*Uamuzi wa Mahakama ya Rufaa wapuuzwa na viongozi
*Wanaopinga kuhama wabambikiwa kesi mahakamani
*Mwanamke afungwa miezi 6 jela, mtoto alelewa na bibi
Wananchi
kadhaa katika eneo la Maramboi, Kijiji cha Vilima Vitatu, Wilaya ya
Babati mkoani Manyara, hawana makazi baada ya nyumba zao kuchomwa moto
ili kumpisha mwekezaji raia wa Ufaransa.
Waliofikwa na maafa hayo ni Watanzania wafugaji wa jamii ya
Kidatoga. Kampuni ya Kifaransa ya Un Lodge En Afrique Limited (ULEA),
imepewa kinyemela ardhi ya wafugaji hao ili kuendesha shughuli za utalii
kupitia Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ya Burunge.
Kampuni
hiyo inamilikiwa na Nicolas Negre (hisa 99) na Stephanie du Marroussem
ambaye ana hisa moja. Raia hao wawili pia ndiyo wakurugenzi wa kampuni
hiyo wakiwa na mwenzao, Antonio Haji ambaye ni raia wa Uswisi.
Wazungu
hao wanakilipa kijiji dola 5,000 (Sh milioni 8) kwa mwaka. Kuchomwa kwa
makazi ya wananchi hao kumefanywa licha ya kuwapo hukumu ya Mahakama ya
Rufani iliyotamka bayana kuwa Kampuni ya ULEA ipo eneo hilo kinyume cha
sheria na hivyo wananchi waachwe waendelee na maisha yao kama kawaida.
Hata
hivyo, ULEA imefanikiwa kuwatumia viongozi kadhaa wa kijiji, wilaya na
Mkoa wa Manyara kuwaminya wananchi hao na kupuuza amri halali ya
Mahakama ya Rufani. Wakili mwakilishi wa wananchi hao, Mayomba Duncan,
akiwa na baadhi ya wananchi hao, alizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam, mwishoni na wiki na kusema wananchi hao wanahitaji
msaada wa haraka wa chakula na makazi.
“Nia
ni kuwaeleza ninyi (waandishi wa habari), na umma wa Tanzania uvunjaji
mkubwa wa Katiba na sheria za nchi yetu, ukiukwaji mkubwa wa haki za
binadamu na kiraia, na kutotekelezwa kabisa kwa dhana ya utawala bora na
utawala wa sheria kwa kuachia vyombo vyenye mamlaka ya kutekeleza
sheria kuingilia uhuru na uamuzi wa Mahakama,” alisema Mayomba.
Historia ya mgogoro
Makazi
ya wanajamii wa Kidatoga na maboma yao yalichomwa moto na watu
wanaosemekana hawajulikani asubuhi ya Septemba 4, mwaka huu. Uchomaji na
uharibifu mkubwa wa mali ulitokana na ushindi wa kesi ya madai ya ardhi
iliyofunguliwa na Halmashauri ya Kijiji cha Vilima Vitatu, na WMA ya
Burunge, dhidi ya wanajamii ya wafugaji ya Wadatoga waishio katika eneo
la Maramboi wakiongozwa na Mama Udaghwenga Bayay na wengine 16.
Shauri
dhidi ya wanajamii hao lilifunguliwa kwa mara ya kwanza katika Baraza
la Ardhi na Nyumba Mkoa wa Manyara-Babati-na lilisajiliwa kama Maombi
Na. 70 ya Mwaka 2008. Ufunguzi wa shauri hilo ulitokana na uamuzi wa
Mkutano wa Kijiji cha Vilima Vitatu wa Desemba 4, 1999 uliotenga eneo
wanaloishi wanajamii hao kwa ajili ya malisho ya mifugo na wanyamapori.
Uamuzi huo wa kijiji uliwezesha kuanzishwa kwa Burunge WMA mwaka 2004.
