Wednesday, 11 September 2013

Tanzania ya sasa ni Madawa ya kulevya na Umwagwaji wa tindikali: Mfanyabiashara amwagiwa tindikali Dar

 
Na Elias Msuya

Posted Jumanne,Septemba10 2013 saa 21:50 PM
Kwa ufupi
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mburahati, Dickson Tungaraza amekanusha kuwepo kwa mgogoro huo“Mimi ninachojua hakuna mgogoro… wewe uko wapi? njoo ofisini ndiyo utajua yote,”

Dar es Salaam. Matukio ya wananchi kumwagiwa tindikali yameendelea kushika kasi nchini baada ya Mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi, Christian Msema wa Mburahati Dar es Salaam, kumwagiwa kemikali hiyo mwishoni mwa wiki na watu wasiojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilus Wambura alisema hana taarifa hizo licha ya tukio hilo kutokea mbele ya Kituo cha Polisi Mburahati.
“Kwa sasa sina hizo taarifa, labda mpaka niulize,” alisema Kamanda Wambura.
Msema maarufu kama ‘Mnyalu’ amelihusisha tukio hilo lilitokea jioni ya Jumamosi Septemba 8 na mgogoro wa eneo la wazi ambapo yeye alikuwa akipinga mfanyabiashara mmoja (jina linahifadhiwa) kulitumia kuegesha magari yake.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mburahati, Dickson Tungaraza amekanusha kuwepo kwa mgogoro huo“Mimi ninachojua hakuna mgogoro… wewe uko wapi? njoo ofisini ndiyo utajua yote,” alisema.
Akizungumza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikolazwa, alisema baada ya kufunga duka lake, watu waliokuwa kwenye pikipiki ya matairi matatu (Bajaj) walimwagia kemikali hiyo na kutoweka.
“Ilikuwa saa mbili usiku baada ya kufunga duka langu nikawa naelekea nyumbani, mara ikaja Bajaj ikasimama mbele yangu. Mmoja wa abiria akaniuliza, vipi bosi, ndiyo unakwenda kuangalia kiwanja chako? Nilipomwangalia ndiyo wakanimwagia tindikali,” alisema Msema na kuongeza:
“Nilipiga mayowe wezi hao wezi hao! Lakini walikimbia bila kukamatwa. Walikuja watu wakanimwagia maji na maziwa na kuniwahisha hospitali.”

source: Mwananchi