Rais Kikwete alimpigia simu rais Kenyatta jioni ya Jumamosi
kutokea mjini New York, marekani, mara baada ya kuwasili mjini humo
akitokea Toronto, canada, ambako alifanya ziara ya kikazi ya siku tatu.
Katika mazungumzo kati ya viongozi hao, rais Kikwete amemweleza rais
Kenyatta mshtuko na hasira yake kutokana na taarifa za kusikitisha za
shambulio hilo la kigaidi .
Rais Kikwete amefuatilia mazungumzo hayo kwa salamu rasmi za
rambirambi ambazo rais Kikwete amemtumia rais Kenyatta akielezea
masikitiko na hasira yake kufuatia mauaji hayo ya watu wasiokuwa na
hatia akitaka kujua jinsi Tanzania inaweza kusaidia juhudi za serikali
ya Kenya katika kukabiliana na madhara ya tukio hilo na balaa la ugaidi
kwa jumla.
Katika salamu zake rais Kikwete amesema shambulio hili linalenga
kuitisha serikali na wananchi hodari wa Kenya na kudhoofisha nia yao ya
kutimiza wajibu wao wa kihistoria wa kuunga mkono jitihada za kuleta
amani katika nchi jirani na yenye matatizo ya Somalia. Rais amesema kwa
maana hiyo, shambulio hilo la woga na lisilo na huruma kabisa dhidi ya
watu wasiokuwa na hatia, lazima lilaaniwe na kushutumiwa vikali na
wapenda amani wote.
Amesema serikali na wananchi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania
wanasimama bega kwa bega na kaka na dada zao wa Kenya katika kipindi
hiki kigumu. Aidha, serikali ya Tanzania inapenda kuihakikishia serikali
ya Kenya itaendelea kuiunga mkono na kushirikiana nayo katika kupambana
na balaa la ugaidi katika sura zake zote.
SOURCE: ITV-DAIMA