Monday 4 November 2013

STORY YA KUHUZUNISHA YA MTOTO Carlos STEVEN


Na Mwandishi wetu
STORY YA KUHUZUNISHA YA MTOTO Carlos STEVEN  ALIYETOLEWA MWANZA KUJA DAR KIMASOMO NA KUPOTEZANA NA BABA YAKE UBUNGO...INALETA CHANGAMOTO

“Nilifika na baba hapa alinichukua toka Mwanza akaniambia ananileta kwa shangazi anayeishi hapa kuja kusoma” anasema Carlos.

Hebu tafakari, kijana wa miaka 12 ambaye hajawahi kufika jijini Dar es Salaam, anafika Ubungo kwa mara ya kwanza akiwa na baba yake, na ghafla wanapotezana.

Hii ilimtokea kijana, Carlos Steven, 13 ambaye alifika hapa jijini mwezi Januari akitokea Mwanza yeye pamoja na baba yake. Baada tu ya kufika katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo, Carlos alipotezana na baba yake.

“Nilifika na baba hapa alinichukua toka Mwanza akaniambia ananileta kwa shangazi anayeishi hapa kuja kusoma” anasema Carlos

Kwa bahati mbaya, Carlos hakuweza kumpata baba yake na matokeo yake, aliishia kuishi katika mitaa ya jiji la Dar es Salaam ambapo kwa sasa anaishi kwa kuuza chupa tupu za maji na kucheza kamari.

Carlos ambaye ameishia darasa la sita anasema: “Natamani kurudi nyumbani na kumuona baba yangu lakini sielewi namna ya kumpata, nnachojua ni kuwa anaitwa Steven John”

Carlos pamoja na watoto wengine wa mitaani katika eneo hili wanaishi maisha yasiyo na utofauti na wanyama. Wanaoga katika Mto wa Msimbazi nyakati za usiku wakati watu wote wamelala.

Wanalala katika vibaraza vya maduka katikati ya jiji ambapo hata hivyo hutakiwa kuchangia gharama ya malazi ya shilingi 200 hadi 300 kwa usiku mmoja.

Chanzo chao kikuu cha mapato ni kuuza chupa tupu zinazozagaa kwa wenye viwanda na kampuni ambazo zinanunua chupa hizo kwa kilo na kucheza kamari au kuombaomba pembezoni mwa barabara.

Hata hivyo, fedha hizo wakati mwingine huenda zisiwe riziki kwao kwani usiku wanapolala vibaka au watoto wa mitaani wenye nguvu zaidi yao, huwanyang’anya kwa nguvu fedha hizo.

Haya ndiyo maisha ya watoto wa mitaani ambapo si Carlos pekee bali lipo kundi kubwa la vijana wanaoishi mitaani Tanzania nzima.

Tovuti ya Humanium Help the Children(HHC) inaeleza kuwa katika Jiji la Dar es Salaam pekee kuna watoto 3,000 hadi 5,000 ambao wanaishi mitaani.

Pia tovuti hiyo inaeleza kuwa watoto hao wengi wao wana umri wa kuanzia miaka mitano hadi 18 ambapo asilimia 80 kati yao ni wanaume wenye umri wa miaka saba hadi 14.

Mkurugenzi wa Elimu kwa Watoto, kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto,(Unicef) Dk Victoria Masabo anasema tatizo la watoto wa mitaani linaendelea kuwa kubwa na gumu kwa sababu kadhaa ikiwemo wazazi na walezi.

“Wazazi na walezi ndiyo watu wa kwanza wanaotakiwa kuhakikisha kuwa mtoto anaishi salama, kuhakikisha yupo wapi na anafanya nini,’ anasema

Anasema talaka, kuvunjika kwa familia na migogoro ndicho chanzo kikubwa kinachosababisha ongezeko la watoto wa mitaani.

Anashauri kuwa taasisi zitafute njia mbadala kuhakikisha kuwa watoto wa mitaani wanapata maeneo maalumu kwa ajili ya watoto hao na wahakikishe wanakaa katika maeneo hayo, wanapata elimu hadi watakapokuwa watu wazima.

Dk Masabo anasema tatizo hili la watoto wa mitaani lisipofanyiwa kazi basi taifa litazalisha wezi, majambazi, makahaba na kizazi haribifu.

Ipo sheria Tanzania ambayo inaeleza kuwa iwapo polisi atamkuta mtoto wa mitaani anayeonekana hana umiliki wa wazazi, basi atatakiwa amchukue na kumpeleka katika taasisi.

Sheria ya watoto ya mwaka 2009 inakataza watoto kuzagaa mitaani na iwapo wataonekana mitaani basi sheria hiyo inasema wanatakiwa kupelekwa kwa ofisa ustawi wa jamii.

Afisa ustawi wa jamii anatakiwa afuatilie iwapo mtoto au watoto hao wana wazazi na kama hawana wazazi basi watafutiwe wazazi mbadala na kama hao pia hawatapatikana basi watoto hao wapelekwe katika vituo maalum au taasisi.

Kwa bahati mbaya, sheria hii haifuatiliwi na wanajamii au hata na polisi watunza sheria, na matokeo yake watoto wa mitaani wanakosa haki zao na furaha ya utoto wanayotakiwa kuipata.

Mwisho.