Saturday, 2 November 2013

Nyumba ndogo zatesa vigogo, wenye nazo

 
Na Raymond Kaminyoge, Mwananchi

Posted  Alhamisi,Oktoba31  2013  saa 12:51 PM
Kwa ufupi
Siku ya kuoana na hata kabla, kuna ahadi ambazo watu hao hupeana;hasa zinahusiana na kuheshimiana na kufanya mambo yenye lengo la kuonyesha upendo wa dhati na kuimarisha ndoa yao na familia kwa ujumla.

Japo wengine wanaweza kuwa na maana tofauti, ndoa inafahamika kuwa ni muungano baina ya watu wa jinsi tofauti yaani mwanaume na mwanamke.Kwa Wakristo ndoa inapaswa kuwa ya mke mmoja na mume mmoja, wakati kwa Waislamu, mume anaruhusiwa kuoa zaidi ya mke mmoja.
Siku ya kuoana na hata kabla, kuna ahadi ambazo watu hao hupeana;hasa zinahusiana na kuheshimiana na kufanya mambo yenye lengo la kuonyesha upendo wa dhati na kuimarisha ndoa yao na familia kwa ujumla.
Hata hivyo hapa nchini kama ilivyo katika nchi mbalimbali za nje, kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya wanandoa kutoheshimu viapo walivyopeana siku wanafunga ndoa.
Baadhi ya wasomi maarufu katika masuala ya ndoa, Kertzer, David I na Marzio Barbagli (2001) wanasema katika utafiti wao walioupa jina la the history of the European family yaani historia ya familia Ulaya, uliochapishwa na Chuo Kikuu Yale, Marekani kuwa ndoa njema ni ile ambayo watu wake wanajali kwa vitendo ahadi walizopeana za kuishi vizuri. Kwa bahati mbaya kuna watu wanaingia kwenye ndoa wakiwa wanaelewa vizuri, baada ya kuanza kuwa umaarufu au kuwa na fedha, ndoa zao hugeuka na kuanza kuwa mbaya.
Badala ya fedha kuwa sehemu ya kusaidia maisha yaweze kuwa bora,zinaonekana kuchangia kuwa na ndoa zilizokithiri migogoro.
Wengi huanza kurudi usiku wa manani au hata kulala nje kwa visingizio vya wingi wa kazi au hata safari feki za kazi.
Watafiti Evans, Tanya (2005) katika chapisho walilolipa jina la Women, Marriage and the Family yaani wanawake ndoa na familia wanasema kutoheshimu ndoa kunasababisha baadhi ya watu kushindwa kuwa na maisha bora kwa sababu ya kutumia fedha nyingi bila sababu za maana.
“Wengine nje ya ndoa wana zaidi ya wanaume au wanawake mmoja, hii yote ni kuonyesha namna gani si bora, kwani walio bora hujua namna ya kuvifanya hata visivyo vizuri view vizuri” inasema sehemu ya utafiti wa wasomi hao ikizingumzia tabia za baadhi ya watu wa kada mbalimbali.
Hivi karibuni, Rais Robert Mugabe aliwaonya mawaziri wake dhidi ya `nyumba ndogo’ akisema baadhi ya mawaziri wanatumia mali zao nyingi kuwa katika uhusiano wa kimapenzi wa wanawake wasio wake zao.
Kuna viongozi wameoa wake wengine na kuachana na wale wa awali bila sababu za maana, huku watoto wao wakiwa na maisha duni. Kinachoonekana ni kama wake wengi wa viongozi na watu wenye fedha, wanaishi kwenye ndoa kwa kuvumilia, siyo kwa furaha; wengi kwa nje wanaonekana wana furaha, ndani ni shida.
Wengine hawajawahi kupanda gari pamoja na waume zao kwenda kwenye matembezi, na hata wanapotaka ukaribu huambiwa kwani shida ni nini kama kula si unakula…watu hawaingii kwenye ndoa kufuata kula, bali uhusiano mzuri wenye amani, wanasema watafiti Berstein na Nina (2007) katika utafiti wao walioupa jina la “Polygamy, Practiced in Secrecy” yaani katika maana isiyo rasmi ndoa za wake wengi zinavyoendesha kwa kificho.
 
