Na Sweetbert Lukonge, Mwananchi
Posted Jumanne,Oktoba22 2013 saa 12:6 PM
Posted Jumanne,Oktoba22 2013 saa 12:6 PM
Kwa ufupi
Mashabiki 57,422 walishuhudia pambano hilo na kuingiza Sh500 milioni.
Dar es Salaam. Furaha ya kupita kiasi ndiyo
iliyosababisha zaidi ya watu 20 kuzimia uwanjani wakati walipokuwa
wakishuhudia mchezo wa Ligi Kuu kati ya Simba na Yanga uliofanyika juzi
Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo uliokuwa umejaa na presha kubwa
kuanzia kwa wachezaji hadi kwa mashabiki wa pande zote mbili ulimalizika
kwa timu hizo kufungana mabao 3-3.
Kwa mujibu wa Kiongozi wa Kikosi cha Maafa cha
Msalaba Mwekundu, Bushiri Mgamba aliyekuwa akiongoza kikosi cha huduma
ya kwanza uwanjani hapo alisema kuwa sababu kubwa ya watu hao kuzimia
ilitokana na kuwa na furaha kupita kiasi.
Alisema baadhi ya watu wanapokuwa na furaha kupita
kiasi wanapatwa na hali hiyo, lakini siyo kwa kila mtu na ndiyo maana
hiyo juzi waliozimia uwanjani hapo walikuwa wachache ingawa waliokuwa na
furaha walikuwa ni wengi.
“Hali hiyo pia inaweza kuzuilika, ambapo ni mtu mwenyewe anaweza kujizuia ili isimpate,” alisema Mgamba.
Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa kikosi hicho cha
maafa cha Msalaba Mwekundu ambaye pia aliwahi kuwa daktari wa timu ya
Yanga, Juma Sufiani aliliambia gazeti hili kuwa katika mechi hiyo watu
wengi walizimia kipindi cha kwanza.
Alisema watu hao walipatwa na hali hiyo baada ya
Yanga kufunga bao la pili na lile la tatu, mabao ambayo yalipachikwa
wavuni na Hamis Kiiza.
“Mabao hayo yalisababisha watu hao kuzimia ambao
wengi wao walikuwa ni mashabiki wa Yanga kwani walikuwa na furaha kupita
kiasi na kujikuta wakizimia.
“Pia katika kipindi cha pili cha mchezo huo hali
hiyo ilihamia upande wa mashabiki wa Simba, ambapo napo baadhi yao
walizimia, ilikuwa ni baada ya timu hiyo kupata bao la pili na la tatu
yaliyofungwa na Joseph Owino na Gilbert Kaze,” alisema Sufiani.
Aliongeza kuwa, ‘‘Watu hao walipatiwa huduma
uwanjani hapo na hali zao ziliendelea vizuri na hadi kufikia jana
kulikuwa hakuna taarifa yoyote mbaya.”
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), Angetile Osiah aliliambia gazeti hili kuwa hali hiyo ilikuwa ni
ya kushangaza, lakini walikuwa wamejipanga vilivyo kukabiliana na tukio
lolote ambalo lingetokea uwanjani hapo.
“Tulikuwa tumejipanga vizuri kabisa, watu wa
huduma ya kwanza walikuwapo wa kutosha na wote waliopatwa na hali hiyo
walipatiwa huduma, ni matumaini yetu kuwa hali zao ni nzuri kwani hadi
sasa hatuna taarifa yoyote mbaya,” alisema Osiah.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI