Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Posted Septemba7 2013 saa 11:51 AM
Posted Septemba7 2013 saa 11:51 AM
Kwa ufupi
Munyonyo. Kundi la wapiganaji wa M23 huko
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), limesema kwamba lipo tayari
kukutana na Rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila, kama ilivyokubaliwa kwenye
mkutano wa viongozi wa nchi za maziwa makuu uliofanyika Uganda juzi.
Utayari huo unatokana na agizo lililotolewa baada
ya mkutano wa wakuu hao wa nchi kukubaliana kwamba ni vyema Serikali ya
DRC ikirejea kwenye mazungumzo na M23 kwa ajili ya kumaliza tofauti zao
kwa njia ya amani.
Katika mkutano huo uliofanyika huko Munyonyo,
Uganda, wakuu hao wa nchi walisema kwamba ni vyema mashambulizi dhidi ya
wapiganaji wa M23 yakasitishwa kwa sasa ili kutoa mwanya wa mazungumzo.
Mkutano huo uliitishwa na Rais Yoweri Museveni
ambaye kwa sasa ndiye mwenyekiti wa Mkutano wa Kimataifa wa Nchi za
Maziwa Makuu, ambao ni chombo muhimu katika kuangalia masuala ya amani
na usalama kwa nchi 12 wanachama.
Mwaka jana, Serikali ya DRC na M23 walianza
mazungumzo ya kutafuta amani chini ya Serikali ya Uganda lakini
yalikwama huku M23 wakiituhumu Serikali kwa kukataa kutoa ushirikiano.
Kiongozi wa kundi hilo Bertrand Bisimwa aliliambia
Shirika la Habari la AFP kwamba wapo tayari kufanya mazungumzo hayo ili
kufikia mwafaka.
“Wawakilishi wetu wapo tayari Kampala na
wameshakubaliana kwamba watazungumza kuhusu amani na viongozi hao wawili
wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,” alisema Bisimwa.
Naye msemaji wa DRC, Lambert Mende , alisema
kwamba Serikali imefurahia suala la kukubali kwa viongozi wa Kundi la
M23 kufanya mazungumzo hayo.
Alisema Serikali na M23 wanatakiwa kukubaliana
namna ya kuiweka DRC katika hali ya usalama kwani raia wengi
wameshapoteza maisha mpaka sasa, huku wengine wakiishi bila amani.
M23 waliuvamia mji wa Goma Mashariki mwa DRC
Novemba mwaka jana lakini jeshi la DRC likisaidiwa na kikosi maalumu cha
Umoja wa Mataifa kwa ajili ya DRC, Monusco, ziliweza kuudhibiti mji
huo.
Rwanda imeshutumiwa kwa kuwaunga mkono M23 madai ambayo hata hivyo iliyakanusha vikali.
Viongozi wa M23 walitangaza kusitisha mapigano
wiki iliyopita wakisema wako tayari kushiriki katika kupatikana amani
nchini humo.
Mazungumzo kati ya Serikali na kundi hilo yalisambaratika mwezi
Mei mwaka jana. Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kanda ya
maziwa makuu, Mary Robinson, yuko ziarani katika kanda hiyo.
M23 imetokana na askari Watutsi, ambao walitoka
katika jeshi la nchi hiyo Aprili mwaka jana, ambapo inadaiwa walichukua
silaha nyingi kutoka jeshini kabla ya kujitenga ambazo ndizo wanazitumia
mpaka leo.
Wakati huohuo, Vikosi vya kulinda amani vya Umoja
wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vimeelezea uwezekano
wa kuanzisha mashambulizi mapya dhidi ya M23.
Msemaji wa vikosi vya Umoja wa Mataifa nchini
Kongo Felix Basse alisema kuwa, vikosi hivyo vya Umoja wa Mataifa
vinafanya juhudi za kurejesha usalama katika maeneo yaliyokombolewa
kutoka mikononi mwa wapinzani.
Harakati za makundi ya wapinzani hususan M23 mkoani Kivu Kaskazini, zimezorotesha hali ya usalama wa eneo hilo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo Mawaziri wa Mambo
ya Nje wa eneo la Maziwa Makuu Barani Afrika wametaka kusitishwa
mashambulio dhidi ya M23 , Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kutoa
mwanya kwa mazungumzo ya amani yanayofanyika Kampala, Uganda.
source: Mwnanachi
source: Mwnanachi