Maoni ya watafiti 

Watafiti hawa wanasema wengi wanasema wameoa mke mmoja, ingawa katika uhalisia wana zaidi, kwa kuwa wengine huko nje hutoa huduma zote kama mke. Wengine ambao pia ndoa zao zinawaka moto ni viongozi wa dini, ni mojawapo ya dalili za kujua hilo ni kuangalia kama ni watu wanaoweza kutembea pamoja au la.
Mara nyingi ukiona wanandoa hawatembei pamoja hasa nyakati za mwisho wa wiki au sikukuu, kama hakuna sababu labda za ugonjwa, mwingiliano wa kazi au zinazofanana na hizo, yaweza kuwa ni ishara kuwa ndoa yao ni mbaya, tayari mmoja ana mwingine nje, hivyo hajali tena kuwa karibu na mwenza wake wa ndoa.
Kauli ya Mugabe huenda ikawa ni muhimu kujadiliwa na jamii zote duniani kutokana na ukweli kuwa kumekuwa na hisia zinazofanana na Mugabe katika nchi nyingi.
Mugabe alitoa kauli hiyo kwenye harusi ya mpwa wake.Huku akiwasihi wanandoa kuwa waaminifu katika ndoa zao, Mugabe alionya dhidi ya kile alichokitaja kama tabia ya wanaume kuwa na `nyumba ndogo’ akisema kuwa mawaziri wake aliowatarajia kuwa watu wenye maadili mema, pia walikuwa na tabia ya uasherati.
Kwa mujibu wa jarida la New Zimbabwe, Mugabe anasema kuwa, “mali ambayo baadhi ya mawaziri wanayo ndiyo chanzo cha matatizo kwenye ndoa.
Anasema nyumba ndogo siyo jambo jema na anasisitiza kuwa anajua kuwa mawaziri wake wote wana tabia ya uasherati ambalo siyo jambo jema katika jamii.
“Nawasihi muachane na tabia hiyo. Mwammume mmoja na mke mmoja bila shaka itafanikisha ndoa zenu,” anasema Mugabe akimaanisha watu kuheshimu ndoa zao.
Hoja ya Mugabe
Rais huyo anasema “Wanawake lazima wapigane dhidi ya tabia hii”.
Anasisitiza kuwa usawa wa kijinsi haupaswi kumaanisha kutupilia mbali tamaduni na maadili. Mugabe anasema tabia hiyo ya ngono ndiyo inayochangia kuenea kwa ugonjwa wa Ukimwi kwani anawafahamu mawaziri wengi wanaougua ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, neno ndoa ni makubaliano rasmi ya mwanamke na mwanamume ya kuishi pamoja kama mke na mume. Ingawa neno `nyumba ndogo’ bado halijawekwa rasmi kwenye Kamusi za Kiswahili lakini likitumiwa linaeleweka vizuri katika jamii.
Linaeleweka vizuri kwa sababu suala la mwanamume kuwa na nyumba ndogo ni la kawaida sana hapa nchini ndiyo maana hata msamiati huo unaeleweka vizuri.
Dini zote zinakataza watu kuwa mahusiano ya kimapenzi bila ya kuwa na ndoa. Kwa Wakristo kuna amri ya sita ambayo inakataza kuzini wakati Waislam dini hiyo inakataza hata kuikaribia zinaa.
Kwa hiyo mwanamume anapokuwa na nyumba ndogo ni dhahiri kuwa anavunja amri ya sita kwa kuzini ama kufanya zinaa.
Ingawa Mugabe ameweka wazi kwamba katika nchi yake kuna mawaziri wenye nyumba ndogo kwa maana ya kwamba wanaozini ni lazima tujiulize hali ikoje hapa nchini Tanzania? Kiongozi anapokosa uaminifu kwenye ndoa itakuwa vigumu kuwa muaminifu kwenye taasisi anayoiongoza. Viongozi ndiyo wanatakiwa kuwa waaminifu katika jamii ili wananchi waweze kuiga matendo mema unayoyafanya, wanasema watafiti Berdahl, J. L., & Anderson, C. (2005) katika utafiti wao walioupa jina la Men, women, and leadership yaani wanaume, wanawake na uongozi.
Wasomi hao wanasema ingawa viongozi wa dini wamekuwa mstari wa mbele kukemea watu wasijihusishe na nyumba ndogo kwa sababu huathiri ndoa zao, watu wanajiita kwa majina ya dini mbalimbali wamekuwa hawajali mafundisho ya dini zao.
Katibu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wa zamani, Blandina Nyoni aliwahi kusema watu wengi wamekuwa si waaminifu katika ndoa zao na kwamba hilo ndilo tatizo la kuendelea kuenea kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Wanakufa kwa Ukimwi ndani ya ndoa
Katika utafiti uliofanywa mwaka 2007 hadi 2008 na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa Kupambana na Ukimwi (NACP), unaonyesha asilimia 6.6 ya wanawake walio katika ndoa wameathiriwa na virusi vya Ukimwi wakati wanaume ni asilimia 4.6.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT, Amin Sandewa ambaye anaishi na virusi vya Ukimwi, aliwahi kusema kwamba baadhi viongozi wa Serikali na wale wa kidini walio katika ndoa wanashiriki vitendo vya uasherati.
Mchungaji Sandewa anasema viongozi unawakuta wanakemea vitendo vya uasherati wakati wenyewe wanashiriki vitendo hivyo, tena baadhi ya viongozi hao wenye ndoa chafu ni wale ambao ukiambiwa huwezi kuamini kwa namna walivyo na hadhi katika jamii. “Viongozi wenye ndoa ni lazima tubadilike, nyumba ndogo hazitatusaidi, zaidi ya kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi na kuwa katika hali mbaya kiuchumi, maana kuwa na nyumba ndogo ni gharama,” alisema Sandewa.
Kama wewe uko kwenye ndoa, pata muda wa kujitathimini…je, hali ya ndoa yako ikoje? Je, unafanya mambo ambayo ungependa mwenza wako akufanyie? Jibu unalo. Wapo wengine wamekataa hata kuwasomesha watoto wao kwa sababu wamegombana na wake zao, watoto wana kosa gani? Inaendelea Kesho

SOURCE: MWANANCHI