Kwa ufupi
- Akieleza zaidi mahakamani hapo, Bensouda alisema kuwa Ruto na wenzake waliapa kutwaa madaraka kwa njia yoyote na walipoona jaribio lao kwa kuingia Ikulu kwa njia ya kura limeshindikana walianzisha hila kwa kuchochea machafuko ya kikabila.
Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto amekana mashtaka yote yanayomkabili kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama hiyo, Fatou
Bensouda anayesimamia kesi hiyo, alisema watuhumiwa wawili waliofikishwa
mahakamani hapo jana, Ruto na mtangazaji wa Redio, Joshua arap Sang
wanakabiliwa na mashtaka matatu kila mmoja, ambayo ni kuwalazimisha watu
kukimbia makazi yao, mauaji na kuchochea ghasia.
Kesi hiyo imeanza kusikilizwa siku chache baada ya
Bunge la Kenya kupiga kura kutaka nchi hiyo ijitoe uanachama wa ICC,
wakieleza kwamba imekuwa haina tija na inatumiwa kuwakandamiza Waafrika.
Ruto ambaye alionekana kujiamini alifika kwenye
jengo la Mahakama akiwa ameambatana na baadhi ya wabunge waliosafiri
kutoka Kenya hadi The Hague kwa ajili ya kumuunga mkono.
Mwendesha Mashtaka wa ICC, Fatou Bensouda alianza
kwa kusoma mashtaka matatu yanayomkabili kiongozi huyo wa Kenya na
akaiomba Mahakama hiyo kumtia hatiani kutokana na vurugu zilizojitokeza
baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Akiwasilisha hoja ya mashtaka, Bensouda alisema
kuwa Ruto ni mwanasiasa aliyejawa na kiu ya madaraka na wakati fulani
aliitii kiu yake kwa gharama ya maisha ya wengine. Alieleza kuwa Ruto
alianzisha machafuko alipoona shabaha yake kutwaa madaraka kwa njia ya
kura kushindwa.
“Ruto alikuwa mwanasiasa mwenye nguvu sana ambaye
alikuwa tayari kuratibu uhalifu dhidi ya binadamu ili kukidhi matakwa
yake ya kutwaa madaraka.
Ni vigumu sana kutathmini maumivu na mateso
waliyoyapata wanaume, wanawake na watoto ambao baadhi yao walichomwa
moto huku macho yao yakishuhudia kile kilichotendeka. Wengi waliteswa
hadi kufa huku wengine wakitimuliwa kutoka kwenye nyumba zao na kwenda
kuishi uhamishoni,” alisema Bensouda katika sehemu ya hoja
zilizowasilishwa na upande wa walalamikaji.
Akieleza zaidi mahakamani hapo, Bensouda alisema
kuwa Ruto na wenzake waliapa kutwaa madaraka kwa njia yoyote na
walipoona jaribio lao kwa kuingia Ikulu kwa njia ya kura limeshindikana
walianzisha hila kwa kuchochea machafuko ya kikabila.
Alisema upande wa walalamikaji uko tayari
kuthibitisha madai kwamba Ruto alihusika kuandaa mashambulizi dhidi ya
wananchi wa kabila la Kikuyu.
“Tupo tayari kudhibitisha madai yetu pasipo na
shaka yoyote kwamba mashambulizi ya Wakikuyu yaliratibiwa na kutekelezwa
na wahusika hawa,” alisema Bensouda.
Wakati Bensouda akiendelea kuwasilisha ushahidi
upande wa pili, Ruto alionekana kuwa mtulivu na wakati fulani alitikisa
kichwa na kisha akanyanyua glasi ya maji na kunywa. Kuna wakati pia
alitabasamu na kuendelea kufuatilia kwa makini ushahidi wa upande wa
walalamika.
