Wednesday, 9 October 2013

Wakimbizi wa Somalia walalamikia wito wa kufungwa kwa kambi za wakimbizi Kenya

Na Bosire Boniface, Garissa
Oktoba 08, 2013
Saadia Ahmed Hussein, mwenye umri wa miaka 42, alisema kwamba wakimbizi wa Somalia wanaoishi katika kambi za wakimbizi Kenya wanapaswa kuachiwa kurejea nyumbani kwa hiari yao na "wakiwa na kumbukumbu nzuri".

Mwanaume wa Kisomali akijaribu kuingia katika kituo cha usajili katika kambi ya Dagahaley kwenye majengo ya kambi kuu ya wakimbizi ya Daadab nchini Kenya tarehe 24 Julai, 2011. [Na Phil Moore /AFP]
Hussein aliondoka Somalia mwaka 1993 na sasa anaishi katika kambi ya Hagadera katika majengo ya kambi kuu ya Daadab kaskazini mashariki mwa Kenya. Daadab ni makazi ya kiasi cha watu 390,000, wengi wao wakiwa ni Wasomali ambao wamekuwa wakiishi hapo kwa zaidi ya miaka ishirini. 

"Ninashukuru kwa makaribisho ambayo sisi kama Wasomali tulipata, [lakini] ninataka zaidi kurejea nyumbani," aliiambia Sabahi. "Nilifika Kenya nikiwa na kumbukumbu mbaya baada ya kupoteza wanafamilia wanne wakiwemo wazazi wangu wote wawili katika vita, lakini nataka kurejea huko nikiwa na kumbukumbu nzuri."

Hussein alisema kuwa wito unaotolewa na baadhi ya maafisa wa serikali ya Kenya kwa ajili ya kufungwa kwa kambi za wakimbizi juu ya wasiwasi kwamba majengo hayo yanatumika kama "viwanja vya mafunzo" vya magaidi ni kwa nia mbaya. 

"Sio kitu kizuri kuwa katika kambi, na wengi wetu tumekuwa tukisubiri kwa shauku siku ambayo tutarejea nchi kwetu na kujenga upya maisha yetu," alisema, na kuongeza kwamba serikali ya Kenya hawana haja ya kuwatoa wakimbizi nje ya kambi kwa nguvu. 

Alisema kuwa idadi kubwa ya wakimbizi ni watu wanaofuata sheria.
"Tunahisi uchungu wa Kenya [juu ya ugaidi] kwa sababu inatuathiri sisi moja kwa moja," alisema. "Lakini wakimbizi walio wengi hawapaswi kuteseka kwa watu wachache wapotofu ambao wamejiunga na al-Shabaab."
Yusuf Mukhtar Abdille, mwenye umri wa miaka 45 ambaye pia anaishi katika kambi ya Hagadera, alisema kwamba ikiwa serikali itafunga kambi ya Daadab hilo litakuwa pigo mara mbili kwa wakimbizi ambao walilazimishwa kuondoka katika maeneo ya mjini mapema mwaka huu.

"Mwezi Juni nilizingatia wito wa serikali wa kuondoka mji wa Garissa kufuatia maelekezo ambayo yaliwataka wakimbizi wote wanaoishi maeneo ya mjini kurejea katika kambi [walizopangiwa]," aliiambia Sabahi.
"Bado hata sijakaa vizuri na sasa serikali inataka kuzifunga kambi," alisema. "Kwa wito huu mpya, inaelekea kwamba maelekezo ya serikali ya kututoa katika maeneo ya mjini hayakuwa nia njema."
Kufuatia shambulio la al-Shabaab katika jengo la biashara la Westgate mjini Nairobi, mkuu wa kamati ya ulinzi ya bunge Ndung'u Gethenji alitoa wito wa kufungwa kwa makambi.

Kenya lazima ifikirie mara mbili "ukarimu wake wa kuzisaidia kambi za wakimbizi ndani ya mipaka yetu," Gethenji alisema hapo tarehe 30 Septemba.

Katika kujibu hilo, shirika la Amnesty International liliukosoa wito wa serikali wa kufunga kambi za wakimbizi, kwa kusema haijafikia kiwango cha usalama ambacho kinahalalisha kurejea wakimbizi kwa kiwango kikubwa.

"Kenya ipo katika ulazima wa kuwalinda wale wanaotafuta hifadhi katika ardhi yake. Kanuni hii ni msingi wa mfumo wa kimataifa wa ulinzi na haiwezi kukiukwa," alisema Naibu Mkurugenzi wa Amnesty International kwa Afrika Sarah Jackson.

"Kuwarejesha wakimbizi Somalia, ambako pande zote ziko katika mzozo, ikiwa ni pamoja na al-Shabaab, kuendelea kufanya mashambulizi dhidi ya wananchi, kungeyafanya mambo kuwa mabaya zaidi na kungekuwa ni ukiukaji wa sheria ya kimataifa," alisema. 

Hata hivyo, Gethenji akashikilia msimamo wake, kwa kusema kwamba kufunga kambi kungekuwa moja ya njia za kushughulikia mashambulizi ya ghafla ya kigaidi nchini. 

"Makambi yamepitiliza madhumuni yake," Gethenji aliiambia Sabahi. "Hivi sasa yanaandikisha, kuficha na kuwa viwanja vya mafunzo kwa magaidi. Kwa hali yoyote ile, kambi hizi zilikusudiwa kuwa hatua za muda mfupi." 

Alisema kwamba kamati yake ingeamua hali hiyo zaidi kabla ya kuifikisha kesi bungeni ndani ya mwezi Oktoba.
"Tulikuwa na fursa kadhaa za kuyafunga makambi haya huko nyuma lakini kila mara kumekuwa na wito wa kutoa muda zaidi," alisema.

Lakini aliyekuwa Naibu Spika wa bunge la Kenya Farah Maalim Mohamed alisema kwamba serikali haipaswi kuharakisha kufunga makambi wakati bado mazungumzo yanaendelea juu ya utaratibu mzuri wa kuwahamishia wakimbizi.

Maalim, ambaye aliwakilisha jimbo la uchaguzi la Kaunti ya Garissa ambako majengo ya wakimbizi yanafika, alisema mchakato wa haja za kuwarejesha kuhakikisha katika mpito wa taratibu.
"Wale wanaoomba kufungwa kwa makambi za wakimbizi sio wajuzi wa ulinzi wa kimataifa ambao uko katika kambi za wakimbizi," Maalim aliiambia Sabahi." Itakuwa sio kama kufunga makambi ya watu waliokimbia makazi yao. Jumuiya ya kimataifa lazima ihusishwe na lazima iwe kwa hiari ya mtu."

SOURCE: SABAHIONLINE.COM