Friday 25 October 2013

‘Vyama vya siasa vimebadilika kifikra’

Mwanasheria maarufu, Profesa Chris Peter Maina PICHA|MAKTABA 
Na Fidelis Butahe, Mwananchi

Posted  Alhamisi,Oktoba24  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Mwanasheria mwingine, Berious Nyasebwa alivipongeza vyama hivyo na kusisitiza kuwa uamuzi uliochukuliwa umejaa busara na hekima.


Dar es Salaam. Baadhi ya wasomi jijini Dar es Salaam, wamevipongeza vyama vya siasa kwa kitendo cha kukubaliana kuhusu maboresho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kuifanya Serikali kuandaa hati ya dharura.
Wasomi hao wamesema vyama hivyo vimeonyesha kubadilika kifikra.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, wasomi hao walisema ili nchi iweze kupata Katiba Mpya yenye masilahi kwa nchi husika, lazima wananchi na vyama vya siasa wakubaliane na kuwa kitu kimoja, jambo ambalo limedhihirika juzi.
Mwanasheria maarufu, Profesa Chris Peter Maina alisema, “Vyama vimetoa hoja nzito kuhusu kasoro zilizomo katika sheria husika, pamoja na kuamua kuweka kando tofauti zao na kuungana, binafsi nimependa zaidi hoja zao za msingi zilizolenga masilahi ya taifa kuliko vyama vyao.”
Profesa huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar, alisema hata wabunge wa vyama hivyo wanapaswa kuwa kitu kimoja katika kupitisha mabadiliko hayo.
Mwanasheria mwingine, Berious Nyasebwa alivipongeza vyama hivyo na kusisitiza kuwa uamuzi uliochukuliwa umejaa busara na hekima.
“Hoja hii ya Serikali sidhani kama itapingwa na wabunge ikifika bungeni, wanasiasa wameamua kukubaliana na wametambua wazi kuwa tendo la kuandika Katiba Mpya ni la maridhiano si la mtu binafsi wala chama fulani” alisema Nyasebwa.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Profesa Gaudence Mpangala alisema, “Binafsi nimepata matumaini mapya juu ya mchakato huu baada ya vyama kuamua kuweka kando tofauti zao. Kilichofanyika ni mageuzi ya kifikra.”
Hata hivyo Profesa huyo alisema kulikuwa na ulazima kwa tume hiyo iliyokuwa imalize kazi yake Novemba 1 kuomba kuongezewa muda, kwa maelezo kuwa bado ilihitaji kufanya uchambuzi wa maoni mbalimbali, ili kukamilisha rasimu ya pili ya Katiba.
“Sidhani kama muda ulioongezwa utaathiri mchakato mzima wa Katiba.”

SOURCE; MWANANCHI