Ruto akana mashtaka
“ Sasa Ruto ni fursa yako kusimama na kujitetea
kuhusiana na mashtaka yaliyopo mbele yako,” alisema mmoja wa majaji
kwenye kesi hiyo. Wakati aliposimama Ruto hakuwa na maneno mengi mbali
ya kurudia maneno yake mara tatu “Sina hatia, sina hatia, sina hatia”.
Ilipowadia zamu ya utetezi wa upande wa
washtakiwa, Mwanasheria wa Ruto, Karim Khan alikosoa vikali maelezo ya
walalamikaji aliyoyaita kuwa ni “uzushi” na baadhi ya washahidi
walirubuniwa kwa fedha ili kutoa ushahidi wa uwongo.
“ Waheshimiwa majaji, najua haki ni muhimu
itendeke, lakini katika hili hakuna ukweli wowote. Sehemu kubwa ya
ushahidi uliotolewa na walalamikaji na hapa singependa nimlalamikie
Bensouda kwani ushahidi huu ulikusanywa na mtangulizi wake Ocampo…hakuna
ukweli wowote.
“ Ushahidi huu umekusanywa bila ya kuwepo mwongozo
wa Mahakama hii waheshimiwa majaji… tena napenda nithibitishe hapa,
Ruto ni mwanasiasa mwadilifu tena mtu safi aliyeletwa kwenye Mahakama
hii kwa makosa,” alisisitiza Khan katika sehemu ya ushahidi wake.
Ili kuonyesha msisitizo wa hoja zake, Mwanasheria
Khan alilazimika kutumia sehemu ya mahojiano yaliyofanywa baina ya Ruto
na Mtangazaji wa K24 Jeff Koinange.
Inakariwa kuwa zaidi ya watu 1,200 walipoteza
maisha wakati wa machafuko hayo ya baada ya uchaguzi na wengine 600,000
walifurumishwa toka sehemu zao na kwenda kuishi maeneo ya mbali kwa
kuhofia usalama wa maisha.
Taarifa za hivi karibuni zinasema kuwa zaidi ya
watu 40,000 bado wanaendelea kuishi kwenye makambi kutokana na makazi
yao kuharibiwa.
Hata hivyo serikali ya Rais Uhuru Kenyatta wiki
iliyopita ilisema kuwa hadi ifikapo Septemba 20 mwaka huu kambi hizo
zitakuwa zimefungwa na wahusika wake watapatiwa msaada wa fedha ili
kujenga nyuma mpya.
Baadhi ya mlolongo wa matukio muhimu kabla ya machafuko na baada ya machafuko hayo
Rais Mwai Kibaki alitangazwa mshindi wa uchaguzi
wa mwezi Desemba 2007 huku mpinzani wake Raila Odinga aliyalalamikia
matokeo hayo
• Vuguvugu la upinzani lilianza rasmi na kufuatiwa na machafuko
yaliyosambaa nchi nzima. Vikosi vya polisi vilikabiliana vikali na
makundi ya waandamanaji.
• Kiasi cha watu 1,200 waliuawa na wengine 600,000 walikimbia nyuma zao
• Uhuru Kenyatta aliyekuwa kwenye kambi ya Kibaki alishutumiwa kwa kuchochea mapigano dhidi ya wafuasi wa Odinga.
• William Ruto aliyekuwa kwenye kambi ya Odinga alilalamikiwa kwa kuchochea mapigano dhidi ya wafuasi wa Kibaki
• Kilianzishwa majadiliano ya kusaka amani na
baadaye April 2008 mkataba kugawana madaraka ulisainiwa kutokana na
majadiliano yaliyoendeshwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
cKofi Annan
• Machi 23, 2013 Kenyatta na Ruto waliungana na kufanikiwa kushinda uchaguzi mkuu
• Septemba 10, kesi dhidi ya Ruto ilianza rasmi wakati kesi dhidi ya Kenyatta akitazamiwa kuanza Novemba
Macho yake yanapepesa kwa umbali mfupi na kisha
anaelekea moja kwa moja katika chumba maalumu ambacho kimefurika
wataalamu wa sheria.
source: Mwanachi
source: Mwanachi