Tuesday, 15 October 2013

Kikwete: Tumeshinda maadui zetu

Rais Jakaya Kikwete akizungumza na wabunge wa Chadema, Chiku Abwao na Mchungaji Peter Msigwa (kushoto) mjini Iringa, jana wakati wa sherehe za kuhitimisha mbio za Mwenge. Picha ya ikulu 
Na Waandishi Wetu, Mwananchi

Posted  Jumanne,Oktoba15  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
“Tunataka tuwe na Katiba itakayojenga, siyo kubomoa, kutugawa kwa misingi ya kiitikadi,” alionya Rais Kikwete.


Dar/Iringa. Rais Jakaya Kikwete amesema maadui wote ambao walitaka kupandikiza chuki miongoni mwa Watanzania kwa lengo la kuvuruga amani ya nchi wamedhibitiwa .
Rais Kikwete alisema kuwa Serikali yake itaendelea kulinda amani ya nchi na maadui wote wanaohusika na kutaka kuvuruga nchi watachukuliwa hatua kali za kisheria. “Kulikuwapo na upepo mbaya, lakini kwa sasa Tanzania ni shwari na tumemshinda adui,” alisema Rais Kikwete jana kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere yaliyoandamana na sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru, mkoani Iringa.
Alisema katika siku za hivi karibuni, maadui wasioitakia mema Tanzania walikuwa na mkakati wa kuvuruga amani ya nchi, lakini Serikali kwa kushirikiana na vyombo vya dola vimewadhibiti na nchi iko salama.
Rais Kikwete alisema kuwa Serikali haiwezi kuvumilia vitendo vya uvunjifu wa amani kwa sababu inajua wazi kwamba nchi ikiingia kwenye mgawanyiko, mshikamano utavurugika na shughuli za maendeleo zitasimama.
Katiba Mpya
Rais Kikwete alisema mwaka 2014 ni mwaka wa kipekee kwa nchi kwa kuwa utakuwa na mambo makubwa matatu yatakayofanywa.
Rais Kikwete alisisitiza kwamba Katiba Mpya ni lazima ikamilike mwakani kama mambo yatakwenda kama ilivyopangwa.
Vilevile, alisema mwakani Tanzania itasherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyoondoa udhalimu na kuwarudishia Wazanzibari heshima ya mwanadamu na utu wake.
“Pia tutasherehekea miaka 50 ya Muungano wetu. Nawaomba Watanzania wajiandae kuyafanikisha vizuri mambo hayo ili historia mpya ifunguliwe nchini.
“Wazanzibari waanze miaka mingine baada ya miaka hamsini ya uhuru wao, muungano uanze miaka mingine baada ya miaka hamsini na Katiba Mpya itupeleke miaka mingine tukiwa wamoja,” alisema Kikwete.
Rais Kikwete alionya kuwa asingependa mchakato wa kupata Katiba Mpya uligawe taifa na kuleta mfarakano utakaovunja umoja wa kitaifa badala ya kuuimarisha.
“Tunataka tuwe na Katiba itakayojenga, siyo kubomoa, kutugawa kwa misingi ya kiitikadi,” alionya Rais Kikwete.

Alisema kuwa kaulimbiu ya maadhimisho ya Kumbukumbu ya Baba wa Taifa kwa mwaka huu ni kusisitiza mshikamano wa kitaifa unaopinga mbinu zozote za kuligawa taifa. “Kaulimbiu ya mwaka huu; Tanzania ni wamoja, tusigawanywe kwa misingi ya tofauti zetu za dini, itikadi, rangi au rasilimali,” alisema Rais Kikwete.
Alisisitiza kuwa amekusudia mabadiliko ya Katiba ambayo mchakato wake unaendelea yawe ya kulipeleka mbele taifa kimaendeleo kwa zaidi ya miaka 50 ijayo.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alisema atapendelea kuona Katiba Mpya inazinduliwa Aprili 13, mwakani, siku ambayo ni kumbukumbu ya kuzaliwa Baba wa Taifa.
Alisema kitendo hicho kitaienzi zaidi siku hiyo na kuandamana na mpango wa kubadilisha maadhimisho ya kitaifa ya kumkumbuka Mwalimu Nyerere kutoka Oktoba 14 siku aliyofariki na kuwa Aprili 13, siku aliyozaliwa.
..ataka kuvuruga Mwenge
Maadhimisho ya Mwenge nusura yaingie dosari baada ya mwanamume kujichomeka katika kundi la wanahabari akiwa na lengo la kumdhuru kiongozi wa Mbio za Mwenge.
Kitendo hicho kilifanyika wakati Rais Kikwete akiwa tayari ameshuka chini katika jukwaa dogo akisubiri kukabidhiwa mwenge huo, mtu huyo alichomoka kutoka katika kundi la waandishi wa habari na kujaribu kumvamia kiongozi wa Mbio za Mwenge, Juma Ali Sima aliyekuwa ameshikilia Mwenge huo.
Hata hivyo, jitihada za mtu huyo za kutaka kumvamia kiongozi wa Mwenge zilikwama baada ya kudhibitiwa vikali na askari waliokuwa wakilinda amani uwanjani hapo.
Katika kipindi hicho, Rais Kikwete pamoja na wasaidizi wake wengine walikuwa mita kama tisa kutoka katika eneo la tukio akisubiri kukabidhiwa Mwenge huo.
Rais Kikwete alisema kilele cha maadhimisho ya Mbio za Mwenge kimefanywa kuwa pia siku ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere tangu afariki miaka 14 iliyopita.
Alisema Watanzania wote bila kujali vyama vyao wana wajibu wa kuyakumbuka mema yote ya Mwalimu Julius Nyerere ikiwa ni pamoja na mafundisho yake.
Rais pia alisema ili kumkumbuka zaidi Mwalimu Nyerere alipendekeza siku yake ya kuzaliwa ndiyo iitwe Nyerere Day na ianze kusherehekewa kwa mbwembwe, iwe na mijadala ya kazi zake na itumiwe kufanya shughuli mbalimbali za kujenga taifa kwa lengo la kumuenzi.


Kuhusu dawa za kulevya
Katika maadhimisho hayo, Rais Kikwete alizungumzia mkakati wa Serikali yake wa kupambana na dawa za kulevya kwamba kitaanzishwa chombo maalumu kwa ajili ya kazi hiyo.
Alisema kazi ya kupambana na dawa za kulevya ni ngumu na hatari kutokana na wanaofanya kazi hiyo kuwa na fedha nyingi, lakini Serikali itawalinda wote.

SOURCE: MWANANCHI