Na Julieth Ngarabali, Mwananchi
Posted Jumanne,Oktoba22 2013 saa 12:41 PM
Posted Jumanne,Oktoba22 2013 saa 12:41 PM
Kwa ufupi
Mazingira ya elimu yakiboreshwa na kuwa rafiki kwa
walemavu, katu ulemavu hauwezi kuwa kikwazo kwa watu wenye ulemavu
kushindwa kusoma.
Mkakati wa kitaifa wa utekelezaji wa Mpango wa
Elimu Jumuishi, utaleta manufaa na mabadiliko chanya ya kielimu kwa
watoto wenye ulemavu, ikiwa utatekelezwa kama ulivyopangwa kuanzia
uboreshaji wa miundombinu, vifaa, watumishi wa elimu na walimu.
Pia mkakati huo usipochakachuliwa, utaleta
uaminifu zaidi kwa familia nyingi zenye watoto wenye ulemavu, hivyo
kuwasukuma kuwapeleka watoto wao shuleni, kwani wataamini katika ubora
wa malezi ya walimu kwa watoto hao.
Mbali na ubora wa malezi ya walimu, imani ya
wazazi katika kuwapeleka watoto walemavu shuleni, itaongezeka kama
shuleni kuna vifaa vya kutosha na miundombinu iliyoandaliwa kwa ajili ya
kundi hilo la wanafunzi.
Kisa cha Edson Kunambi
Mazingira ya elimu yakiboreshwa na kuwa rafiki kwa
walemavu, katu ulemavu hauwezi kuwa kikwazo kwa watu wenye ulemavu
kushindwa kusoma. Hili limejidhihirisha kupitia kwa mtoto mwenye ulemavu
wa kutokusikia na kusema, Edson Kunambi (13), mkazi wa Kibaha ambaye
katika makala haya anaonyesha furaha na mafanikio anayoyapata baada ya
kuchanganywa katika darasa moja na watoto wengine wasio na ulemavu
Akizungumza na gazeti hili kwa lugha ya alama,
huku akitafsiriwa na mwalimu wake Idd Besha, Kunambi anayesoma darasa la
tano, anasema anapenda kusoma katika shule jumuishi kwa sababu watoto
wengi wako makini kujisomea, tofauti na ilivyo katika shule maalumu za
watu wenye ulemavu.
Tofauti na shule aliyokuwepo awali, anasema katika
darasa ya elimu jumuishi kila mtoto anajishughulisha kujifunza iwe kwa
kusoma, kuchora au kufanya hesabu.
Akiwa na umri wa miaka minne, anasema alipelekwa
kusoma elimu ya awali katika shule ya watoto wenye ulemavu wa uziwi
Buguruni Dar es Salaam, ambako alisoma hadi darasa la tatu. Badaye
akahamishiwa katika shule jumuishi anayosoma sasa ampapo mwaka huu yuko
darasa la tano.
Akishirikiana vyema na wanafunzi wenzake, Kunambi
amekuwa moto wa kuotea mbali darasani kwa kuwa na matokeo mazuri
kushindwa wanafunzi wengi wasio na ulemavu. Kwa mfano, anasema mwaka
2012 alishika nafasi ya pili darasani.
“Mwaka huu 2013 sikufurahi sana maana nimekuwa wa 17 darasani,’’ anasema.
Mama yake mzazi, Onoratha Kunambi anasema mtoto
wake huyo ni mzaliwa wa kwanza katika familia ya watoto watatu, lakini
ni yeye tu mwenye ulemavu wa kutokusikia na kuzungumza.
Anaeleza kuwa Edson alizaliwa miaka 13 iliyopita
kwa njia ya kawaida. Alipofikisha miezi minane na wiki mbili alianza
kusumbuliwa sana na mafua. Baadaye hata alipokuwa akilia hakutoa sauti,
huku mdomo ukimjaa mate mengi.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI