Wednesday 9 October 2013

Polisi, Sumatra wafanikiwa kusitisha mgomo wa mabasi

Baadhi ya Abiria wakiwa wamesimama nje ya Mabasi jana katika Kituo cha Mabasi Ubungo kabla ya kuanza kwa safari kutokana na mgomo wa mabasi yaendayo mikoani na nchi za jirani uliosababisha adha kwa wasafiri hao, Mgomo huo ulikuwa unaishinikiza Serikali kupunguza ghalama za ongezeko la tozo katika Mizani. Picha na Venance Nestory
Na Venance Nestory
Posted  Jumanne,Oktoba8  2013  saa 17:26 PM

Kwa ufupi

    “Kwa kawaida mabasi yaendayo mikoani na nchi za jirani huanza safari kuanzia saa 12 asubuhi lakini kwa leo hali imekuwa tete na imetulazimu kufika sehemu ya tukio kujionea hali halisi na kuzungumza na baadhi ya madereva kujua nini chanzo cha mgomo.

Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) waliwabana na kuwalazimisha madereva wa mabasi yaendayo mikoani na nchi za jirani hadi wakasitisha mgomo wao kwenye Kituo cha Mabasi cha Ubungo jijini Dar es Salaam.

Wamiliki wa mabasi walitangaza kutosafirisha abiria mapema leo asubuhi ili kushinikiza kufutwa kwa msamaha wa tozo kwenye mizani kwa uzito wa magari uliozidi ndani ya asilimia tano ya ule unaokubaliwa kisheria.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga aliingilia kati suala hilo kwa kuwataka  wenye mabasi kusitisha mgomo huo kwani wasingekuwa wamewatendea haki abiria, ambao tayari walikuwa wamenunua tiketi kwa ajili ya safari za leo asubuhi.

Alisema kuwa mgomo huo ni batili na haukufuata taratibu na kuwataka madereva kuwapeleka abiria kama kawaida.

“Kwa kawaida mabasi yaendayo mikoani na nchi za jirani huanza safari kuanzia saa 12 asubuhi lakini kwa leo hali imekuwa tete na imetulazimu kufika sehemu ya tukio kujionea hali halisi na kuzungumza na baadhi ya madereva kujua nini chanzo cha mgomo.

“Kwa maelezo ya awali ya baadhi ya madereva, hawajagoma bali walipokea amri kutoka kwa wamiliki wa mabasi waliowataka wasianze safari kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni kutofikiwa mwafaka katika kikao cha jana baina yao na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.

“Kwa sasa hali ni shwari tumeshafanya mawasiliano na wamiliki wa mabasi na tumekubaliana safari zianze huku baadhi ya viongozi wa Wizara ya Ujenzi na Sumatra wakienda kukutana nao kuzungumzia suala lao,” alisema Kamanda Mpinga.

Mkurugenzi wa Barabara wa Sumatra, Giled Ngewe alisema kama wenye mabasi walitaka kugoma basi walipaswa kutokatisha tiketi.


SOURCE: MWANANCHI