Msemaji wa Jeshi la Wananchi Tanzania, Meja Eric Komba akizungumza na 
waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusiana na ushiriki wa 
Tanzania katika Operesheni ya Ulinzi wa Amani katika nchi ya Demokrasia 
ya Kongo (DRC). Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Assa 
Mwambene. Picha na Aika Kimaro 
            
    Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Posted Septemba7 2013 saa 8:54 AM
Posted Septemba7 2013 saa 8:54 AM
Kwa ufupi
Ni kile kilichoenda kushirikiana na vikosi vya nchi za maziwa makuu kwa msaada wa Umoja wa Mataifa.
Dar es Salaam. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa 
Tanzania, (JWTZ) limeeleza kuwa Tanzania haikupeleka kikosi cha jeshi 
hilo kwenye Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri
 ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)(Monusco) kwa ajili ya kupigana na 
Rwanda, bali kusaidia kulinda amani.
Ufafanuzi huo umekuja siku mbili baada ya Rais 
Jakaya Kikwete kukutana na Rais Paul Kagame wa Rwanda, kufuatia baadhi 
vyombo vya habari vikiandika habari jinsi JWTZ kilivyopambana na waasi 
wa Kikosi cha M23 na kukisambaratisha, sambamba na malumbano kati ya 
Tanzania na Rwanda.
Askari wa Tanzania na wale wa Afrika Kusini wako DRC kwa kazi ya kulinda amani. Malawi bado haijapeleka majeshi yake.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, msemaji 
wa JWTZ, Meja Erick Komba alisema,“Kikosi cha Tanzania kilichopo DRC ni 
sehemu ya Kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika 
(SADC), kilichotoa mchango wake katika Jeshi la Umoja wa Mataifa 
(Monusco) na kinafanya kazi chini ya komandi ya Monusco.”
Alifafanua kuwa kazi ya kikosi hicho ni kuzuia 
waasi kujitanua, kuvunja nguvu yao pamoja na kuwapokonya silaha, huku 
akisisitiza kuwa sio kweli kuwa Tanzania ilikuwa ikipigana na Rwanda au 
waasi wa M23, kama ambavyo imekuwa ikielezwa.
“Ridhaa ya kikosi chetu kwenda DRC ilikubaliwa pia
 na Rwanda, nchi ambayo ni mwanachama wa nchi za maziwa makuu. Aidha 
Rwanda imesaidia kuruhusu kikosi cha Tanzania kupitisha watu,vifaa na 
zana nchini kupitia nchi hiyo kwenda DRC,” alisema.
Alisema kuwa vikosi hivyo ambavyo mbali na Waasi 
wa M23 pia vimekuwa vikipambana na vikosi vya Waasi vya ADF na FDLR, 
kwamba bado vinaendelea kulinda amani nchini DRC na kama kunaibuka 
mapambano navyo hulazimika kujibu mapigo.
Kikosi cha Munusco kilianza kupambana na waasi, 
Agosti 27, mwaka huu na askari wa JWTZ, Khatibu Mshindo alikuwa miongoni
 mwa waliouawa kwa kupigwa bomu na M23 Mjini Goma ulioko Mashariki mwa 
DRC. baada ya kuzuka mapigano makali.
source: Mwananchi
source: Mwananchi
 
  