Monday, 16 September 2013

NI MAFANIKIO. Kutoka shambani hadi mjumbe Tume ya Katiba Mpya


Kibibi Mihogo akitoa maelekezo kwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Halmashauri wakati wa ukusanyaji wa maoni ya Rasimu ya Katiba Mpya mkoani Tanga. Picha na Excuper Kachenje 
Na Exuper Kachenje

Posted  Jumapili,Septemba15  2013  saa 13:25 PM
Kwa ufupi
  • Hata hivyo anasema: “Moyo wangu ulichoka, nilipenda mazao ya mizizi, nilipenda kukutana na wakulima, sikupenda kazi ya maabara; …sikufanikiwa. Nilitaka kwenda katika siasa, nikaacha baada ya kuona aina ya ubaguzi hasa kwa watu wapya kwenye siasa, nikakata tamaa.”


Ukipita katika mitaa mbalimbali ya Mji wa Unguja, Kibibi Mihogo ni miongoni mwa majina maarufu.
Umaarufu wa jina hilo umetokana na mchango wake katika kufanikisha mambo mbalimbali kwenye jamii hasa kwa wanawake wa Zanzibar, akielemea zaidi katika masuala ya kilimo, utafiti na harakati za kupunguza umaskini.
Kibibi Mihogo ambaye jina lake halisi ni Kibibi Mwinyi Hassan ni mzaliwa wa Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini, Unguja katika Visiwa vya Zanzibar.
Ni mtoto wa kwanza kati ya wanne kwa baba mmoja na mama mmoja, akiwa na ndugu wengine wa baba mmoja mzee Mwinyi Hassan.
Mwanamke huyu ambaye pia ana watoto wanne akiwa pia ni mjane baada ya mumewe kufariki dunia, Juni mwaka jana, alianza safari yake ya elimu katika shule ya msingi iliyopo kati ya Kijiji cha Bwejuu na Paje.
Baadaye alijiunga na Sekondari ya Machipi iliyopo Ifakara, wilayani Kilombero, Morogoro, ambapo alisoma mchepuo wa kilimo na kuhitimu mwaka 1979.
Katika mahojiano na mwandishi wa makala haya, wilayani Kilindi mkoani Tanga, alipokuwa kikazi na Tume ya Mabadiliko ya Katiba anayoifanyia kazi sasa, Kibibi aliye na Shahada ya Uzamili ya Rasilimali Watu, anaeleza kuwa baada ya kumaliza kidato cha nne alijiunga na Chuo cha Kilimo Ilonga, wilayani Kilosa, pia mkoani Morogoro kabla ya kuajiriwa na Wizara ya Kilimo Zanzibar katika Idara ya Elimu kwa Wakulima.
“Kati ya mwaka 1982 hadi 1985 nilifanya kazi ya vipindi vya kilimo katika Televisheni ya Zanzibar (TVZ) na vipindi vya redio, Sauti ya Tanzania Zanzibar. Pia nilikuwa nikitoa ushauri kwa wakulima. Mwaka 1986 nikaenda kusomea Diploma ya Kilimo na Uzalishaji Mazao, nikahitimu mwaka 1988,” anaeleza Kibibi.
Anasema kuwa baada ya hapo alipangiwa kazi katika Kituo cha Utafitijeni wa Mazao ya Mizizi maarufu Kizimbani mjini Zanzibar na kuwa Ofisa Utafiti wa zao la muhogo na nazi.
“Utafiti ulinifundisha mengi, nilisafiri nchi nyingi, ulinifanya nijulikane Unguja yote. Nilikutana na wakulima, pia kuwafundsha uandaaji na uzalishaji mazao bora ya mizizi hasa mihogo, niliojifunza Nigeria. Niliweza kutambua aina ya mihogo na magonjwa ya mimea kwa kutazama majani yake tu na hapo ndipo nikapewa jina la Kibibi Mihogo. Najivunia utaalamu na kujulikana ,” anasimulia.
Kibibi anamtaja Rais Mstaafu wa Zanzibar Dk Salmin Amour Juma kuwa alimwezesha kupata shahada baada ya kuwatangazia Wazanzibari nafasi za udhamini wa masomo nchini Mauritius mwaka 1998, ambapo miaka mitatu baadaye alihitimu na aliporejea Zanzibar alikuwa mkuu wa Maabara ya Kuzalisha Mbegu katika Kituo cha Utafiti Kizimbani.
Hata hivyo anasema: “Moyo wangu ulichoka, nilipenda mazao ya mizizi, nilipenda kukutana na wakulima, sikupenda kazi ya maabara; …sikufanikiwa. Nilitaka kwenda katika siasa, nikaacha baada ya kuona aina ya ubaguzi hasa kwa watu wapya kwenye siasa, nikakata tamaa.”