Monday 16 September 2013

Utoke vipi wakati wa usiku?


Posted  Jumapili,Septemba15  2013  
Kwa ufupi
  • Wanawake wengi wamekuwa wakiamini kuwa nguo ya kubana ndiyo inayompendeza mtu, lakini ukweli ni kwamba nguo inayokupendeza ni ile inayokuweka huru. Haijalishi imebana sana ama fupi sana.


Mitindo ni pamoja na kujiamini, unapovaa nguo ya kutokea hasa wakati wa usiku, unatakiwa kuonyesha jinsi gani vazi lako lina thamani. Vilevile onyesha kiasi gani uko huru na vazi hilo. Kwa mujibu wa wataalamu wa mambo ya mitindo, sifa ya vazi la usiku ni kuzungumza.
Vazi lako linatakiwa kutoa taswira halisi uliyonayo mvaaji. Lijieleze lenyewe kwamba; “Niko kwenye ‘good time’, siogopi lolote, mimi ni mkali” Lionyeshe unavyojiamini mbele ya watu.
Nguo ya kutokea usiku ni vazi la kipekee na maalumu. Watu wengi hujaribu kuonekana tofauti wanapokuwa katika mavazi haya, kwa kufanya kila kitu wanachotumia kuwa maalumu, kuanzia vipodozi hadi mapambo mengine.
Licha ya juhudi kadha za kutengeneza mwonekano mzuri, lakini mara nyingi kufikia lengo limekuwa tatizo kubwa kwa wavaaji walio wengi. Kutokana na ukweli huo, mbunifu Ally Remtulah amekuja na dondoo kwa mavazi ya usiku;
Uzuri wa vazi
Jambo hili huanzia kwa mvaaji. Hakikisha unakubaliana na vazi lako, kwani kwa kufanya hivyo, itasaidia kukuonngezea kujiamini, hivyo kuonekana mrembo zaidi.
Kuwa huru katika kupiga hatua.
Hakisha viatu ulivyovaa vinakupa uhuru wa kutembea kwa madaha kadri uwezavyo, bila kukuvurugia utaratibu. Mwondoko mzuri mara nyingi una nafasi katika kukupendezesha na kulipa thamani vazi lako.
Wanawake wengi wamekuwa wakiamini kuwa nguo ya kubana ndiyo inayompendeza mtu, lakini ukweli ni kwamba nguo inayokupendeza ni ile inayokuweka huru. Haijalishi imebana sana ama fupi sana.
Usivae kitu cha ‘ajabu’ kama wewe si mtu wa ‘ajabu’.
Hakikisha unakuwa wewe halisi katika mavazi yako. Mavazi ya Lady Gaga ni utambulisho wake, hivyo hayawezi kuendana na mtu yeyote isipokuwa yeye mwenyewe. Hilo pia unapaswa kulifahamu.
Usichague vazi la bei rahisi.

Mwanamke, simamia kwenye ubora. Wakati mwingine kwa kuchagua kitu cha bei rahisi unaweza kujikuta unaishia kupoteza thamani yako halisi. Kwani hata wanaokutazama watakuona.
Usivae ‘Dar Combine’
Dar combine inamaanisha vazi linlovaliwa na wengi. Hivyo wewe mwanamke jitahidi kutafuta vazi la kipekee, siyo vibaya ukavaa hata la mtumba, lakini la mbunifu anayejulikana. Hii itasaidia kukufanya uoenekane unaelewa maana halisi ya mitindo.
Kuwa makini na mtindo wa nguo yako.
Kwa kuwa kila mmoja ana umbo la aina yake ni vyema unapochagua nguo kuangalia mtindo upi hasa unaendana na aina ya umbo lako. Ikiwa umbo lako linaendana na suruali, vaa suruali, lakini kama haliendani, usilazimishe.
Zingatia hali ya hewa
Katika uchaguzi wako ni muhimu kuzingatia hali ya hewa kwa wakati husika. Kuvaa vazi lisiloendana na hali ya hewa ya wakati husika, kunaweza kukuondolea hali yako ya kujiamini, hata pia kukufanya usiwe huru. Kitendo hicho huchangia kuharibu siyo tu mwonekano wako, bali hata wa vazi ulilovaa.
Imeandaliwa na Maimuna Kubegeya
Mitindo: Fashion Avenu
SOURCE: MWANANCHI