Monday, 16 September 2013

TANZANIA YATUHUMIWA KUWABAKA RAIA WA MALAWI,KURUGENZI YA HABARI YAKANUSHA

Msemaji wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene akitoa ufanunuzi kwa waandishi wa habari jana mjini Dar es salaam juu ya taarifa zilizochapishwa na gazeti la Malawi News kuwa Wamalawi waishio nchini Tanzania wanaogopa kutoka nje kutokana na ubaguzi wanaofanyiwa na Watanzania taarifa ambazo sio kweli.
Msemaji wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene akiwaonyesha waandishi wa habari jana mjini Dar es salaam kichwa cha habari cha gazeti la “Malawi News” kinachosemeka “MALAWIANS FACE XENOPHOBIA IN TZ” ambacho kilichapishwa na gazeti hilo kuhusu madai ya kubaguliwa raia hao wa kutoka Malawi jambo ambalo sio kweli.

Na Benedict Liwenga-MAELEZO_Dar es salaam

SERIKALI ya Tanzania imekanusha taarifa zilizochapishwa na gazeti la nchini Malawi lijulikanalo kama “Malawi News” kuwa Wamalawi waishio nchini Tanzania wamekuwa wakiogopa kutoka nje kutokana na ubaguzi wanaofanyiwa na Watanzania.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Assah Mwambene amesema kuwa taarifa hizo ni za kupotosha umma na kuleta chuki dhidi ya Tanzania na nchi jirani na hazina ukweli wowote ule.

Bw. Mwambene ameongeza kuwa hakuna raia yeyote wa kutoka Malawi aliyebakwa wala kunyanyaswa kwa namna moja ama nyingine.

“Hakuna mwananchi yoyote kutoka Malawi aliyebakwa , wala hakuna raia yoyote wa Malawi aliyepo hapa nchini anayeogopa kutoka nje kwa sababu ya ubaguzi wowote ” amesisitiza Mkurugenzi huyo.

Amesema kuwa licha Tanzania kuwakamata wahamiaji haramu 1030 kutoka Malawi, Serikali ya Tanzania iliwapa fomu ili kama walikuwa wanahitaji kuishi nchini wahalalishe uwepo wao hapa Tanzania kwa wale wote walionyesha nia ya kuendelea kuwepo hapa nchini .

Aidha wahamiaji wote haramu 1030 kutoka Malawi waliachiwa huru na wanaendelea kukamilisha taratibu za kuhalalisha uwepo nchini.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa mpaka sasa kati wahamiaji haramu 1030 hakuna aliyewekwa ndani ama kushikiliwa na vyombo vya dola kwa kosa la kuwepo kinyume.

Kufuatia taarifa hizo ,Mkurugenzi huyo amelitaka gazeti hilo kusahihisha taarifa hiyo na kuiomba radhi Tanzania kwa upotoshaji huo na kuongeza kuwa kauli hiyo ni sawa na matusi kwa Tanzania.

Aidha amesema kuwa hadi hivi sasa zaidi ya wahamiaji haramu 24,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokarisia ya Kongo (DRC) , Rwanda, Burundi , Uganda na Zambia wamerejeshwa makwao kwa kosa la kuishi Tanzania bila vibali.
 
SOURCE: KILELE CHA HABARI- TANZANIA