Wednesday, 11 September 2013

Profesa Maina auponda muundo wa Bunge la Katiba

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (Juwakita), Shamim Khan akichangia hoja kwenye warsha ya kujadili Rasimu ya Katiba Mpya iliyoandaliwa na Jukwaa la Katiba Dar es Salaam jana. Picha na Fidelis Felix. 

Na Fidelis Butahe

Posted  Jumanne,Septemba10  2013  saa 21:22 PM
Kwa ufupi
  • Ni ule wa kuchagua wajumbe 116 katika Bunge maalumu la Katiba.


Dar es Salaam. Mwanasheria maarufu, Profesa Chris Peter Maina ameuponda muundo wa Bunge la Katiba la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kushauri utizamwe upya kabla ya kufanyika kwa kura ya maoni mwakani.
Profesa huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar, alisema kama hilo lisipofanyika inaweza kupatikana Katiba Mpya yenye mlengo wa chama kimoja cha siasa na kufafanua kuwa tatizo hilo limetokana na upungufu katika sheria ya mabadiliko ya Katiba ambayo imefanyiwa marekebisho kidogo na kupitishwa na wabunge mjini Dodoma wiki iliyopita.
“Vyama vya siasa vinaweza kujipanga na kuweka watu wao katika zile nafasi 166 za wawakilishi wa kawaida katika Bunge maalumu la Katiba, hapohapo kumbuka kuwa wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi Zanzibar wanaingia katika Bunge hilo,” alisema.
Wakati Profesa Maina akieleza hayo, Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Profesa Palamagamba Kabudi alisema, kazi ya tume hiyo itaishia katika Mabaraza ya Katiba na kwamba katika hatua nyingine za Bunge la Katiba na kura ya maoni haitahusika.
Kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Bunge la Katiba litakuwa na wabunge 604 na wawakilishi 81 ambapo uwakilishi mkubwa utatoka katika vyama vya siasa huku CCM wakiwa na wabunge 398 sawa na asilimia 66 na upinzani wabunge 206 sawa na asilimia 34.
Alhamisi iliyopita wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walipitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, muswada ambao haukuungwa mkono na wabunge wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi kwa madai kuwa umejaa makosa mengi.
Kambi ya upinzani walitaka muswada huo usitishwe,huku wabunge wa CCM wakipinga,hali ambayo iliibua vurugu.
Wapinzani walikuwa wakipinga mambo kadhaa ikiwa ni kutokushirikishwa katika kutoa maoni kwa Wazanzibari na suala la Rais kupewa madaraka ya kuteua wajumbe wa Bunge maalumu la Katiba.
Akizungumza jana katika kongamano la Katiba lililoandaliwa na Jukwaa la Katiba (Jukata), Profesa Maina alisema ikiwezekana wabunge wanatakiwa kuelimishwa juu ya ushiriki wao katika bunge hilo ili watambue kuwa wanachokwenda kukifanya siyo kwa ajili ya kuwaondoa wao bungeni, bali ni kwa ajili ya Tanzania ya zaidi ya miaka 50 ijayo.
“Ukikosekana moyo wa dhati wabunge wanaweza kuizuia Katiba, inawezekana kabisa vikaingiza watu wao.Tatizo lilikuwa katika sheria ya mabadiliko ya Katiba, nadhani watu walikuwa na haraka ya kwenda katika mchakato huo. Katiba Mpya inapatikana katika Bunge la Katiba huo ndiyo wasiwasi wangu,” alisema.
Alisema kuwa Bunge hilo haliwajibiki kufuata Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwamba linaweza kuweka mambo yao wenyewe.
Profesa Kabudi alisema, kati ya hatua nne za kupata Katiba Mpya, hatua mbili ndiyo zinaihusu Tume ya Katiba moja kwa moja ambazo ni kukusanya maoni ya wananchi na makundi maalumu pamoja na Mabaraza ya Katiba, “Tume haitahusika katika Bunge la Katiba na kura ya maoni.”


Alisema katika utoaji wa maoni ya Katiba Watanzania walionyesha wazi kutotaka kuchezewa kwa miiko ya uongozi, uwajibikaji, maadili ya uongozi, uwazi, haki, usawa na amani, huku akisisita kuwa vitu hivyo ni vya msingi katika mustakabali wa nchi.
Alisema hata masuala yaliyotolewa maoni na wananchi lakini hayakuingizwa katika rasimu yanayohusu sera, sheria na utekelezaji yameorodheshwa na tume itawapatia viongozi ili wayasome.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukata, Deus Kibamba alisema mpaka sasa rasimu ya pili ya Katiba bado haijaandaliwa wakati Bunge la Katiba limepangwa kuanza mwezi Novemba mwaka huu.
“Tunataka kujua itachukua muda gani mpaka kupata rasimu hii ya pili. Hatujaridhishwa na marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya Katiba, hayana mashiko kwani uteuzi wa wajumbe 166 pamoja na uteuzi wa rais ni moja ya kasoro kubwa,” alisema.
Alifafanua kuwa mwakani kuna uchaguzi wa Serikali za mitaa, mwaka 2015, unafanyika uchaguzi mkuu hivyo Katiba hiyo haiwezi kuwa imepatikana.
“Kongamano hili litakuja na mapendekezo kadhaa ikiwa ni pamoja na kufikisha kilio hiki kwa Rais ili tushauriane naye kitatokea nini kama Katiba Mpya itakuwa haijapatikana katika chaguzi hizi, kama ikiwezekana turekebishe maeneo yanayohusu uchaguzi katikamaeneo yanayohusu uchaguzi katika Katiba ya sasa maana maoni yake yameshatolewa na wananchi.”
 
source: Mwananchi