Jana ulimwengu uliadhimisha ‘Siku ya Kuzuia Kujiua Duniani’, ambayo kimsingi iko chini ya usimamizi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), yenye ofisi pia hapa nchini.
Kwa kawaida siku hii iliyoanza mwaka 2003, tangu wakati huo imekuwa ikiendelea kuadhimishwa kila ifikapo Septemba 10, lengo kubwa ni kuamsha hisia za umma juu ya tatizo hilo la watu kujiua ambalo linaendelea kuonekana kubwa nchini na Duniani kwa ujumla.
Makadirio ya shirika hilo la afya, yanaonyesha kuwa watu 1000,000 ulimwenguni hujiua kila mwaka, sawa na watu 3,000 wanaojiua kila siku, sawa pia na mtu mmoja anayejiua katika kila baada ya sekunde 40. Walio na umri kati ya miaka 15 na 25 ndio wanaoongoza kwa visa vya kujiua.
Kadhalika ripoti inaeleza takwimu za watu wanaojaribu kujiua ukilinganisha na miaka mitano iliyopita kwamba zimezidi hadi kuwa kati ya mara 10 hadi 20.
Hali ngumu za kiuchumi, kusambaratika kwa familia, unywaji wa pombe, dawa za kulevya ni baadhi ya masuala ambayo huchochea watu kujiua, huku masuala yanayohusiana na mapenzi (kina pendapenda) yakielezwa kuwa ndiyo kinara hasa kwa vijana.
Hali ya kujiua nchini
Kulingana na taarifa za Wizara ya Mambo ya Ndani Tanzania, watu wanaojiua wanaongezeka. Kwa mfano inasema katika miaka mitano mfululizo watu zaidi ya 3,420 walijiua, huku kasi ya hao wanaojiua ikionekana kuongeza kwa zaidi ya asilimia kati ya sita na 10, huku wanaume ndiyo wakielezwa kuongoza kujiua, kwa asilimia 70.
Hali kadhalika watoto 59 wenye umri chini ya miaka 18 walijiua. Kwa jumla wastani wa watu 684 wamekuwa wakijiua au kuthubutu kutaka kujiua kwa mwaka.
Kulingana na taarifa za Jeshi la Polisi, watu walio na umri wa miaka 15 na 25, ndio wanaoongoza, sababu kubwa ni matatizo ya kimapenzi na mengine ya kijamii na kifamilia.
Wengine ambao nao hujiua ni wafanyakazi wastaafu kutoka ofisi za Serikali na watu binafsi na sababu kuu ni hali ngumu ya uchumi.
Sababu nyingine ni kuambukizwa magonjwa mbalimbali yakiwamo yale yasiyo na tiba hasa Ukimwi. Wengi wanaojiua huamini hilo ni jambo zuri kwao kuwaondolea hali ya sononeko moyoni ambayo imekuwa ikiwasumbua, kitu ambacho siyo kweli.
Prof. Gad Kilonzo wa Chuo kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (Muhas) anaeleza dalili za mtu anayeweza kuonyesha ishara mbaya ya kuweza kujiua kuwa ni kuonyesha kukata tamaa au kuonyesha mabadiliko makubwa ya tabia hasa za kutaka kujitenga na watu wengine akiwa mwenye sononeko au kutopata majibu ya shida inayomkabili.
Ajiua kwa mke kukataa mali zisiuzwe
Mtu anayedaiwa ni raia wa Rwanda, France Mathias(75) amejinyonga Wilayani Kyerwa baada ya mke wake ambaye ni Mtanzania kupinga wazo la marehemu la kutaka wauze mali zote na kuondoka huku operesheni ya kuwasaka wahamiaji haramu ikiwa imeshika kasi.
Kabla ya kujinyonga katika tukio la juzi asubuhi katika kijiji cha Kikukulu, marehemu alichanachana kiasi cha fedha za Kitanzania kinachokadiriwa kufikia shilingi milioni saba zilizotokana na mauzo ya kahawa.
Binti wa marehemu, Merania France anasema tangu kuanza kwa operesheni ya kuwasaka wahamiaji haramu, wazazi wake waliingia katika mzozo mkubwa. Baba alitaka wauze mali zote na kuondoka nchini.
Anasema mama yake ambaye ni mwenyeji wa Wilaya ya Ngara alikataa mpango wa marehemu. Siku moja kabla ya tukio la kujinyonga mama huyo alitoroka usiku akiwa na watoto watano na hawajulikani walipo, ndipo mwanamume akaamua kujiua.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kikukulu, Joseph Leo anasema marehemu alikuwa kwenye orodha ya wahamiaji haramu, lakini hakuwa na taarifa ya kuzuka kwa ugomvi kwa wanandoa hao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Philip Kalangi anasema atawauliza wasaidizi wake kwani wakati huo alikuwa kwenye operesheni ya kuwaondoa wahamiaji haramu.
Sababu nyingine za kujiua na tiba yake
Wanasaikolojia mbalimbali wanasema msingi wa watu kufikiria kujiua ni kushindwa kupata majibu kwa shida zinazowasonga mbele. “Baadhi watu huamua kujiua si kwa sababu wanapenda kufa, sababu kubwa ni kutotaka kuyashuhudia matukio yanayowakumba katika maisha yao. Wengi waliokutwa wamejiua wamekuwa wakiacha ujumbe au barua zikieleza maneno kama ” Heri nife kuliko kuyaona haya”, ”hii ni aibu sitaweza kuvumilia”, ”kwa nini haya yanipate mimi” anasema Modester Kimonga, mwanasaikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma.
Anasema uchungu ndani ya moyo ndiyo unaomsukuma mtu kuamua kujiua, uchungu huu unasababishwa na matukio mengi sana ambayo huvunja moyo, husababisha mtu kupata sononeko moyoni mwake. Baadhi ya sababu ni kama ndoa kuyumba, uchumi kuporomoka, kustaafu, kutengwa na jamii na kunyanyaswa. “Kuna aina nne za vifo vya kujiua:(i)Egoistic suicide, hutokana na hali ambayo mtu anakosa ushirikiano kutoka kwenye jamii yake, yaani wale wanaomzunguka. Hii humsababishia kuona maisha hayana maana kwake hivyo anaona ni bora afe na huamua kujiua. Huwapata watu wengi ambao hawana wenza, hasa wanaume
(ii) “Ni kinyume cha egoistc, yaani hutokea katika jamii ambayo watu wanashirikiana sana, hivyo matakwa ya jamii hupewa kipaumbele kuliko matakwa ya mtu binafsi, hivyo kusababisha mtu kujiona anapuuzwa.
(iii) Anomic suicide, ni ile hali ambayo hutokana na uchumi kuyumba, (iv) Fatalistic suicide yaani ni ile hayi ya mtu kuamua kujiua kwa sababu anaishi kwenye maeneo yenye manyanyaso. Mtu huamua kufa kuliko kuishi katika hali ya kunyanyaswa.
Hii hutokea hasa magerezani au katika baadhi ya nyumba ambazo kuna unyanyasaji,” anafafanua mtaalamu huyo katika mahojiano na mwandishi wa makala haya na kusisitiza umuhimu wa watu kufikiria zaidi namna ya kupata majibu kwa matatizo yao, badala ya kuwaza kujiua.
source: Mwananchi
source: MWANANCHI