Uamuzi
wa Mkutano Mkuu wa Kijiji wa mwaka 1999 ulipingwa vikali na Mkutano
Mkuu uliofuata wa kijiji hicho hicho ulioitishwa Mei 10, 2006. Katika
Mkutano huo, kijiji kilipinga kuanzishwa kwa Burunge WMA kwa maelezo
kwamba lengo lake lilipotoshwa, na kwamba wanakijiji wakazi
hawakushirikishwa, bali viongozi wachache kwa kushinikizwa na Afisa
Wanyamapori wa Wilaya.
Baada
ya uamuzi huo wa kijiji, Mwenyekiti wa Kijiji, Belela Erasto,
alimwandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Wanyamapori mnamo Mei 12,
2006 akimweleza Mkurugenzi wa Wanyamapori kuhusu uamuzi wa kijiji wa
kujiondoa kwenye WMA na JUHIBU (yaani Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori
Burunge). Uamuzi uliotolewa baada ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori
kupokea barua hii ya Kijiji haujulikani.
Pamoja
na pingamizi zote za uanzishwaji wa Burunge WMA, na pingamizi za kutoa
ardhi ya kijiji kwa Burunge WMA, Februari 23, 2007 Burunge WMA iliingia
mkataba wa uwekezaji katika eneo la Burunge WMA na Kampuni ya Kifaransa
ya Un Lodge En Afrique Limited (ULEA). Katika mkataba huo, Burunge WMA
walitoa haki yote ndani ya eneo la Burunge WMA kwa ULEA ili kuiwezesha
ULEA kuendesha biashara ya kambi na matembezi ya kitalii kwa muda wa
miaka mitatu.
Katika
mkataba huo, moja ya mambo ambayo Burunge WMA ilitakiwa kufanya ni
kuhakikisha kwamba eneo lote la Burunge WMA haliishi watu kwa muda wote
wa mkataba. Hayo yote, na utoaji wa ardhi yote iliyoko ndani ya Burunge
WMA yalifanyika kwa malipo ya dola elfu tano tu za Marekani kwa mwaka!
Mkataba
huo pia uliainisha bayana kwamba uwekezaji wowote na maendeleo yoyote
ndani ya WMA inayohusu utumiaji na ukazi katika ardhi utatakiwa kufuata
Sheria za Ardhi ya Vijiji ya mwaka 1999. Hilo halikufuatwa, na badala
yake uvunjifu mkubwa wa Sheria za Ardhi ulifanyika.
Kutokana
na kuingia kwa mkataba huo, Aprili 11, 2008 uongozi wa Kijiji cha
Vilima Vitatu na uongozi wa Kata ya Nkaiti ulikutana na Mkuu wa Wilaya
ya Babati kujadili taarifa ya mpango wa matumizi bora ya ardhi. Katika
taarifa hiyo pungufu mbalimbali ziliainishwa, na kikao kikahamia eneo la
Maramboi ambako wanajamii hao wanaishi. Katika eneo la Maramboi, kikao
kilikutana na wanajamii 84 waishio Maramboi, na kuwataarifu kuwa eneo
hilo limetengwa kwa ajili ya malisho na wanyamapori na si eneo la
makazi. Wakaelezwa utaratibu wa uhamiaji kutoka kijiji kimoja kwenda
kingine.
Mkuu
wa Wilaya ya Babati alitoa maelekezo kuwa mwekezaji amepewa ekari 45 tu
ambazo ataweka kambi ya kulaza wageni wa kitalii, na kuwaagiza kuwa
wale wote waliojenga katika eneo la mwekezaji waondoke mara moja na
wapewe maeneo mengine katika eneo la Mfulu wa Ng’ombe na maeneo mengine
hapo hapo Maramboi. Wafugaji 17 waliainishwa kuwapo ndani ya eneo la
mwekezaji.
Mkutano
huo na Mkuu wa Wilaya ulifuatiwa na mkutano mwingine Mkuu wa Kijiji wa
Aprili 14, 2008 uliohudhuriwa na watu mbalimbali akiwamo Luteni Kanali
mstaafu Werema akiiwakilisha ULEA kutoka Arusha. Kichojadiliwa katika
Mkutano huo Maalum ni eneo la mwekezaji. Kijiji kiliazimia kuwa
mwekezaji apokewe, na kwamba familia 17 za wafugaji waishio ndani ya
eneo la mwekezaji waondoke mara moja na kupewa maeneo mengine ya kujenga
makazi yao .
