Monday, 16 September 2013

KANISA: "ZANZIBAR HAITAKI MUUNGANO...

 


*Lasononeka kuumizwa kwa matakwa ya kisiasa
*Lasema tindikali kwa mapadri ni salamu za kujitenga
*Padri Mwang’amba alazwa Muhimbili, agoma kuongea

KANISA Katoliki Jimbo la Zanzibar, limesema matukio ya kigaidi yanayotekelezwa dhidi ya mapadri wa kanisa hilo, yana mkono wa kisiasa wenye lengo la kushinikiza visiwa hivyo kujiondoa katika Serikali ya Muungano.

Limesema upo ushahidi usiotiliwa shaka unaoonyesha kuwa, Wazanzibari wengi wanataka Muungano utoweke na visiwa hivyo viwe na Serikali yake kamili.
 
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Jimbo la Zanzibar, Padri Arbogast Mushi, katika mahojiano yake na MTANZANIA Jumapili, yaliyofanyika katika viunga vya Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako Padri Anselmo Mwang’amba, amelazwa akipatiwa matibabu baada ya kumwagiwa tindikali juzi na watu wasiojulikana.

Padre Mushi alisema sauti za wananchi wa Zanzibar zinasikika zikiupinga Muungano na matukio ya kinyama yanayofanywa sasa yakiwalenga viongozi wa dini na watu wengine, yanalenga kushinikiza visiwa hivyo kuachwa huru.

Alisema, jamii kubwa ya watu wa Zanzibar ni waumini wa dini ya Kiislamu, hivyo ni kundi dogo la watu ambalo limeamua kushinikiza sauti za Wazanzibari zisikilizwe kwa kutumia njia hizo chafu, kulazimisha mamlaka kuchukua hatua na pia kuwatisha watu wasio waumini wa dini hiyo kuamini kuwa siyo salama kuishi katika visiwa hivyo kwa mtu ambaye siyo Muislamu.

“Kila unapokwenda unasikia wanataka Muungano utoweke, wanataka nchi yao, mtu anaweza kufanya kwa faida binafsi ili kuonekana kuwa ni Waislamu, hiki ni kikundi cha wachache wakorofi wanaotaka Zanzibar isitawalike,” alisema Padri Mushi.

Padri huyo alisema ingawa hapendi kulihusisha tukio lililompata Padri Mwang’amba na masuala ya dini, lakini zipo hisia za kuwepo kwa kikundi cha watu wachache ambao wanataka Zanzibar isitawalike.

Alisema viongozi wa Kanisa Katoliki wa ngazi za juu, wanatarajiwa kukutana hivi karibuni kujadili mwenendo huo wa mambo na kwamba watatoa tamko rasmi baada ya mkutano wao huo.

Wakati Padri Mushi akieleza hayo, Padri Thomas Assenga wa Parokia ya Mtakatifu Joseph ya Zanzibar, ambaye alisafiri na majeruhi kutoka Zanzibar kuja Hospitali ya Taifa Muhimbili, ameliambia MTANZANIA Jumapili kuwa miezi miwili iliyopita, Padri Mwang’amba alitishiwa na watu wasiojulikana wakati akitoka kutoa huduma kwenye kituo cha wazee, kinachofahamika kwa jina la Welezo.

“Kila siku alikuwa anakwenda kufanya huduma kituo cha wazee. Mwezi wa saba mwaka huu wakati akielekea huko, alikutana na watu wakifanya mazoezi. Ni desturi ya Wazanzibari kufanya mazoezi sehemu yenye kilima na barabarani, sasa alipowakuta wakiendelea na mazoezi barabarani alipiga honi ili apishwe lakini kitendo hicho kiliwakera, mmoja akamwambia watamuonyesha,” alisema Padri Assenga.

Akieleza mwenendo wa kila siku wa Padri Mwang’amba, alisema padri huyo ambaye pia ni msaidizi wa Paroko wa Parokia ya Roho Mtakatifu Cheju, ingawa mara nyingi siku za Jumapili hutoa huduma katika Parokia ya Mpendae, pia hutoa huduma katika kituo cha wazee cha Welezo katika siku za wiki.

Padri Mwang’amba alifikishwa katika Hospitali ya Muhimbili kitengo cha dharura majira ya saa 5 asubuhi akitokea Zanzibar ambako alikuwa akipatiwa huduma katika Hospitali ya Mnazi Mmoja visiwani humo.

Baada ya kufikishwa Muhimbili jana, Padri Mwang’amba alifanyiwa uchunguzi wa mwili mzima kwa zaidi ya masaa matatu, kabla ya kupelekwa katika wodi namba kumi jengo la Kibasila ambako amelazwa kwa ajili ya matibabu zaidi. Agoma kuzungumza na kupigwa picha
Padri Mwang’amba ambaye alifikiwa na gazeti hili kitandani alipolazwa katika wodi ya Kibasila, aligoma kuzungumzia hali yake sambamba na tukio lililomkumba.

Hata hivyo, baada ya wauguzi watatu wanaomuangalia kwa karibu kumsihi azungumze na waandishi wa habari, alisema: “Asanteni kwa ukarimu wa kuniona, naendelea na matibabu kama mnavyoona,” kisha alinyamaza na kujifunika shuka hadi usoni.

Muuguzi wa zamu wa Wodi ya Kibasila, Ruthguard Rutabingwa, ambaye alithibitisha kupokelewa kwa Padri Mwang’amba, alisema hali yake inaridhisha.

Padri Mwang’amba alimwagiwa tindikali juzi majira ya saa 10 jioni maeneo ya Mlandege ambako alikwenda kupata huduma ya kutoa ‘Photocopy’.

Akiwa ndani ya chumba cha huduma hiyo, alipigiwa simu na kutoka nje kwa nia ya kuzungumza, ndipo ghafla alitokea mtu mmoja akiwa ameshika kopo linaloaminika kuwa na tindikali aliyommwagia usoni na kusambaa mpaka kifuani na mikononi, kisha akatokomea kusikojulikana.

Tukio la sasa ni mwendelezo wa matukio ya aina hiyo ambayo yameendelea kushamiri kwa kasi kubwa visiwani humo.

Mbali na Padri huyo, mwaka jana Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga alimwagiwa tindikali, pia Mei mwaka huu Sheha wa Shehia ya Toronto, Wilaya ya Magharibi Unguja, Mohamed Omar Said alipatwa na mkasa huo.

Mbali na hao, takribani mwezi mmoja uliopita raia wawili wa Uingereza, Kate Gee (18) na Kirstie Trup (18), Agosti mwaka huu, nao walimwagiwa tindikali katika maeneo ya Mji Mkongwe, Zanzibar, tukio ambalo kwa kiasi kikubwa lilitia doa visiwa hivyo kimataifa.


Source: MTANZANIA