Kwa ufupi
Kwesigabo alizitaja bidhaa za vyakula
zilizochangiwa kupungua kwa mfumuko wa bei na kiwango cha punguzo kwa
asilimia katika mabano kuwa ni pamoja na mikate na nafaka (2.2),
vitafunwa (3.8), mahindi ( 1.6), unga wa ngano (2.5), unga wa muhogo (
0.6) na unga wa mtama (3.4).
Dar es Salaam. Mfumuko wa bei nchini umezidi
kupungua na sasa umefikia asilimia 6.7 kwa mwezi Agosti, 2013, kutoka
asilimia 7.5, Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) imebainisha, katika
taarifa yake ya matokeo ya mfumuko wa bei kwa mwezi Agosti.
Akizungumza na waandishi wa habari jana,
Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa NBS, Ephrahim Kwesigabo
alisema kupungua kwa mfumko huo wa bei kunamaanisha kuwa kasi ya
upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa mwezi Agosti imepungua
kulinganisha na mwezi Julai.
“Kwa kiasi kikubwa kupungua kwa mfumuko wa bei
nchini kumechangiwa na kupungua kwa mfumko wa bei za bidhaa za vyakula
na vinywaji baridi kutoka asilimia 8.0, mwezi Julai hadi asilimia 6.5,
mwezi Agosti, 2013.”, alisema Kwesigabo.
Hata hivyo Kwesigabo alisema kwa upande mwingine
kasi ya ongezeko la bei kwa bidhaa zisizo za vyakula imebakia kuwa
ileile ya asilimia 7.3, kama ilivyokuwa Julai 2013.
Alisema kupungua kwa mfumuko huo wa bei kuna
maanisha kuwa kuna unafuu wa maisha kwa mlaji na kwamba hiyo inaonesha
kuwa Tanzania inapiga hatua nzuri katika uchumi wa nchi.
Kwesigabo alizitaja bidhaa za vyakula
zilizochangiwa kupungua kwa mfumuko wa bei na kiwango cha punguzo kwa
asilimia katika mabano kuwa ni pamoja na mikate na nafaka (2.2),
vitafunwa (3.8), mahindi ( 1.6), unga wa ngano (2.5), unga wa muhogo (
0.6) na unga wa mtama (3.4).
Bidhaa nyingine ni kuku wa kienyeji (0.9), samaki
wabichi (2.6), karanga (2.0, mbogamboga (2.4), nyanya (9.9), vitunguu
maji ( 2.0), viazi vitamu ( 4.8), mihogo (4.1) na sukari ( 0.5).
“Bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kupungua
kwa mfumuko wa bei ni viatu (0.3), samani (0.1), vyombo vya udongo
(1.0), vifaa vya elektroniki vya kurekodia picha na sauti (0.3).”,
aliongeza Kwesigabo.
Akizungumzia uwezo wa shilingi ya Tanzania katika
kununua bidhaa na huduma, alisema umepungua kwa Sh28.54 na kufikia
Sh71.46, kutoka mwezi Septemba, 2010 hadi sasa.
soource: Mwananchi
soource: Mwananchi