Uamuzi
huo ulirudiwa na uongozi wa kijiji katika taarifa yake kwa Mkuu wa Mkoa
wa Manyara ya Aprili 21, 2008. Cha kushangaza ni jinsi kijiji, chini ya
uongozi wa Mwenyekiti Belela Erasto, kilivyobadili uamuzi wake wa mwaka
2006 na kuamua kurudia tena Burunge WMA.
Wananchi wafunguliwa kesi
Baada
ya uamuzi huo, yaliyofuata ni kwa wanajamii wa Kidatoga kufunguliwa
kesi za jinai, zikiwamo za uvunjaji, wizi wa fedha taslimu, wizi wa
baiskeli, na wizi wa shati; mali zilizodaiwa kuwa za mwekezaji au
wafanyakazi na wapambe wake. Katika kesi nyingine, wanajamii hao hao
walishitakiwa kwa kutishia kumpiga mmoja wa wafanyakazi wa mwekezaji.
Mashauri
hayo yalifunguliwa katika Mahakama ya Mwanzo Magugu. Baada ya wakili wa
Kampuni ya F K Law Chambers kuingilia, yalihamishiwa Mahakama ya Wilaya
Babati. Mashauri yote mawili yaliishia kwa wanajamii hawa kuachiwa huru
kwa kukosekana ushahidi.
Wakati
mashauri hayo ya jinai yakiendelea, Mei 9, 2008 Halmashauri ya Kijiji
cha Vilima Vitatu na Burunge WMA walifungua shauri la madai ya ardhi
katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya, Mkoa wa Manyara - Maombi
Namba 70 ya mwaka 2008 – dhidi ya wanajamii 17 wanaodaiwa kuwa ndani ya
eneo la mwekezaji wakiongozwa na mama Udaqwenga Bayay.
Wanajamii
walipoteza shauri hilo katika Baraza la Ardhi na, kwa kutoridhika,
walikata rufani Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi. Rufaa yao
ilisikilizwa na Jaji Ngwala. Akaitupilia mbali. Kwa kutoridhika,
wanajamii walikata rufani katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania, ambacho
ni chombo cha mwisho cha utoaji haki nchini.
Mahakama ya Rufani yatenda haki
Machi
15, 2013 jopo la majaji watatu, wakiongozwa na Jaji Msoffe, Jaji Sauda
Mjasiri, na Jaji Profesa Ibrahim Juma, walitoa uamuzi uliowapa ushindi
wanajamii hao. Katika uamuzi wao, Majaji wa Mahakama ya Rufani waliweka
bayana kwamba:
(i)
Katika utoaji na ugawaji wa ardhi kwa Burunge WMA, kijiji hakikufuata
maelekezo ya Sheria kwa maana ilikuwa lazima kwa wajibu rufani
(Halmashauri ya Kijiji cha Vilima Vitatu na Burunge WMA) kuonesha kwa
ushahidi kwamba kijiji kiligawa ardhi kwa Burunge WMA kwa kufuata
taratibu zilizoainishwa na Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori kabla kesi
dhidi ya wanajamii haijaamuliwa; na
(ii)
Kwa kuangalia taarifa zilizokuwa mbele ya Mahakama ya Rufani,
hakukuwa na Information Data Sheet na Land Use Plan ambavyo ni muhimu
katika maombi ya kufanya eneo husika kuwa eneo la hifadhi ya
wanyamapori. Kwa maana hiyo, kifungu cha 13 cha Sheria ya Uhifadhi wa
Wanyamapori kilikiukwa.
