norway pamoja na kuwa na uchumi mzuri, lakini ina idadi kubwa ya watu wanaojinyonga,” alisema Ngowi.
Akizungumzia ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii, Costantine Akitanda, alisema taarifa hiyo iko sahihi na kwamba karibu kila Mtanzania analalamika.
“Ukichunguza utagundua kuwa karibu kila Mtanzania analalamika. Hata sera zilizopo hazina mfumo unaowawezesha watu kunufaika na maliasili za taifa,” alisema Akitanda.
Pamoja na msukosuko wa uchumi ulioitikisa dunia kuanzia mwaka 2008, dunia imeshuhudia watu wakiongeza viwango vyao vya furaha kutokana na sababu mbalimbali kulingana na mahali nchi ilipo.
Mkazi wa Mabibo, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Vick Manonge, alisema ripoti hiyo inaonyesha hali halisi ilivyo hivi sasa hapa nchini, kwa kuwa watu wengi wanaonekana kuwa na hasira.
“Kama kuna mtu hakubaliani na hilo (ripoti hiyo) aangalie kwenye daladala watu walivyo na hasira bila sababu ya msingi, mwingine hataki aulizwe hata nauli, “ alisema Manonge.
Katika siku za hivi karibuni baadhi ya viongozi wakubwa duniani wamekuwa wakizitaka Serikali kutunga sera za maendeleo zitakazoendana na hali halisi ya maisha ya watu wa eneo husika, ili kuweka mazingira yatakayowaletea wananchi furaha.
Baadhi ya huduma zinazotolewa na serikali ni afya, kutengeneza ajira, elimu na kuweka mazingira bora ya kujiwezesha kichumi kwa kila Mtanzania.

SOURCE: MWANANCHI