Wizara ya Ulinzi na JKT itaendelea kuboresha mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria. Hatua hii inafuatia kurejeshwa upya kwa mafunzo hayo kama Serikali ilivyokuwa imeahidi.
Mafunzo hayo yaliyoanza mapema 2013 yanatarajiwa kuwahusisha vijana 41,341 waliomaliza kidato cha sita katika shule mbali mbali nchini. Katika awamu ya kwanza vijana 5,000 (12%) walitakiwa kuhudhuria mafunzo kwa muda wa miezi mitatu kuanzia mwezi Machi 2013 hadi Juni 2013.
Awamu ya pili ya mafunzo hayo iliyoanza mwezi Juni JKT ilitarajiwa kuchukua vijana 10,000 (24%) na kumaliza mafunzo yao mwezi Septemba 2013. Katika awamu ya tatu itakayoanza mwezi Oktoba 2013 JKT itachukua vijana 15,000 (37%).
Aidha, awamu ya nne JKT itachukua vijana 11,341 (27%) mwanzoni mwa Januari 2014 na vijana hao watamaliza mafunzo mwezi Aprili, 2014 na hivyo kukamilisha idadi ya vijana waliomaliza kidato cha sita kwa mwaka 2013.
Utoaji wa mafunzo haya kwa miezi mitatu mitatu unafuatia maagizo ya Serikali kwani kwa muda wa miezi sita iliyokusudiwa wakati wa kurejesha mafunzo hayo ni wazi vijana wengi wasingepata fursa hiyo adhimu.
Changamoto kubwa zinazolikabili JKT ni pamoja na hofu wanayokuwa nayo wazazi kutokana na visingizio wanavyopewa na vijana baada ya kuwasili makambini. Tunawaasa wazazi kutojengewa hofu kwa taarifa zisizo rasmi wanazopewa na watoto wao kwani Wizara ilizifanyia kazi hofu zilizoelezwa na vijana na kubaini kuwa hazina ukweli. Kwa mfano, mtoto anadai kuwa anaumwa na hapati matibabu, lakini tunapofuatilia tunamkuta yupo kwenye gwaride (mzima wa afya).
Cha kufurahisha baadhi ya vijana hao hao wakati wa kumaliza mafunzo wamekuwa hawana haraka tena ya kuondoka makambini! Pili, lipo tatizo la kukwepa mafunzo (dodging). Mfano katika awamu ya kwanza tulitarajia kupokea vijana 5,000 lakini waliojitokeza ni 4,712 (vijana 288 wakiwa wamekwepa mafunzo). Katika awamu ya pili kati ya vijana 10,000 ni vijana 9,510 tu ndio waliojitokeza, (watoro 490).
Tunapenda kuwahakikishia wote wanaokwepa mafunzo kuwa wataendelea kufuatiliwa na mara watakapopatikana hatua za kuwarejesha katika mafunzo zitachukuliwa.
Changamoto ya tatu ni kutopatikana kwa huduma za mtandao (internet) makambini. Wizara inatambua umuhimu wa mtandao na hivyo juhudi zitafanyika siku za usoni kuyaunganisha makambi kwa kadri mkonga wa Taifa unavyozidi kuenea nchini.
Hata hivyo, kijana anayekuwa mafunzoni kwa miezi mitatu atajikuta hana muda wa kutumia huduma hiyo kutokana na majukumu aliyonayo. Kwa wanaoomba nafasi vyuo vya elimu ya juu upo utaratibu wa kuwaruhusu kutumia huduma zilizo nje ya makambi.
Aidha, JKT linakabiliwa pia na changamoto ya kutoa mafunzo kwa muda mrefu zaidi kutokana na maombi ya vijana wanaomaliza na pia maombi ya waheshimiwa wabunge. Hii ni ishara njema ya kuona umuhimu wa mafunzo yanayotolewa na kwa kadri makambi yatakavyoongezeka nchini suala la muda wa mafunzo pia litaangaliwa.
Changamoto nyingine ni miundombinu michache ikilinganishwa na idadi kubwa ya vijana wanaotarajiwa kumaliza kidado cha sita na vyuo kila mwaka. Suluhisho la jambo hili litapatikana baada ya kupanuliwa kwa makambi ya JKT.
Wizara inaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili kuwa na mpango utakaohakikisha vijana wanaofaulu vizuri wanapata mafunzo mapema na kuwawezesha kujiunga na vyuo vya elimu ya juu kwa wakati. Kwa wale wanaojiunga sasa na ambao tayari wamedahiliwa, Wizara imewasiliana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili kupata orodha yao na hatimaye kuwawekea utaratibu wa kujiunga na mafunzo hayo baada ya kumaliza masomo yao.
Imetolewa na Luteni Kanali Juma Nkangaa Issa Sipe,
Msemaji, Wizara ya Ulinzi na JKT,
Simu: 0756448787/0655878744/0784370500/0772516666.
Barua pepe: jnisipe@modans.go.tz; jnisipe@yahoo.com; jnisipe@gmail.com.
Source: http://www.wavuti.com