Viongozi wa kijiji, WMA waipuuza Mahakama ya Rufani
Kwa
kuzingatia ukiukwaji wa Sheria ulioainishwa, Mahakama ya Rufani
ilikubali rufaa ya wanajamii na kutaka Kijiji cha Vilima Vitatu na
Burunge WMA kulipa gharama zote za kesi. Wanajamii, walipeleka maainisho
ya gharama za kesi na kuomba Mahakama, kupitia Baraza la Ardhi la
Wilaya, kukaza hukumu ya Mahakama ya Rufani. Wakati haya yakisubiriwa,
uvunjifu wa haki za binadamu na kiraia, vilianza. Licha ya kukiuka haki
za binadamu na utawala bora, uamuzi wa Mahakama ya Rufani ulipuuzwa
kuanzia hapo.
Halmashauri
ya Kijiji cha Vilima Vitatu, pamoja na Burunge WMA, badala ya
kutekeleza na kufuata maelekezo yaliyotolewa kwenye hukumu ya Mahakama
ya Rufani, waliitisha vikao mbalimbali kujadili hukumu hiyo na kutoa
uamuzi unaopingana na hukumu ya Mahakama ya Rufani.
Waliamua yafuatavyo:
(i)
Walipitisha uamuzi wa kumgawia tena mwekezaji eneo la ardhi lenye
ukubwa wa ekari 45 likizungukwa na eneo la kilometa moja kila upande,
yaani jumla ya kilometa za mraba zaidi ya nne na ekari 45; na
(ii)
Walipitisha uamuzi wa kuwaondoa kwa nguvu, na kuwachomea nyumba
wanajamii ya kifugaji kinyume na uamuzi wa Mahakama ya Rufani. Uamuzi
ulifanywa katika vikao rasmi na visivyo rasmi ndiyo uliosabababisha
kuchomwa moto kwa nyumba za wafugaji hao.
Sheria zilivyovunjwa
Sheria
ya Ardhi hairuhusu kijiji kugawa ardhi inayozidi ekari 50 kwa mtu
yeyote yule. Mwekezaji katika Kijiji cha Vilima Vitatu amepewa haki juu
ya ardhi inayozidi kiasi kilichainishwa kisheria
Utafiti
uliofanywa katika ofisi ya Msajili wa Kampuni nchini (BRELA), Kampuni
ya Un Lodge En Afrique Limited ni kampuni ya kigeni iliyosajiliwa
Tanzania, na ambayo hisa zake zote zinamilikiwa na wageni wawili –
Nicolas Negre (hisa 99), na Stephanie Planteau Du Marroussem (hisa 1) –
wote wakiwa raia wa Ufaransa. Sheria za Ardhi haziruhusu mtu asiye raia
wa Tanzania kumilikishwa ardhi isipokuwa tu kama ardhi hiyo itatolewa na
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa ajili ya uwekezaji pekee. ULEA
amemilikishwa ardhi na Kijiji cha Vilima Vitatu na kupewa haki juu ya
ardhi ya Burunge WMA kinyume cha Sheria ya Uwekezaji na Sheria za Ardhi.
Kwa
mujibu wa kifungu cha 107A cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mahakama inatamkwa kuwa ndiyo mamlaka yenye kauli ya mwisho ya
utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mahakama ya Rufani –
ambacho ndicho chombo cha mwisho cha utoaji haki katika Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania – imeshatamka bayana kwamba Burunge WMA haikuwa
imeanzishwa kwa kufuata sheria na taratibu, na kwamba ardhi iliyopewa na
Kijiji cha Vilima Vitatu haikupewa kihalali na ilikiuka misingi ya
Sheria.
Kwa
hukumu hiyo ya Mahakama ya Rufani, mkataba uliowekwa kati ya Burunge
WMA na mwekezaji wa ULEA ni batili. Kitendo cha Burunge WMA na kijiji
kuendelea kukumbatia, jambo ambalo tayari Mahakama imetamka kuwa ni
batili, ni kitendo cha kuvunja Katiba ya nchi yetu na kinaonesha dharau
kubwa na udhalilishaji kwa Mahakama.
