Friday 25 October 2013

Sekta binafsi yaijia juu serikali ugawaji vitalu vya gesi, mafuta

25th October 2013

Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, akizungumza na wajumbe mbalimbali (hawapo pichani) wakati wa kongamano na maonyesho ya pili ya mafuta ya gesi yaliyomalizika jijini Dar es Salaam jana.
Wakati  leo Rais Kikwete akitarajiwa kuzindua ununuzi wa hisa ugawaji vitalu vya mafuta na gesi kwa kampuni mbalimbali zikiwamo zile za ndani na nje ya nchi, sekta binafsi nchini zimeijia juu serikali  kwamba haina ulazima wa kuliharakisha kabla sera ya jinsi ya kuwanufaisha Watanzania ikiwa haijakamilika.

Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam wakati Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), kampuni binafsi na washiriki mbalimbali walipokuwa wakitoa mada na hoja zao kwenye mkutano wa gesi na mafuta.

Mwenyekiti wa TPSF, Dk. Reginald Mengi, alihoji kuwa, serikali itawezaje kutoa vitalu vya gesi na mafuta, bila kuwa na sera.

“Kama serikali haina sera ya kutoa vitalu, je, unauzaje rasilimali za taifa bila ya kuwa na sera? Tusionekane tunauza rasilimali za taifa bila kuwapo kwa sera,” alisema Dk. Mengi.

Dk. Mengi, alisema: “Tanzania ni tajiri, gesi tuliyonayo ndiyo mtaji wenyewe, lakini kusema fedha hazipo, hivyo tuite wageni waje kuwekeza, haiwezekani.
Mtaji  si kile tulicho nacho kwenye mifuko yetu, bali kama wenye akili tunajua ulipo. Fedha zipo kwenye masoko ya fedha.”

Mkurugenzi wa kampuni ya Mansoor Industries Ltd, Alkarim Hirani, alisema mkutano huo umetoa nafasi kwa Watanzania kujua kile kilichokuwa kinaendelea na pia umewafungua na kuhoji kwanini serikali ina uharaka wa ugawaji na ununuzi wa vitalu hivyo.

Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi, alisema sera ya usimamizi wa mafuta na gesi ilishakamilika na kupitishwa Oktoba mwaka huu isipokuwa rasimu ya sera inayolenga kuwashirikisha Watanzania namna ya kunufaika na rasilimali hizo, inatarajiwa kuwekwa hadharani Desemba mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE