Wednesday, 9 October 2013

Haramia mkuu wa zamani wa Somalia sasa aongoza mapambano dhidi ya uaharamia

Mahojiano na Abdi Moalim, Mogadishu
Oktoba 08, 2013
Mohamed Abdi Hassan aliyekuwa haramia wa Somalia, ambaye anajulikana kwa lakabu ya "Afweyne", wakati fulani alikuwa mmoja wa viongozi wa maharamia waliokuwa wakiogopwa sana ambaye alikuwa akifanya kazi hiyo pwani ya katikati ya nchi hiyo.
  • Mohamed Abdi Hassan 'Afweyne' akizungumza kuhusu Shirika Linalopambana na Uharamia Nchini Somalia, ambalo alilianzisha kusaidia kuwarekebisha waliokuwa maharamia, kwenye mkutano huko Mogadishu tarehe 18 Septemba, 2013. [Abdi Moalim/Sabahi] Mohamed Abdi Hassan 'Afweyne' akizungumza kuhusu Shirika Linalopambana na Uharamia Nchini Somalia, ambalo alilianzisha kusaidia kuwarekebisha waliokuwa maharamia, kwenye mkutano huko Mogadishu tarehe 18 Septemba, 2013. [Abdi Moalim/Sabahi]

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka wa 2012 ya Kikundi cha Ufuatiliaji cha Umoja wa Mataifa kwa Somalia, Afweyne na mtoto wake wa kiume Abdiqaadir walihusishwa katika utekaji nyara wa meli saba kati ya Aprili 2009 na Oktoba 2012.
Lakini baada ya kutangaza mwezi Januari kwamba alikuwa ameyatoa maisha yake kwenye "shughuli za gengi" kwenye bahari kuu, Afweyne amejishughulisha katika jitihada katika mikoa ya Mudug na Galgadud akibadilisha zaidi ya vijana 1,000 ambao walifuata uongozi wake na kujitoa kwenye uharamia.
Katika mahojiano ya kina na Sabahi, Afweyne, ambaye sasa ana umri wa miaka 60, alikana kuwa alishawahi kuchukua mateka au kukusanya fedha haramu, lakini alisema unajutia kazi aliyoifanya siku za nyuma na sasa ameachana nayo.
Sabahi: Ilikuaje ukawa mtu maarufu kwa uharamia?

Afweyne: Nilikuwa namiliki kampuni kubwa ya uvuvi na matokeo yake yalikuwa makubwa, lakini wakati meli za nje zilipotushambulia na tusingeweza kutoka baharini au kuendesha maisha, tuliamua kuchukua hatua ya kujilinda wenyewe, ambayo ilikuwa njia halali ya ulinzi binafsi na haikuwa kuharibu biashara au msaada.

Tulikuwa tunapambana na wale waliokuwa wakiharibu bahari na kutuzuia kuingia. Kwa hivyo, sikuwa mtekaji nyara, lakini nilikuwa kiongozi wa harakati hizi halali za ulinzi binafsi. Tuliwaandaa vijana katika mkoa na nia ilikuwa kujilinda wenyewe na siyo kuteka nyara.
Tulianza shughuli hizo mwaka 2004. Hata hivyo, niliiacha baadaye wakati ilipobadilika kuwa utekaji na uharamia.

Sabahi: Je, ni lini ulianza kupambana dhidi ya uharamia?

Afweyne: Mwezi Julai 2011, nilianza kujifunza jinsi ya kufanya chochote kuhusu [kupambana na uharamia]. Nilipokuwa na uhakika kwamba ninaweza kuchukua hatua dhidi ya hilo, serikali ilinipa ruhusa kamili ya kupambana na uharamia. Kuanzia wakati huo hadi sasa, nimepata mafanikio ya mfululizo na kufanikiwa katika kuwaleta pamoja [maharamia wengi] katika kituo kimoja.
Sabahi: Kwa nini umeamua kupambana dhidi ya hatua ambayo uliianzisha mwenyewe?

Afweyne: Kuna sababu mbili katika hili.

La kwanza ni kwamba sitaki jina baya kwa nchi yangu na nilifanya uamuzi huu kwa dhamiri yangu na uzalendo wangu […] na lengo langu ni kutokomeza uharamia kwa Somalia nzima.
Sababu ya pili ni kwamba ulimwengu mzima ulifikiri nilianza uharamia [nchini Somalia] na hiyo kwamba uliniathiri vibaya. Sikulifurahia hilo kwa sababu jambo la aibu na baya lilitokea.

Sabahi: Ulianzaje kampeni yako ya kupambana na uharamia?

Afweyne: Nilisafiri katika mikoa kadhaa ya pwani ya Mudug na Galgadud na kufanya mawasiliano [kupitia simu] na watu katika maeneo ambayo sikuweza kuyatembelea ambayo yalikuwa yanadhibitiwa na al-Shabaab. Nilikutana na wazee, wahubiri wa dini na viongozi wa maharamia, ambapo niliwaambia wazo la kuachana na uharamia. Nilifanikiwa.

Sabahi: Ni watu wangapi vijana umewashawishi kuachana na uharamia hadi sasa?

Afweyne: Tumewashawishi 1,023 kuachana na uharamia. Hawa wanajumuisha baadhi ambao wameshawishika kwamba uharamia sio mzuri [na wamerudi kujihusisha katika jamii zao] na baadhi ambao [wanafanyiwa urekebishaji tabia] katika makambi. Matokeo yake, mashambulizi katika fukwe ya Mudug na Galgadud yametokomezwa.
Sabahi: Sasa tunaweza kusema uharamia umekwisha?

Afweyne: Ndiyo, tunaweza kusema hivyo kwa sababu katika miaka miwili iliyopita ambayo nilikuwa nikijihusisha katika kazi hii hakukuwa na shambulio [katika maeneo hayo].
Sabahi: Je, kituo cha shughuli zenu kiko wapi?

Afweyne: Kituo cha shughuli zetu kiko Mogadishu. Jina la Kampuni yetu ni Shirika la Kuzuia Uharamia la Somalia. Tunatambulika na serikali na hakuna maeneo yaliyozuiliwa kwetu. Tunawasiliana na vijana mahali popote walipo ili kuwasaidia.

Sabahi: Nani anayegharimia kazi zenu?
Afweyne: Ninakusanya fedha kutoka kwa wafanyabiashara wa Somalia. Gharama zimetunzwa kwa maandishi lakini siwezi kueleza kuhusu kiasi kilichopo sasa.

Sabahi: Ni aina gani ya nyenzo mnazotumia kukabiliana na uharamia? Je, mnajishughulisha na mashambulizi ya kutumia silaha ili kukabiliana nao?

Afweyne: Hatupambani kuua lakini kubadilisha mawazo. Hii ni kampeni ya kujitambua, na tunaahidi [wale walioacha uharamia] kwamba tutawajali.

Sabahi: Je, una ujumbe gani kuhusu uharamia?

Afweyne: Ninatoa wito kwa vijana ambao bado wanajihusisha na shughuli hii kuacha na kujiunga wao wenyewe na zoezi la kukabiliana na uharamia na kuwaachia mateka wao, kwa sababu ni kitu kibaya sana kuwateka binadamu na kujaribu kupata [fedha za fidia] kutokana na mateka.
Hii sio nzuri kwa ubinadamu, Uislamu wala utamaduni wa Kiislamu. Ninatoa wito pia kwa serikali kuwasamehe vijana wanaoacha uharamia.

SOURCE: SABAHIONLINE.COM