Na Frederick Katulanda
Posted Jumatano,Septemba11 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumatano,Septemba11 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Walalamika kuporwa ardhi na baadhi ya viongozi wa
halmashauri ya wilaya, maofisa usalama, polisi kuwazingira na kuwapora
mabango hayo.
Sengerema. Polisi katika Mkoa wa Mwanza pamoja
na maofisa Usalama wa Taifa wamezima jaribio la wakazi wapatao 10 wa
Kijiji cha Kamanga ambao walikuwa na mabango kulalamikia kuporwa ardhi
yao na baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya Wilaya bila ya fidia.
Sakata hilo limetokea saa 5:30 asubuhi wakati Rais
Jakaya Kikwete akiwa amewasili wilayani Sengerema kupitia njia ya maji
baada ya kuvuka na Kivuko cha Kamanga huku wananchi hao wakijipanga
kuonyesha mabango yao.
Hata hivyo watu ambao idadi yao ilikuwa yapata 10,
wakiwa katika harakati za kutoka na mabango hayo walizingirwa na
maofisa usalama na baadaye polisi na kuanza kupokonywa mabango yao.
Hatua hiyo ya kufika kwa maofisa polisi
kuliwafanya baadhi yao wengine kutimka na mabango na hivyo kufanikiwa
kudaka watatu wakiwa na mabango yao.
Baadhi ya mabango yaliyoonekana kuwa na maneno
yanayolalamikia kuporwa ardhi zao bila ya kulipwa fidia, huku bango
lingine likimtaka Rais Kikwete kusaidia tatizo la ardhi baina ya vigogo
na wananchi.
Sakata la ardhi katika kijiji cha Kamanga
linadaiwa kuibuka baada ya mmiliki wa Kivuko cha Kamanga kufariki na
wajanja kujipenyeza kuandaa watu wanaoitwa wananchi kulalamika wakidai
hawajalipwa fidia.
“Hapa kuna mgogoro wa muda mrefu, kuna kundi la
watu waliibuka na kuzua madai ya kuporwa maeneo yao na mmiliki wa
Kamanga, lakini baada ya kufuatilia tulichobaini ni kuwa walitumia
nafasi ya kufariki kwa mmiliki wa kivuko kutaka kulipwa fidia, lakini
tumewahi kuzikutanisha pande zote mbili, hawa wanaolalamika walilipwa
wazazi wao fidia,” alieleza mmoja wa askari polisi ambaye hakupenda
kutajwa jina lake gazetini.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amemshukia
ofisa mifugo wa wilaya ya Kwimba na kusema ni kikwazo cha maendeleo
kutokana na kukwama kwa mpango wa uzalishaji ng’ombe kwa njia ya kisasa
ya uhamilishaji mbegu (AI).
Akizungumza wakati wa kujadili taarifa ya
maendeleo ya Wilaya ya Kwimba iliyosoma na Mkuu wa Wilaya, Selemani Mzee
alisema njia ya kuzalisha ngombe wa kisasa kwa kupandisha na madume
ambayo inatumiwa wilayani humo haiwezi kuleta mafanikio ya haraka na
kusema tatizo ni ofisa mifugo, Eliakim Ole Wavia.
“Hebu kwanza…., mmesema mnazo ngo’mbe 390,000 sasa
kama mnatumia njia ya kupandikiza mbegu ya kisasa kwa kutumia madume 12
kwa idadi hiyo ya ng’ombe lengo la kumaliza mifugo 390,000
silitakamilika miaka 100. Kwa nini hamtumii njia ya kupandisha mbegu,”
alihoji Rais Kikwete.
Akitoa ufafanuzi Ofisa Mifugo wa Wilaya, Eliakim
Ole Wavia alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kupandisha mbegu 38 na
kupata mimba tatu hivyo waliamua kutumia njia ya kupandisha madume na
kwa kuanza walianza na madume 12, lakini katika mkakati mpya wamepanga
kuongeza madume 32 kwa wastani wa dume moja kwa jike 32.
Hatua hii ilimshangaza Rais Kikwete na kumweleza
ofisa mifugo kama kikwazo cha kufanikiwa kwa mpango wa uhamilishaji na
kwamba ili mpango huo ufanikie naye anatakiwa kubadilishwa vinginevyo
njia anayotumia italeta mafanikio katika kipindi cha miaka 100 wa idadi
ya ng’ombe 390,000.
“Wewe bwana mifugo unanishangaza sana, mbona mimi shambani
kwangu ninapandikisha kwa njia ya mbegu na mafanikio ni mazuri sana.
Sasa ilikuwaje nyinyi mbegu 38 mpate mimba tatu, basi wewe na
mnaopandisha siyo watalaamu,” alieleza Rais Kikwete na kuanza kutoa somo
la uhamilishaji akieleza anavyofanya yeye katika shamba lake Chalinze.
Alisema ukiwa na watalaamu wazuri kazi ya kwanza
huwa ni kuchagua dume bora la mbegu na kisha kulidanganya ili kupata
mbegu na kwamba mbegu zinapopatikana jike huchomwa sindano maalumu
ambayo katika kipindi cha saa 72 hupevusha yai na ndipo mbegu
hupandikizwa. Katika mpango huo uhakika ni asilimia 100 na hata ikikwama
huwa ni mafanikio asilimia 80 kiasi ambacho ni kikubwa.
source: Mwananchi
source: Mwananchi