Kwa ufupi
Pamoja na kusema kwa muda mrefu kwamba inayo
majina ya ‘magwiji wa unga’, wakiwamo baadhi ya wafanyabiashara na
wabunge, Serikali bado imeshikwa na kigugumizi kuwataja hadharani au
kuwafikisha mbele ya sheria.
Habari kwamba Serikali inaandaa Muswada wa aina
yake wa Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini hakika ni za kutia
moyo. Tunasema zinatia moyo kutokana na Muswada huo kupendekeza
uundwaji wa taasisi itakayopewa meno na madaraka kamili kupambana na
biashara ya madawa hayo. Kama sote tunavyofahamu, biashara hiyo ya dawa
za kulevya imepanuka kwa kasi ya kutisha na kuharibu maisha ya vijana
wengi, mbali na kuchafua jina na taswira nzuri ya taifa letu mbele ya
jumuiya ya kimataifa.
Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imekuwa
kichekesho cha dunia kutokana na Watanzania wengi kukamatwa kila kona ya
dunia wakisafirisha dawa hizo. Ripoti ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya
Kupambana na Mihadarati na Uhalifu (UNODC), imesema Tanzania ni kinara
wa kupitisha dawa za kulevya katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Takwimu zinaonyesha kwamba maelfu ya Watanzania
wanashikiliwa katika magereza katika nchi nyingi duniani na wengine
wengi wamenyongwa baada ya kutiwa hatiani na mahakama za nchi ambazo
hazina chembe ya uvumilivu wa biashara hiyo, ikiwamo China.
Ni vigumu kujua jinsi Tanzania iliyokuwa
ikiheshimika sana duniani imebadilika ghafla na kuwa kinara wa dawa za
kulevya. Haipiti siku bila kutangazwa habari za Watanzania kukamatwa
wakiwa na shehena kubwa za dawa hizo katika sehemu mbalimbali duniani.
Jambo la kushangaza ni kwamba wanaokamatwa ni
vijana wanaopewa dawa hizo na wafanyabiashara wakubwa ili kuzisafirisha,
huku wafanyabiashara hao wakiendelea kutesa mitaani.
Pamoja na kusema kwa muda mrefu kwamba inayo
majina ya ‘magwiji wa unga’, wakiwamo baadhi ya wafanyabiashara na
wabunge, Serikali bado imeshikwa na kigugumizi kuwataja hadharani au
kuwafikisha mbele ya sheria. Ndiyo maana tunasema hatua ya Serikali ya
kuandaa Muswada huo wa aina yake ili kuunda chombo chenye meno ya
kupambana na biashara hiyo hakika ni ya kupongeza.
Ni hatua ya kupongeza kwa sababu Serikali sasa
inaonyesha utashi na dhamira ya kupambana na biashara hiyo. Ni kweli
hatua hiyo imekuja ikiwa imechelewa sana kiasi cha tatizo hilo kuonekana
kuizidi kimo, lakini tunaamini muundo, madaraka na meno kitakachopewa
chombo hicho vitatosha kuiangamiza biashara hiyo haramu iwapo
watateuliwa watendaji wenye uadilifu kukiongoza.
Ni habari njema kwamba Muswada unaotayarishwa
unapendekeza chombo hicho kiwe huru, mbali na kuwa na vitengo vyake
vyenye madaraka ya kufanya uchunguzi, kukamata watuhumiwa na
kuwafungulia mashtaka bila kutegemea Jeshi la Polisi nchini. Chombo
hicho kitakuwa na makazi ya pamoja na Mahakama Maalumu itakayoundwa
kuendesha kesi hizo ambazo zitachukua muda mfupi kabla ya hukumu
kutolewa. Hivi sasa kesi hizo zinachukua zaidi ya miaka 10 kumalizika.
Muswada huo unataka watakaopatikana na makosa
wasiwe tena na uhuru wa kulipa faini. Mahakama nazo hazitaruhusiwa kutoa
dhamana kwa watuhumiwa na dawa zitakazopelekwa mahakamani kama ushahidi
zitaharibiwa mara moja, kinyume na sasa ambapo ushahidi huo unatunzwa
kwa muda mrefu. Uzoefu umeonyesha kwamba dawa hizo hupotea au
huchakachuliwa katika mazingira ya kutatanisha.
Tuna kila sababu ya kuwa na matumaini kwamba sasa
kiyama cha wauza ‘unga’ kimewadia. Tunaipongeza Serikali kwa kuweka
mbele masilahi ya taifa kwa kuandaa Muswada usio na simile katika
kupambana biashara hiyo haramu na hatari.
source: Mwananchi
source: Mwananchi