Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Posted Jumatatu,Novemba4 2013 saa 7:50 AM
Posted Jumatatu,Novemba4 2013 saa 7:50 AM
Kwa ufupi
Dar es Salaam. Mjumbe wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba nchini, Dk Sengondo Mvungi amejeruhiwa usiku wa
kuamkia jana, baada ya kukatwa kwa mapanga na watu wasiojulikana
waliovamia nyumbani kwake Mpiji-Magohe, jijini Dar es Salaam.
Dk Mvungi, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Katiba,
Sheria na Haki za Binadamu wa NCCR-Mageuzi aliwahishwa kwenye Taasisi ya
Mifupa Hospitali ya Muhimbili (MOI), ambako amelazwa katika wodi
maalumu huku hali yake ikiwa mbaya.
Taarifa kutoka kwa ndugu na watu waliomtembelea
hospitalini hapo wanasema kwamba hali ya Dk Mvungi ni mbaya kwani
alikuwa hawezi hata kuzungumza.
Akisimulia tukio hilo, dereva wa Dk Mvungi
anayeitwa Emmanuel Ntaro, alisema akiwa nyumbani kwake majira ya saa
6:30 usiku, alisikia mlipuko mkubwa kisha zikasikika kelele zikitokea
nyumbani kwa bosi wake.
“Nilifika na kukuta hajitambui, tukampeleka
Hospitali ya Tumbi Kibaha mkoani Pwani alikopatiwa huduma ya kwanza
kabla ya kumpeleka MOI ambako anaendelea kuchunguzwa na kupatiwa
matibabu,” alieleza Ntaro
Alisema kuwa watu wapatao sita, walivamia nyumbani
kwa Dk Mvungi ambako baada ya kuvunja mlango na kuingia ndani,
walimjeruhi kwa kutumia mapanga huku wakidai wapatiwe fedha. Watu hao
walimsababishia majeraha usoni, kichwani na sehemu nyingine za mwili.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema mbali na kupata matibabu MOI, pia
walilazimika kumpeleka Hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya vipimo zaidi
katika mashine ya CT Scan kama walivyoshauriwa na madaktari wa zamu.
Mbatia alisema kuwa baada ya Dk Mvungi kufanyiwa
kipimo hicho alirudishwa tena MOI kwa matibabu na uangalizi maalumu.
“Hali yake inaanza kuimarika tofauti na nilivyomuona saa nne asubuhi, “
alisema Mbatia muda wa saa 12 jioni jana alipozungumza na gazeti hili.
Alisema kwamba pia watu waliohusika na tukio hilo waliiba kompyuta mpakato (laptop) pamoja na bastola ya Dk Mvungi.
Kamanda wa Mkoa wa kipolisi Kinondoni, Cammilius Wambura alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
“Kweli hilo ni tukio la kihalifu na sisi
tunaendelea kulifanyia kazi. Tunawahakikishia Watanzania kuwa watu hao
watapatikana na kufikishwa kwenye mkono wa kisheria,” alisema.
Kilichotokea
SOURCE: MWANANCHI
Akisimulia tukio hilo, mtoto wa Dk Mvungi anayeitwa Deogratius
Mwarabu, alisema kuwa walipigiwa simu na mdogo wao saa 7.00 usiku wa
kuamkia jana na aliwaeleza kuwa baba yao alikuwa amevamiwa na watu
wanaodhaniwa kuwa majambazi.
Mwarabu alisema watu wapatao sita walivamia katika
nyumba ya Dk Mvungi na kwenda chumba cha nje cha nyumba hiyo anachoishi
fundi wa nyumba hiyo.
Watu wanne ndio walikwenda katika chumba hicho na
kumpiga na nondo mfanyakazi huyo na kumlazimisha awaonyeshe chumba cha
Dk Mvungi. Mwarabu alisema baada ya kumpiga walimfunga kamba mfanyakazi
huyo kisha kwenda kwenye nyumba kubwa kwa kupitia mlango wa jikoni.
Alisema kuwa baada ya Dk Mvungi kusikia kelele aliamua kutoka chumbani
na ndio akakutana na watu hao wakiwa tayari kwenye nyumba anayoishi.
