Na Sharon Sauwa
Posted Alhamisi,Septemba5 2013 saa 21:8 PM
Posted Alhamisi,Septemba5 2013 saa 21:8 PM
Kwa ufupi
- Akijibu swali hilo, Pinda alisema: “Hivi kweli Mbowe una ngoja hadi muswada unafika ngazi ya Bunge, ndipo unakuja na hoja hiyo wakati tulikuwa na fursa kubwa?”
Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema
Serikali haitauondoa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba kwa sababu mambo ambayo Kambi ya Upinzani Bungeni inayadai,
yanazungumzika na yanaweza kubadilishwa kwa mamlaka ya wabunge.
Pinda alikuwa akijibu swali la nyongeza la
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe katika
kipindi cha Maswali ya Kwa Waziri Mkuu Bungeni, Dodoma jana.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema),
alisema yapo matukio ya kibabe, kejeli, matusi na ya dharau ambayo
yamekuwa yakifanya kuchelewa kwa utaratibu mzima wa utungaji wa
sheria... “Pamoja na rai mliyoiondoa, sisi tunasema yapo maeneo mengi
yasiyo na tija ambayo yanafanya msingi wa marekebisho ya sheria mlioleta
jana (juzi), kuwa hayana tija kwa mchakato huu.”
Akijibu swali hilo, Pinda alisema: “Hivi kweli
Mbowe una ngoja hadi muswada unafika ngazi ya Bunge, ndipo unakuja na
hoja hiyo wakati tulikuwa na fursa kubwa?”
Alisema kwa mambo ambayo alielezwa kuwa ndiyo
yaliyosababisha wabunge wa kambi ya upinzani kutoka nje ya Ukumbi wa
Bunge juzi, hakuna atakayeona umuhimu wa kuondoa muswada huo.
“Kwa sababu ni vitu ambavyo ndani ya Bunge hili
vinazungumzika na vinaweza kubadilishwa kulingana na mamlaka mliyopewa,”
alisema.
Katika swali la msingi, Mbowe alisema mchakato wa
Katiba Mpya unahitaji ustahimilivu, ushirikiano, uwazi, dhamira njema na
kwamba wabunge wanapaswa kutambua kuwa wapo wadau nje ya Bunge
wanahitaji ushirikiano.
Pinda alisema: “Mategemeo ni wabunge tulio ndani
tutaujadili muswada huu kikamilifu na maeneo yote ambayo yanadhaniwa
yanaweza yasiwe na tija, neema kwa nchi yetu, ni jukumu letu kujadili
kwa uwazi, uaminifu na kiukweli.
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR –Mageuzi),
alihoji kama Serikali haioni ni busara mazungumzo ya kisiasa kufanyika
kwanza kisha yakafuatiwa na sheria ambayo itasaidia kuunda dhana ya
dola. Alisema kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa Katiba kwa kuruhusu
mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar.
Kuhusu hilo, Pinda alisema kulikuwa na mashauriano
makubwa kati ya vyama, taasisi na pande mbili za Muungano kabla muswada
huo kufikishwa bungeni na kwamba Katiba Mpya itameza yote yaliyomo
katika katiba hiyo ya zamani na kuja na mawazo mapya ambayo itaongoza
Taifa.
source: Mwananchi
source: Mwananchi