Na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Posted Jumanne,Oktoba15 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumanne,Oktoba15 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
“Huwezi kusema kufanya kazi kila siku watahitaji
kuongezewa fedha, hapana kwani wanalipwa fedha nyingi. Nitaendelea
kufanya mawasiliano nao kuona ni jinsi gani suala hili tunaweza
kulimaliza.”
Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe ameitupia lawama Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) kwa kile
alichokieleza kulala kwao siku za mapumuziko na sikukuu kunarudisha
nyuma ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam.
Waziri Mwakyembe aliyasema hayo jana wakati wa
ziara ya kikazi bandarini hapo akiwa ameongozana na Mkurugenzi Mtendaji
Mkuu wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Omari Issa.
Mwakyembe alisema watendaji na viongozi wa
bandari, wamekuwa wakifanya kazi saa 24 ili kuhakikisha meli zinashusha
mizigo haraka na wahusika wanachukua mizigo hiyo pasipo vikwazo.
“Bandari wanafanya kazi saa 24 kwa siku saba za
wiki bila kupumzika, lakini wenzetu wa TRA wao sikukuu na siku za mwisho
wa juma wanalala hali hii inaturudisha nyuma kimapato,” alisema Dk
Mwakyembe.
Aliongeza: “Nchi bado ipo nyuma, tunahitajika
kuchapa kazi usiku na mchana kuhakikisha tunasonga mbele na hii
itafanikiwa ikiwa kila mmoja atatekeleza wajibu wake ipasavyo.”
Alisema kama TRA wataanza kufanya kazi kila siku, hakuna shaka kwamba taasisi za fedha (benki) nazo zitaiga hatua hiyo.
“Huwezi kusema kufanya kazi kila siku watahitaji
kuongezewa fedha, hapana kwani wanalipwa fedha nyingi. Nitaendelea
kufanya mawasiliano nao kuona ni jinsi gani suala hili tunaweza
kulimaliza.”
Aidha, amewataka wamiliki wa Bandari Nchi Kavu
(ICDs), kufanya kazi ya kutoa mizigo ya wateja wao kila siku ili
kuepusha usumbufu usio wa ulazima.
“Unakuta mtu anahitaji kutoa mizigo yake lakini
wahusika siku za mapumziko hawafanyi kazi. Kwa nini wasifanye kazi kila
siku kama bandari,” alihoji Mwakyembe.
Naye Mtendaji Mkuu wa BRN, Omari Issa alisema
ameamua kufanya ziara hiyo kujionea changamoto wanazokutana nazo ili
kuona ni jinsi gani wataweza kuzitafutia ufumbuzi.
Kwa upande wake Meneja wa Bandari, Awadhi Massawe
alisema changamoto wanazokabiliana nazo ni ufinyu wa maeneo ya kuhudumia
meli na kuhifadhi shehena za mizigo.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI