Na Pamela Chilongola, Mwananchi
Posted Jumatatu,Septemba23 2013 saa 11:19 AM
Posted Jumatatu,Septemba23 2013 saa 11:19 AM
Kwa ufupi
Wananchi hawajui kwa nini viongozi wa Serikali wakiwemo polisi wanashindwa kupiga marufuku biashara hiyo.
Dar es Salaam. Tatizo la ukahaba linaonekana kukua nchini, likiwemo Jiji la Dar es Salaam, kwa watu kufanya vitendo hivyo kwa staili tofauti.
Huku baadhi ya watu wakidaiwa kufanya ukahaba
ofisini kwa kuvaa mavazi yasiyo na staha, kwa lengo la kuwawinda
wanaume, baadhi yao wanajiuza waziwazi mitaani hasa nyakati za usiku,
achilia mbali wale wanaojiuza mchana kwa kusimamisha watu na kujifanya
wanaomba msaada au lifti za magari kisha anaomba namba ya simu.
Ahadi nyingi zimetolewa na Serikali kuhusiana na
kukomesha biashara hii chafu, bila mafanikio, huku swali kuu likiwa ni
nani hasa wananunua makahaba?
Utafiti unaonyesha kuwa wanunuzi wakuu wa makahaba
ni watu wenye hali ya wastani kimaisha, wakiwemo waume za watu, huku
baadhi ya wale wanaojiuza ni wake za watu. Sababu kubwa ni migogoro
katika ndoa, tabia tu za mtu mwenyewe kupenda ngono na matatizo mengine
ya kiafya na kiuchumi.
Biashara haramu hadharani
Ni jambo la kushangaza, lakini ndicho
kinachozungumzwa kwamba kuna madanguro yameanzishwa katika baadhi ya
mitaa ya jiji la Dar es Salaam, watu wazima pia wakiwemo watoto
wanajiuza.
Madanguro hayo yaliyopo eneo la Buguruni Madenge
imedaiwa kuwa ni chanzo cha watoto hasa wa kike kuacha shule na
kujiingiza kwenye ukahaba.
Jumla ya madanguro 15 yenye vyumba 170 yapo eneo
hilo la Buguruni Madenge, huku yakitishia kuharibu mwelekeo wa watoto
wanaoishi jirani na madanguro hayo hasa baada ya kuonekana baadhi yao
kujiingiza kwenye ukahaba. Wakazi wa eneo hilo sasa wameonya kwamba
watachukua hatua za kuyafunga madanguro hayo, baada ya kile wanachosema
kwamba Serikali ni kama haitaki kufanya hivyo.
Wametangaza kuwa kabla ya mwisho wa mwezi huu,
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala ayafunge madanguro hayo,
asipofanya hivyo wataandamana kuelekea kwenye ofisi ya Kamanda huyo,
huku wengine wakisisitiza kwamba watayafunga kwa nguvu.
Wananchi waandamana
Hivi karibuni baadhi ya wakazi wa eneo hilo
waliandamana hadi kwenye ofisi ya Serikali ya mtaa wao huo,
wakiushutumu uongozi wa Serikali hiyo kwa kushirikiana na baadhi ya
Polisi, kwa kile walichodai kwamba kuna mazingira kama vile wanapokea
rushwa kutoka kwa wamiliki wa madanguro hayo ili yasifungwe.
“Sitaki kuamini kama kweli Serikali au polisi
hawajui kinachoendelea kwenye madanguro haya. Hata kama hawajui, kwanini
tunapolalamika kwenye vyombo vya habari kama hivi hakuna hatua za maana
zinazochukuliwa,” anahoji Thadei Hamdani. ITAENDELEA KESHO
SOURCE: MWANANCHI