Posted Jumanne,Oktoba22 2013 saa 12:48 PM
Kwa ufupi
Maendeleo ya Tehama yamefanya gharama za kutengeneza
na kumiliki wavuti kushuka, huku watengenezaji wake wakiwa karibu na
wateja.
Katika dunia ya leo, watu hususan
wafanyabiashara kuwa na wavuti (website) sio jambo la anasa wala la
hiari. Kwa walio makini wavuti ni jambo la lazima.
Maendeleo ya Tehama yamefanya gharama za
kutengeneza na kumiliki wavuti kushuka, huku watengenezaji wake wakiwa
karibu na wateja.
Kila kona katika miji yetu wapo wataalamu
wanaoweza kutengeneza wavuti, achilia mbali kampuni za Tehama kama vile
Wordpress na Blogspot zinazowawezesha watumiaji wake kuwa na wavuti bila
ya kulipia gharama yoyote.
Hata hivyo, kumiliki wavuti sio mwisho wa safari.
Wamiliki wengi wana wavuti, lakini hazifanyi kazi kwa kuwa zimelala
usingizi mnono. Kwa wenye biashara wavuti ni sehemu ya kujitangaza na
pia njia mojawapo ya kuwasiliana na wateja.
Makala haya yanakusudia kuainisha makosa kadhaa
yafanywayo na wamiliki wa wavuti na namna ya kuyaepuka kwa minajili ya
kuupa mafanikio wavuti wako.
Kukosa mwelekeo
Japo wavuti katika dunia ya sasa, ni sehemu ya
biashara, wamiliki wengi hapa nchini hawajui nini kifuate baada ya kuwa
na wavuti. Wengi huishia kwenye hatua ya kuwa na wavuti pekee.
Hivi umejiuliza kwa nini uliamua kuwa na wavuti? Haingii akilini kama jibu lako litakuwa ulifanya hivyo ili tu nawe uonekane.
Ili uweze kuona matunda ya wavuti, lazima ujue
lengo na mwelekeo wako. Kwa wenye biashara, mwelekeo huo lazima uende
sambamba na biashara husika. Kwa mtazamo wangu sioni tija ya kuwa na
wavuti kama mtu hatojali maslahi hasa yale ya kibiashara.
Kutokutumia takwimu
Takwimu ni mojawapo ya vitu muhimu kwenye wavuti
wowote. Hata hivyo, wengi hawajui umuhimu wake achilia mbali namna ya
kuzitumia.
Swali muhimu, kama hujui idadi ya watembeleaji wa
wavuti wako, wanafanya nini wakiwa huko au wanapendelea kurasa zipi za
wavuti; utawezaje kupima uwezo wa wavuti uliouanzisha?
Kimsingi, takwimu hutoa picha halisi ya matumizi ya watembeleaji
wa wavuti wako. Aidha takwimu zitakujulisha tabia za wateja wako,
kurasa wanazopendelea, mahala walipo na hata muda wanaopenda kufungua
wavuti wako.
Angalia mfano huu. Unamiliki wavuti kuhusu mgahawa
uliopo Arusha, lakini kwa kutumia takwimu unabaini asilimia kubwa ya
watembeleaji wanapatikana mkoani Dar es Salaam. Kwa mfanyabishara makini
hii ni taarifa ya kuifanyia kazi kwa maendeleo ya mgahawa.
Ili kutatua tatizo hili, unashauriwa kutumia
programu za takwimu, huku ukitafuta wataalamu wanaoweza kukutafsiria
maana ya takwimu hizo kwenye lugha ya kibiashara zaidi.
Katika wavuti nyingi hivi leo,wahusika wameweka
takwimu kuhusu watembeleaji pekee. Idadi pekee haitoshi kwani kuna mengi
yanayopaswa kujulikana ili hatimaye yaweze kufungamanishwa na bishara
na hata uwekezaji kwenye Tehama.
Kukosekana sehemu ya kutafuta taarifa
Kwa wavuti kubwa zilizo na vitu vingi au kufanyiwa
mabadiliko ya mara kwa mara, sehemu ya kutafuta taarifa (search button)
ni lazima.
Sehemu hii sio tu itasaidia kuokoa muda wa
watembeleaji wa wavuti ambao hawana muda wa kuanza kujaribu kurasa moja
hadi nyingine, lakini pia utasaidia kuongeza muingiliano kati ya wavuti
na watembeleaji.
Cha muhimu hakikisha unakuwa na sehemu ya kutafuta
taarifa kwenye wavuti wako. Pia hakikisha unaunganisa kitafuto hiki na
mitambo ya takwimu, ili kukupa picha halisi ya vitu gani ambavyo watu
wanavitafuta kwa kiasi kikubwa kwenye wavuti.
Zingatia mfano ufuatao; Una wavuti kuhusu saluni
ya kinamama, ukiwa na sehemu ya kutafuta taarifa na kisha takwimu
zikaonyesha watu wengi wanatafuta bidhaa X, taarifa hiyo itakuwezesha
kuboresha mpango wa biashara yako.
Kurasa zisizoweza kutambazika
Kimsingi watu wengi wanapotafuta taarifa kwenye
wavuti, hawasomi bali wanatambaza (scan) na huondoka mara wanapokosa
taarifa husika. Hapa kuna kosa linalofanywa na wamiliki wa wavuti hasa
Tanzania.
Wamiliki wengi wanashindwa kutoa picha ya website
yao kwa jicho la kwanza. Wavuti na blogu nyingi za Tanzania zimejaa vitu
vingi kiasi msomaji anashindwa aanzie wapi.
SOURCE: MWANANCHI
Ilivyo hutakiwi kuandika maneno milioni moja ili kumfanya mtu
atumie wavuti wako. Watembeleaji hawana muda wa kuanza kudokoa kitu
kimoja kimoja. Wengi wanadhani, kuwa na makala nyingi ndio kufanikiwa.
Andaa taarifa inayojitosheleza katika njia nyepesi na rafiki zaidi.
Kukipa kisogo Kiswahili
Inasikitisha kuona wamiliki wengi wakitumia lugha
ya Kiingereza kwenye wavuti zao ambazo kimsingi wateja wao wakubwa ni
watumiaji wa lugha adhimu ya Kiswahili.
Inawezekana matumizi ya Kiingereza yakawa mujarabu
zaidi ikiwa biashara husika ni ya kimataifa, lakini kama biashara ama
taarifa inahusu zaidi Watanzania ambao wengi wanatumia Kiswahili, hakuna
haja ya kutumia lugha ngeni.
Matumizi ya lugha ipi inafaa kwenye wavuti
yategemee vitu kama vile lengo na mwelekeo wa wavuti na nani unawalenga.
Ukijiuliza haya utakuwa na nafasi nzuri ya kuchagua lugha ya kutumia
katika wavuti wako.
Wapo wanaotumia lugha zaidi ya moja kufikisha taarifa kwenye wavuti zao. Ni jambo la kupongeza na la kuigwa.
Mkata Nyoni ni mtaalamu wa Menejimenti ya Teknolojia ya Habari na Mshauri wa Biashara.
Anapatikana kupitia barua pepe: mnyoni@dudumizi.com
Anapatikana kupitia barua pepe: mnyoni@dudumizi.com