Wananchi wateswa, wabambikiwa kesi
Kabla
na baada ya uchomaji nyumba, wananchi hao wamekuwa wakifunguliwa kesi
mbalimbali za jinai, kuwekwa kizuizini, na kuhukumiwa kwa makosa ya
kutungwa. Kwa sasa, tayari kesi kadhaa zimefunguliwa dhidi yao katika
Mahakama ya Mwanzo Magugu, Wilaya ya Babati. Miongoni mwa kesi hizo ni:
(i)Shauri la Jinai Namba 112/ 2013 – Mshitakiwa: Ghinyanga Gidamajod na Mabee Giyamu. Mabee ni mtoto wa Giyamu Marish.
(ii)
Shauri la Jinai Namba 174/2013 – kati ya Lekshon Laiza na Gaudence
Diwani. Huyu Gaudence ni kijana wa chini ya umri unaoruhusiwa
kushitakiwa katika Mahakama za kawaida, lakini alishahukumiwa kifungo
cha miezi sita jela bila faini. Kwa sasa ametoka baada ya kukata rufaa
na kuweka wakili.
(iii)
Shauri la Jinai Namba 264 la 2013 – mshitakiwa Bujaji Gisima. Huyu ni
mzee wa miaka 70 na alishatumikia kifungo cha miezi sita jela. Yupo nje
kwa sasa.
(iv) Shauri la Jinai Namba 268/2013 – mshitakiwa, Wakim Giyamu. Huyu ni kijana wa Giyamu Marish. Kesi yake bado ipo mahakamani.
(v)Shauri
la Jinai Namba 273/2013 – mshitakiwa Dagabonga Mabe. Huyu ni mke wa
Mabee Giyamu – mwenye Shauri la Jinai Namba 112/2013. Mama huyu
alihukumiwa miezi sita jela bila faini, na ametumikia kifungo akimwacha
mtoto wake mchanga wa miezi sita tu akiwa na nyanya yake.
(vi)
Shauri la Jinai Namba 277/2013 – mshitakiwa Bukuchan Giyamu. Huyu ni
mke wa Giyamu Marish. Kwa hiyo, katika familia hii mama, kijana wake na
mkwewe; wote wanashitakiwa au wameshahukumiwa na kutumikia vifungo.
(vii)
Shauri la Jinai Namba 278/2013 – mshitakiwa Kipara Giyamu – huyu pia ni
mtoto wa Giyamu Marish ambaye shauri lake linaendelea .
(vii) Shauri la Jinai Namba 422/ 2013 – mshitakiwa, Saidi Qamunga. Shauri lake linaendelea.
(ix) Shauri la Jinai Namba 423/2013 – mshitakiwa Julius Nduruu. Shauri hili linaendelea.
(x) Shauri la Jinai Namba 424/2013 – mshitakiwa Goerge Sikarika. Shauri linaendelea mahakamani.
Familia
moja tu ya Mzee Giyamu Marish inakabiliwa na kesi nne – moja dhidi ya
mama yao, mbili dhidi ya watoto wao, na moja dhidi ya mke wa mtoto wao.
Ukimya wa viongozi wa Serikali
Mkuu
wa Mkoa wa Manyara, Erasto Mbwilo, bado hajachukua hatua za kuhakikisha
wawekezaji na viongozi wengine wanaheshimu uamuzi wa Mahakama ya
Rufani.
Hata
hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Hanang’ ambaye amewahi kukaimu nafasi kama
hiyo katika Wilaya ya Babati, Christina Mdeme, alishatoa msimamo
akiwataka viongozi wa WMA na kijiji waheshimu uamuzi wa Mahakama ya
Rufani.
Alisema
kama Mahakama ya Rufani imewaona wananchi hao wana haki, waachwe
waendelee kuishi hapo, na kwamba uamuzi wa aina hiyo hauhojiwi.
Wakati
huo Mkuu wa Wilaya ya Babati, Khalid Mandia, alikuwa mgonjwa.
Aliporejea ofisini akaendelea na msimamo wa kuwataka wananchi hao
waondolewe ili kumpisha mwekezaji.
Katika sakata hili, uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa Mandia na Mbwilo wapo upande wa mwekezaji.
SOURCE: JAMHURI MEDIA
|