“Walimkata panga utosini halafu wakampiga usoni kwa kutumia ubapa wa panga. Aliangukia upande wa uso,” alisimulia Mwarabu.
Baada ya tukio hilo, watu hao walimwamuru
mfanyakazi aliyekuwa amefungwa kamba alale chini huku wengine
wakiendelea kufanya upekuzi kwenye nyumba hiyo.
Alisema baada ya hapo walikwenda kwenye chumba anacholala Dk Mvungi na kumkuta mkewe, ambaye walimwamuru awape fedha.
“Mama alitoa fedha, lakini hatukuweza kujua ni kiasi gani alichotoa. Maana tumemwacha apumzike kwanza,” aliongeza Mwarabu.
Kwa mujibu wa Mwarabu, majambazi hao baada ya
kupewa fedha, walidai kuwa fedha hizo hazitoshi na kutaka mke wa Dk
Mvungi awaongezee zaidi.
“Walimtishia mama kuwa wangemchinja kama asingetoa
fedha zaidi, naye akasisitiza hakuwa na fedha na kuwaruhusu wamchinje,”
alisema Mwarabu.
Katika kushinikiza atoe kiasi cha fedha zaidi,
watu hao walimpiga kwa stuli Mama Mvungi na kumuumiza miguu yake ndipo
wakaanza kupekua kwenye makabati ya chumba chao cha kulala.
Kwa mujibu wa mtoto huyo wa Dk Mvungi, mbali na
kuchukua kompyuta na bastola watu hao walichukua simu tano, ambapo mbili
zikiwa za Dk Mvungi, mbili za mama yao na moja ya mfanyakazi wao.
Alisema katika nyumba hiyo wanaishi watu sita. Dk Mvungi, mkewe, fundi
wa nyumba na wajukuu watatu.
Mwananchi ilipomtafuta tena Mwarabu jana jioni
kujua hali ya Dk Mvungi, alisema kwamba bado baba yake yuko mahututi na
kwamba alikuwa hawezi kuzungumza
JK amjulia hali
Rais Jakaya Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi waliokwenda kumwona Dk Mvungi hospitalini alikolazwa.
Viongozi wengine waliokwenda kumtazama ni pamoja
na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema, Mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Warioba na Makamu wake Jaji
Agustino Ramadhan.
Warioba asikitika
Naye Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Jaji Joseph Warioba alisema tukio hilo ni baya na limewashtua na
kuwaachia simanzi. Alisema kuwa wanasubiri taarifa itakayotolewa na
vyombo vya usalama kuhusu tukio hilo.
“Hali ya mwenzetu ni mbaya, nimemwona hospitalini
na kwa kuwa alikuwa bado anahudumiwa na madaktari, sina cha kueleza
zaidi ya kuwaomba matabibu wetu waendelee kupigania afya yake ili arejee
katika hali yake ya kawaida,” alieleza Jaji Warioba.
Jaji Warioba aliwaomba Watanzania wote waungane
kumwombea mjumbe huyo, ambaye ni kiungo muhimu katika tume hiyo na
kwamba kumkosa katika kipindi hiki ni dhahiri kutaongeza pengo katika
utendaji wa kila siku.
Naibu Katibu wa Tume hiyo, Casmir Kyuki alisema
tukio hilo analichukulia kuwa ni la kihalifu na kwamba kuna uwezekano
ndio athari za kauli zinazotolewa na wanasiasa dhidi yao (watumishi wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba), kwamba wanalipwa pesa nyingi.
“Hawa watu walilenga kupata pesa ambazo waliamini
mwenzetu alikuwa nazo. Hii inatokana na watu hasa wanasiasa kusema
maneno bila hata kujiridhisha,” alieleza Kyuki.
Kyuki alisema wajumbe wa tume wanaishi uraiani
bila ulinzi wowote kwa sababu wanafahamu hali zao ni za kawaida, lakini
kutokana na maneno dhidi yao jamii inadhani kuwa wana fedha nyingi sana.
“Magari tunayotumia yana nembo, watu wanafanya kazi mpaka usiku, matokeo yake ndiyo hayo,” alisema Kyuki.
SOURCE: MWANANCHI