Imebadilishwa: 10 Septemba,
2013 - Saa 14:31 GMT
Ufaransa inajiandaa kuwasilisha azimio kwa baraza la usalama la
umoja wa Mataifa kulitaka kuziweka silaha za kemikali za Syria chini ya udhibiti
wa jamii ya kimataifa ili ziweze kuharibiwa.
Hii ni kwa mujibu wa waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo Laurent
Fabius.Alisema kuwa azimio hilo huenda likaja na adhabu kali sana kwa Syria ikiwa itakataa kutii masharti yake.
Hatua ya Ufaransa inakuja baada ya tangazo la mpango wa kutaka silaha hizo kudhibitiwa na nchi za magharibi.
Hata hivyo Syria imesema kuwa haikatai pendekezo la Urusi ingawa hakuna maelezo zaidi kuhusu pendekezo hilo.
Awali bwana Fabius, aliyetoa kauli yake kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Paris, alisema kuwa azimio hilo lenye vipengee vitano, litapendekeza kuwa Syria ieleze bayana kuhusu silaha zake za kemikali.
Hatua hiyo pia itaruhusu wachunguzi wa kimataifa kuziona silaha hizo pamoja na kuziharibu.
Azimio lenyewe litawasilishwa chini ya sura 7 ya mkataba wa UN inaozungumzia hatua za kijeshi na hatua zinginezo zisizo za kijeshi kutumika kurejesha amani Syria.
Mpango huo ulijadiliwa siku za nyuma lakini ukapewa kipaumbele kutokana na shinikizo zilizotolewa hivi karibuni.
Serikali ua Urusi imezuia juhudi zote za Ufaransa katika baraza la usalama la umoja wa mataifa dhidi ya Syria.
source: BBC Swahili